Tuesday 30 January 2018

Kiwanja cha Ndege Iringa yaifunga CRDB




Kikosi cha Timu ya soka ya Kiwanja cha Ndege cha Iringa kilichopo eneo la Nduli wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya mchezo wao dhidi ya Benki ya CRDB. Wa kwanza kulia ni Meneja wa Kiwanja hicho, Bi. Hanna Kibopile.

Na mwandishi Wetu
Timu ya soka ya Kiwanja cha Ndege cha Iringa kilichopo eneo la Nduli imewafunga CRDB benki kwa magoli 2-0 katika mchezo wa mashindano ya watumishi wa umma na binafsi yanayofanyika kwenye uwanja wa Lugalo.

Mashindano hayo ya kwanza na ya kuvutia yameanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi.Amina Masenza ili kuwajengea afya na kujenga uhusiano mzuri kati ya umma na binafsi, ambapo magoli ya Kiwanja cha ndege yalifungwa na Mwika Nyangi na Daniel Mtweve.

Timu 23 zinashiriki kwenye mashindano hayo na zimegawanywa katika makundi manne ambapo timu ya Kiwanja cha ndege cha Iringa inaongoza katika kundi lake la C wakijikusanyia pointi sita (6) baada ya kushinda mechi mbili ilizocheza.

Timu nyingine zinazounda kundi C ni pamoja na Benki ya Posta, Iringa DC, Tanesco na IDY DC, wakati kundi ‘A’  linaundwa na RAS, TANROADS, IRUWASA, TRA, Magereza, DIRA timu za kundi ‘B’ ni Veta, Manispaa, Polisi, Kiumaki na Sido na zinazounda kundi ‘D’ ni Zimamoto na vyuo  vya RUCU, Mkwawa, Iringa, na Kleruu.

Hata hivyo bingwa wa mashindano hayo yanayofanyika asubuhi na jioni katika viwanja vya Chuo cha Mkwawa, Kleruu, Lugalo na Kichangani atazawadiwa sh. 350,000, wakati mshindi wa pili atapata 250,000 na watatu sh.200,000 pia kutakua na zawadi nyingine mbalimbali. 

Sunday 28 January 2018

Simba ya Mwendo Kasi Yaichapa Majimaji 4-0

Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Soka Ligi Kuu Tanzania Bara Simba leo imezidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 35 baada ya kucheza mechi 15 na kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa pointi tano zaidi ya Azam FC iliyopo nafasi ya pili. Yanga ambayo juzi iliifunga Azam, ni ya tatu ikiwa na pointi 28.

Simba ilipata bao la kuongoza lililofungwa na John Bocco katika dakika ya 17 baada ya kuunganisha wavuni kona na Shiza Kichuya.

Bocco alifunga la pili katika dakika ya 26 akimalizia kwa kichwa krosi ya Said Ndemla.
Majimaji walinyimwa penalti ya wazi katika dakika ya 19 baada ya Juuko Murshid kumchezea rafu, Geofrey Mlawala lakini mwamuzi akasema ipigwe adhabu ndogo.

Timu hiyo ya Songea ilizinduka na kujaribu kutengeneza nafasi mbili baada ya kulifikia lango la Simba, lakini walishindwa kufunga.

Kilindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko, ambapo ilimtoa Murshid na kumuingiza James Kotei, na kuongeza kasi kwa timu hiyo.

Emmanuel Okwi aliiongezea Simba ushindi baada ya kufunga bao  la tatu katika dakika ya 52 baada ya mabeki wa Majimaji kushindwa kuokoa mpira wa kona uliochogwa na Kichuya.

Okwi alifunga bao la nne likiwa la pili kwake katika dakika ya 68 akipokea pasi safi ya Bocco, ambaye alifanya kazi ya ziada kuwatoka mabeki wa Majimaji kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.

Okwi ameendelea naye kuzidi kujichimbia kileleni katika mbio za kusaka kiatu cha dhahabu baada ya kufikisha mabao 12 hadi sasa.

Vikosi vilikuwa;Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Asante Kwasi, Juuko Murshid/James Kotei, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Emannuel Okwi, Said Ndemla, John Bocco, Shiza Kichuya/Laudit Mavugo na Jamal Mnyate.

Majimaji: Salehe Malande, Lucas Kikoti, Mpoki Mwakinyuke, Kenned Kipepe, Paulo Maona, Hassan Hamisi, Peter Mapunda, Yakubu Kibiga, Geofrey Mlawa/Six Mwasekaga, Maccel Bonaventure na Jafar Mohamed.


Katika mchezo mwingine, Singida United jana walishinda bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Namfua, Singida.

Roger Federer Bingwa US Open 2018 kwa Wanaume

MELBOURNE, Australia
ROGER Federer leo ametwaa taji lake la sita la Australian Open na la 20 kubwa baada ya kushinda seti tano dhidi ya Marin Cilic.

Mswisi huyo alipoteza mechi tano mfululizo wakati akipoteza seti ya nne, lakini aliibuka na kushinda kwa 6-2 6-7 (5-7) 6-3 3-6 6-1.

Federer, mwenye umri wa miaka 36, amekuwa mchezaji wanne baada ya Margaret Court, Serena Williams na Steffi Graf kushinda mataji makubwa 20 au zaidi kwa mchezaji mmoja mmoja.


"Ni ndoto imetimia baada ya kufanikiwa kutwaa taji hili, “alisema Federer, ambaye ameshinda matatu kati ya mataji matano makubwa.

Bayern Munich Yatoka Nyuma na Kushinda 5-2

BAYERN, Ujerumani
BAYERN Munich imeibuka na ushindi wa mabao 5-2  licha ya kuwa nyuma kwa mabao mawili baada ya dakika 12 na kuifunga Hoffenheim na kuongeza uongozi wake katika Bundesliga na kufika pointi 16 zaidi.

Vinara hao walijikuta wakiwa nyuma kwa mabao yaliyofungwa na Mark Uth na winga wazamani wa Arsenal Serge Gnabry, ambaye naichezea kwa mkopo Hoffenheim kutoka Bayern.

Lakini mabao kutoka kwa Robert Lewandowksi na Jerome Boateng yaliwawezesha wenyeji kuwa sre zikiwazimebaki dakika 25 kabla ya mchezo kumalizika.

Juhudi za Kingsley Coman na Arturo Vidal ziliiweka Bayern Munich kuwa mbele baada ya mapumziko.


Sandro Wagner aliongeza bao la tano kwa vinara hao wa ligi.

Ronaldo Bado Handsome Licha ya Kuumia Usoni

MADRID, Hispania
MCHEZAJI Cristiano Ronaldo anasema kuwa ‘bado ana sura nzuri’ baada ya sura yake kuachwa imejaa damu baada ya kupigwa usoni wakati wakicheza dhidi ya Deportivo La Coruna wiki iliyopita.

Ronaldo alibainisha juzi kuwa bado anataka kubaki Real Madrid licha ya taarifa kuwa hana furaha Hispania.

Picha ilionesha Mreno huyo akijiangalia sura kupitia simu ya mkononi ya daktari wa klabu hiyo wakati akitoka uwanjani akiwa ameumia Jumapili iliyopita kufuatia kugongwa na kupasuka usoni.

Mchezaji huyo ilibidi kushonwa nyuzi tatu juu ya jicho lake wakati akifanyiwa matibabu ya jeraha hilo.

"Wachezaji walinipiga mimi katika mchezo kwa sababu ilibidi wanisimamishe mimi lakini hiyo haikuwa bahati, “alisema Ronaldo katika mahojiano na mtandao wa China wa Dongqiudi.

"Sasa najisikia vizuri, bado nina furaha, bado nina sura nzuri na ninaona vizuri kama mwanzo na hakuna tatizo.”


Ronaldo yuko katika hali mbaya katika soka la nyumbani tangu alipojiunga na Real Madrid akitokea Manchester United mwaka 2009 wakati aliponuliwa kwa rekodi ya dunia ya paui milioni 80 , akifunga mabao sita tu, ingawa anaongoza kwa ufungaji katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Caroline Wozniacki Bingwa Australian Open 2018

MELBOURNE, Australia
CAROLINE Wozniacki amesema kuwa amefurahishwa kwa kuwa sasa hataulizwa tena kuhusu kutopata mataji ya mashindano makubwa baada ya juzi kushinda Australian Open.

Mdenish huyo mwenye umri wa miaka 27, alimchakaza Simona Halep kwa 7-6 (7-2) 3-6 6-4 katika mchezo wa fainali uliofanyika hapa na hatimaye kupata taji lake kubwa la kwanza katika majaribio 43.

Licha ya kumaliza mwaka akiwa katika nafasi ya kwanza duniani mwaka 2010 na 2011, mchezaji huyo alikosa mataji manne makubwa.

"Hata ni mambo mazuri sana kwangu, “alisema Wozniacki.

"Kuanzia sasa kamwe sitaulizwa maswali kama hayo tena. Nasubiri maswali, ‘Lini utakwenda kushinda tajila pili?'

Leo Jumatatu, Wozniacki atarejea kileleni katika viwango vya ubora tangu alipokuwa namba moja kwa mara ya mwisho.

"Ni wazi hilo ni jambo maalum,”aliongeza.

"Nafikiri kuwa bingwa mpya wa mashindano makubwa na bingwa namba moja kwa ubora dunani ni jambo zuri. Nimefurahishwa sana na hilo. Kwa kweli ndoto imetimia.”

Wozniacki ni Mdenish wa kwanza kushinda taji kubwa la mchezaji mmoja mmoja, na kuwa nyuma ya Jana Novotna (45), Marion Bartoli (47) na Flavia Pennetta (49) ambao walishiriki mara nyingi kabla ya kutwaa mataji makubwa.

Pia kwa ushindi huo ameondoka na kitita cha pauni milioni 2.3.


Wozniacki alipongezwa katika mitandao ya kijamii na Serena Williams, ambaye alishindwa kutetea taji lake la Australian Open miezi minne kabla ya kujifugua mtoto wake wa kwanza.

Real Madrid Yaitisha PSG kwa Ushindi wa Mabao 4-1

PARIS, Ufaransa
KLABU ya Real Madrid imechimba mkwara kwa Paris St Germain baada ya kutoa kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Valencia katika mchezo wa La Liga.

Real Madrid itaikaribisha PSG Februari 14 katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya utakaofanyika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabéu.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha siku 280, kocha wa Real Madrid alipanga safu kali ya ushambuliaji iliyowajumuisha kwa pamoja Gareth Bale, Karim Benzema na Cristiano Ronaldo.

Safu hiyo ya ushambuliaji ilianza katika mchezo huo wakati timu hiyo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutolewa katika mashindano ya Kombe la Mfalme dhidi ya timu ndogo ya Leganes.

Valencia iko katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.
Huku Real ikiwa pointi 16 nyuma ya vinara wa La Liga, Barcelona ambayo iko nje ya Kombe la Mfalme, sasa kazi imebaki katika Ligi ya Mabingwa hatua ya 16 bora.

Nacho alisema kuwa timu yao (Real) haina cha kuhofia kutoka kwa vinara hao wa Ligue 1, ambao watawakaribisha katika mchezo wa kwanza.

"Wamekuwa na mwaka mzuri, lakini sisi Real Madrid hatuhofii timu yoyote na tunawea kuifunga timu yoyote ile itakayochea dhidi yetu,”alisema Nacho.

"Mbele yetu kuna changamoto kubwa na tuko vizuri kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.”

Penalti mbili za Cristiano Ronaldo ziliipatia Real Madrid faida kabla ya mapumziko na bao la Santi Mina liliirejesha Valencia katika njia kabla ya mabao ya Marcelo na Toni Kroos.

"Unatakiwa kujua jinsi gani ya kupambana katika mchezo kama huu,”aliongeza Nacho.
"Pointi hizi tatu ni muhimu sana kwetu na zaidi ni na kikubwa ni upande wa saikolojia.”


Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane amekuwa katika kiti moto licha ya timu yake msimu uliopita kutwaa taji la La Liga na kutetea lile la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Kocha wa Simba Aipeleka Sudan Nusu Fainali Chan

CASSABLANCA, Morocco
SUDAN na wenyeji Morocco wametinga nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan 2018) baada ya kushinda mechi zao.

Sudan ambayo inafundishwa na kocha wazamani wa Simba, Zdravko Logarusic (pichani), imetinga nusu fainali baada ya kuifunga Zambia bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Marrakech hapa.

KUJIUNGA NA SIMBA
Baada ya kuondoka Simba, kocha huyo alipewa ofa nono na klabu ya Simba Sports Club ili kuifundisha timu yao.

Alipotua Simba klabu hiyo ilimpatia mshahara mnono pamoja na nyumba eneo la ufukweni mwa Bahari ya Hindi.

Hatahivyo, kwa bahati mbaya, kocha huyo alikuwa hajui Kiswahili na kumfanya kushindwa kuwasiliana vizuri na vyombo vya habari vya Tanzania, ambapo baada ya nusu mwaka alivunjiwa mkataba.

Logarusic alikuwa akiidai Simba kiasi cha Sh milioni 3.6 kutokana na klabu hiyo kuvunja mkataba huku klabu ikidai kuwa eti ni madai ya uongo.

Bao lililofungwa katika kipindi cha kwanza na Malik Saifeldin na kudhihirisha nia yao ya kucheza hatua ya nne bora.

Sudan watacheza nusu fainali ya pili itakayopigwa Jumatano, ama na Nigeria au Angola.

Zambia ambao wanajulikana kama Chipolopolo walifugwa bao hilo pekee katika dakika ya 32 na kufanya Sudan kuwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Hatahivyo, Zambia ilizinduka muda mfupi baadae, baada ya timu hiyo kufanya shambulizi la nguvu baada ya kocha Wedson Nyirenda kumbadili Mwengani na kuingia kiungo Jackson Chirwa, na kuiongezea nguvu timu hiyo ya Kusini mwa Afrika.

Katika mchezo wa awali, wenyeji Morocco walikuwa wa kwanza kukata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya kuifunga Namibia 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Stade Mohamed V jijini hapa juzi jioni.


Mabao yaliyofungwa katika kila kipindi cha mchezo kutoka kwa Ayoub El Kaabi na Salaheddine Saidi kulishuhudia Simba wa Atlas wakistahili ushndi dhidi ya Namibia.

Dar Swim Mabingwa Chipukizi wa Kuogelea

Wachezaji wa Dar Swim baada ya kutwaa taji la ubingwa wa mashindano ya waogeleaji chipukizi Hopac Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
KLABU ya kuogelea ya Dar Swim imetwaa ubingwa wa Tanzania wa waogeleaji chipukizi wenye umri kati ya miaka 7-14 kwa mara ya pili mfululizo baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 3,144.

Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya timu sita, yalimalizika Jumamosi jioni kwenye Bwawa la Kuogelea la  Shule ya Heaven of Peace Academy (Hopac) jijini Dar es Salaam.

Haikuwa kazi rahisi kwa Dar Swim Club kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa klabu za Taliss na Bluefins, ambazo zilionesha upinzani wa hali ya juu.

Taliss ilimaliza katika nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 2,966 huku Bluefins ikimaliza ya tatu kwa kupata pointi 2,945 na Champion Rise ikishika nafasi ya nne kwa kupata pointi 329.
Nafasi ya tano ilichukuliwa na timu ya Wahoo ya Zanzibar kwa kupata pointi 222  na klabu ya Mwanza International School ikimaliza ya sita kwa kupata pointi 44.

Mashindano hayo yalidhaminiwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Coca Cola, Print Galore, Label Promotions, Kisima Water, IST, JNC Events Support & Co limited, Kalu Photography na Knight Support.

Waogeaji wa kike wa klabu ya Dar Swim Club ndio waliochangia ushindi kwa kiasi kikubwa katika mashindao hayo baada ya kuwa wa kwanza kwa kujikusanyia pointi 1,706 na kufuatiwa na Taliss waliopata pointi 1,480 na  Bluefins kwa kupata pointi 1,000.

Wahoo walishika nafasi ya nne kwa upande wa wasichana kwa pointi 190 na kufuatiwa na Mwanza (44) na Champions Rise katika nafasi ya sita kwa kupata pointi 30.

Kwa upande wa wavulana, klabu ya Bluefins ilishika nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 1,755 na kufuatiwa na Taliss (1,321) na Dar Swim Club (1,243), Champion Rise ( 329) na Wahoo katika nafasi ya tano kwa kupata pointi 32.
Katibu Mkuu wa DSC, Inviolata Itatiro aliwapongeza wachezaji na makocha wa klabu hiyo kwa kufanya vyema katika mashindano hayo na kuendelea kuwa mabingwa.
Inviolata alisema kuwa kujituma kwa wachezaji, makocha, viongozi na wazazi kumeiletea sifa timu hiyo.


Mashindani hayo yalishirikisha jumla ya waogeleaji chipukizi 182 walioshindana katika meta 50, 100 na 200 katika staili tano butterfly, freestyle, breaststroke, backstroke na Individual Medley (IM).

Saturday 27 January 2018

Vinara Simba kibaruani Leo Ikiivaa Majimaji

Na Mwandishi Wetu
SIMBA SC kesho Jumapili ina kibarua kigumu pale itakaposhuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kukabiliana na Majimaji FC kwenye mchezo wa kukamilisha raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Mchezo huo utakuwa ndio wa kwanza kwa kocha raia wa Ufaransa, Pierre Lechantre kuiongoza timu hiyo ambaye hivi karibuni aliingia mkataba wa kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo akichukua mikoba iliyoachwa wazi na Mcameroon, Joseph Omog.

Simba inaoongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 32 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 30 huku Yanga ina pointi 28, itahitaji ushindi kwa udi na uvumba ili kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kileleni.

Tangu Simba imtimue kazi Omog mwishoni mwa mwaka jana, timu hiyo ilikuwa chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma ambaye aliiongoza kwenye mechi mbili za ligi na kupata ushindi mnono, iliichapa Singida United mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa, kisha Kagera Sugar ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba mabao 2-0.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwa Simba kutokana na ukweli kuwa Majimaji hawataingia kinyonge, kwani nao pointi tatu zina umuhimu mkubwa baada ya kuwa na pointi 13 kwenye nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi.

Akizungumzia mchezo huo kocha Djuma, alisema kuwa si yeye wala kocha wake mkuu, Lechantre wote hakuna anayefahamu timu hiyo vizuri, lakini hilo haliwatishi kwani wameshapata mbinu za kukabiliana nayo.

Alisema kuwa wamekaa na kupanga mikakati yao ambayo moja wapo ni kuingia kwa kushambulia kwa nguvu mwanzo mwisho ili kuwafanya wapinzani wao hao wasitumie mchezo wa kupaki basi.

“Kiukweli mimi pamoja na Kocha Mkuu hakuna anayeijua vizuri Majimaji, lakini hii haiwezi kutufanya tushindwe kupata ushindi kwao, Simba kwa sasa inajitengenezea nafasi ya kuwa bingwa hivyo tunataka mchezo huu tushinde ili tuzidi kuwa kwenye nafasi nzuri,” alisema Djuma.

Kwa upande wao, Majimaji yenye maskani yake Songea mkoani Ruvuma, kupitia kwa mchezaji wao nyota, Jerry Tegete, alisema kuwa mchezo huo kwao wanautizama kwa jicho la tatu kwani wanahitaji kuondoka na pointi tatu ambazo zitawafanya wasogee juu kwenye msimamo wa ligi.

Alisema kuwa wanafahamu wazi kuwa wapinzani wao hao wameonesha kiwango kizuri hivi karibuni pamoja na ujio wa kocha mpya, utawafanya waingie kwenye mchezo huo kwa kujiamini, lakini hayo yote hayawatishi na wanachokitaka ni kurudi Songea na ushindi tu.


“Ukiangalia ligi kwa sasa inaelekea mzunguko wa pili ambao ni wa lala salama,  tunahitaji pointi tatu kwenye mchezio huo ambazo zitatufanya tukae sehemu nzuri wakati ligi ikiwa inaelekea ukingoni,” alisema Tegete.

Watanzania Watatu Kuunda Kamisheni Anoca

Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA watatu wameteuliwa kuwemo katika Kamisheni mbalimbali za Kamati ya Olimpiki ya Afrika (Anoca),imeelezwa.

Katibu Mkuu TOC, Filbert Bayi
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya Anoca, kilifanyika hivi karibuni jijini Abuja, Nigeria, ambapo Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamisheni ya Olimpiki ya Tokyo 2020.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Bayi jana, mwenyekiti wa kamisheni hiyo ni Omar Seydina wa Senegal wakati wajumbe mbali na Bayi wengine ni Paul Tergat (Kenya), Skander Hachica (Tunisia), Habu Gumel (Nigeria) na Benjamin Boukpeti (Togo).

Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau ameteuliwa kuwa mjumbe wa kamisheni ya Masoko na Mawasiliano wakati mjumbe wa TOC, Irine Mwasanga yumo katika kamisheni ya Wanawake na Michezo.


Taarifa hiyo ilisema kuwa majukumu ya kamati hizo yatatolewa baadae na ofisi ya Katibu Mkuu wa Anoca.

Yanga Yaichapa Azam Kwenye Uwanja waoi

Na Mwandishi Wetu
YANGA imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Hatahivyo, ushindi huo wa Yanga umeendelea kuibakiza timu hiyo katika nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam baada ya kujikusanyia pointi 28.

Washindi walishuka dimbani huku wakicheza bila ya wachezaji wake karibu saba, ambao ni majeruhi, lakini walicheza kandanda safi.

Aidha, mchezaji wa Azam FC Abubakari Salum ‘Sure Boy’ alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumsukuma kwa makusudi, Hassan Kessy mbele ya mwamuzi wa kati Israel Nkongo.

Azam ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya tatu baada ya kuanza kwa mchezo huo likifungwa na Shaban Chilunda, huku Obrey Chirwa akisawazisha dakika ya 30 na la ushindi likifungwa na Gadiel Michael.

Ushindi huo umeendelea kuibakiza  Yanga katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikifikisha jumla ya pointi 28, nyuma ya Azam yenye pointi 30 na Simba 32.

Azam FC ilianza mpira kwa kasi na kufanikiwa kupata bao hilo la uongozi baada ya Chilunda kutengenezewa pasi na Bruce Kangawa.

Baada ya Azam kuongoza bao hilo walianza kupunguza kasi na kuwapa nafasi wapinzani wao kusawazisha kupitia kwa Chirwa aliyepata pasi ya Ibrahim Ajibu ambapo alimzunguka kipa Razaki Abalora na kufunga.

Azam baada ya kusawazishiwa walirudi tena kwenye kasi na kufanya mashambulizi mengi lakini hayakuzaa matunda, na kutoa nafasi zaidi kwa Yanga kujiamini ambapo Gadiel alipiga shuti kali nje ya 18 na kuifungia Yanga bao la pili.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Azam ilikuwa ikiongoza kwa mashambulizi lakini Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili Azam iliendeleza kasi ya mashabulizi bila mafanikio kwani  tayari Yanga iliweka ukuta na kupata wakati mgumu wa kufunga. Hadi mpira unakwisha matokeo hayo
Kocha wa Azam alijaribu kufanya mabadiliko kadhaa lakini hayakuzaa matunda. Dakika 36 alimtoa Bernard Arthur na kumuingiza Salmin Hoza, pia, kipindi cha pili dakika 55 na 65 alimtoa Stephen Kingue na Shaban Chilunda na kuingia Mbaraka Yusufu na Paul Peter.

Kwa upande wa Yanga dakika ya 66 iliwatoa Emmanuel Martin na kuingia Geofrey Mwashiuya, pia, dakika 68 alimtoa Ibrahim Ajibu na kuingia Juma Mahadhi.

Azam FC.Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa, Agrey Morris, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue, Salum Abubakari, Joseph Mahundi, Bernard Arthur, Shaban Chilunda na Enock Atta.

Kikosi cha Yanga. Youthe Rostand, Kelvin Yondani, Gadiel Michael, Hassan Kessy, Raphael Daud, Andrew Vicent, Said Juma, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin.


Mechi nyingine zilizochezwa ni Mwadui dhidi ya Njombe waliopata sare ya mabao 2-2 na Mbeya City dhidi ya Mtibwa sare ya bila kufungana 0-0. Na Kagera Sugar na Lipuli pia zikitoka sare ya 0-0.

TAA Yarudishiwa Kiwanja cha Ndege cha Kahama

 Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (wanne kulia), Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack (Mwenye ushungi) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (watatu kulia), jana wakikagua miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Kahama kabla ya makabidhiano ya kurudishwa serikalini na Kampuni ya Madini ya ACACIA.
Na Mwandishi Wetu, Kahama
KAMPUNI ya madini ya ACACIA yenye kumiliki migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu imekirudisha serikalini Kiwanja cha Ndege cha Kahama kwa ajili ya kuchochea maendeleo kwa ujumla.

Awali mwaka 2005 kiwanja hicho kilikabidhiwa kwa makabidhiano maalum kati ya serikali na iliyokuwa kampuni ya madini ya Barrick walioomba ili kurahisisha shughuli zao za migodini ikiwemo ya kutumia ndege kusafirisha wafanyakazi wao na vifaa.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainabu Telack akihutubia wananchi waliofika kushughudia makabidhiano ya Kiwanja cha Ndege cha Kahama yaliyofanyika jana baina ya Kampuni ya Madini ya ACACIA na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Katika makabidhiano hayo yaliyofanyika jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela aliiomba serikali kusaidia kurefusha barabara ya kutua na kuruka kwa ndege kutoka Km. 1.5 hadi kufikia Km 2, ili kufanikisha utuaji wa ndege kubwa ikiwemo ya Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q400.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (watatu kulia), akisaini nyaraka za makubaliano ya kurudishwa Kiwanja cha Ndege cha Kahama kwa serikali kutoka kwa Kampuni ya Madini  ya ACACIA, ambapo wa pili kulia ni Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu na wakwanza kulia ni Mwanasheria wa ACACIA, Bi Diana Wamuza, huku Naibu Waziri Sekta ya Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa (mwenye miwani) na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack wakishughudia.
“Tunashukuru wenzetu wa ACACIA kwa kurudisha tena serikalini kiwanja hiki, lakini bado tunaimani tutaendeleza ushirikiano baina yetu, lakini ombi langu kwa serikali ni kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege ili ndege kubwa zaidi ziweze kutua ninaimani zitachochea shughuli za kilimo, biashara na madini na uchumi wananchi utaimarika zaidi,” alisema Bw. Mayongela.
 Mwanasheria wa ACACIA, Bi. Diana Wamuza (wa kwanza kulia) akishughudiana makabidhiano ya nyaraka za kurudishwa kwa Kiwanja cha ndege cha Kahama uliofanywa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu.
Naye Naibu Waziri, Mhe. Kwandikwa alisema serikali itahakikisha inasaidiana na wadau mbalimbali ili waweze kurefusha barabara ya kutua na kuruka kwa ndege, ili kufanikisha utuaji wa ndege kubwa za abiria na mizigo, ambazo zitachochea maendeleo ya Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.

Hatahivyo, Mhe. Kwandikwa aliwataka ACACIA kuweka katika mipango yao ya kusaidia ujenzi wa upanuzi na urefushaji wa Kiwanja cha ndege cha Kahama, ili kiweze kutumika kwa lengo la kutua kwa ndege kubwa, ambapo itachochea sera ya kukuza viwanda.
Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa akizungumza mara baada ya makabidhiano ya kurudishwa serikalini Kiwanja cha Ndege cha Kahama kutoka kwa Kampuni ya Migodi ya ACACIA, uliofanyika jana mkoani Shinyanga.  Mwenye ushungi ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Zainab Telack na wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.
“Tunamaeneo mengi sana hapa Shinyanga, tunawaita wawekezaji waje kuwekeza kwa wingi katika ujenzi wa viwanda, kilimo, madini na biashara nyingine, sasa usafiri wa uhakika upo ukizingatia tunaviwanja viwili vya ndege kikiwemo hiki cha Kahama na kile cha Shinyanga, na malighafi, umeme na maji vipo vya kutosha hivyo waje tu kuwekeza,” alisisitiza Mhe. Kwandikwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa, Bi. Telack alisema sasa mkoa wake utainuka kwa kuwa umepata fursa ya kuongezewa kiwanja cha pili cha ndege cha Kahama, ambapo sasa wananchi wataweza kusafirisha mazao ya kilimo na kufanya biashara na mikoa mingine kutokana na usafiri wa ndege ni wa haraka na uhakika.

“Ninakuomba Naibu Waziri najua hili lipo kwenye wizara yako, utusaidie kuharakisha kumalizika kwa kiwanja cha ndege cha Shinyanga, maana hiki hapa tayari kipo ili na sisi tuweze kupata wawekezaji katika viwanda mfano Wachina wasiende kuwekeza mkoani Pwani pekee bali waje na huku, tunaimani tutachochea maendeleo sio ya mkoa wetu tu ila kwa Taifa kwa ujumla,” alisema Bi. Telack.

Kwa upande wa Meneja wa migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyahulu, Bw. Benedict Busuzu alisema wanajivunia tukio la kurudisha kiwanja cha ndege cha Kahama kwa serikali, ili sasa kiweze kutumika na Watanzania wote katika kuchochea ukuaji wa viwanda.


Hata hivyo, Bw. Busuzu ameahidi wataendelea kutoa huduma mbalimbali kwenye kiwanja hicho kama ilivyokuwa awali, na wataendeleza ushirikiano mzuri ulipo kati yao na TAA.