Tuesday 19 March 2019

MultiChoice Yatangaza Fursa kwa Wadau wa Filam Nchini, Afrika


Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya MultiChoice-Tanzania imetangaza  fursa ya kipekee kwa wadau wa tasnia ya filamu Tanzania na barani Afrika kwa ujumla ijulikanayo kama MultiChoice Talent Factory Portal iliyodhamiria kuleta mapiduzi ya hali ya juu katika uaandaaji wa filamu zenye viwango vya kimataifa kutoka barani Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Mkuu wa kitengo cha Uhusiano kutoka MultiChoice Tanzania Johnson Mshana alieleza kuwa programu hiyo ni muendelezo wa programu maalum ya iliyodhamiria kuleta mabadiliko katika tasnia ya filamu barani Afrika.

 “MultiChoice Talent Factory ambayo ni progamu mama  ilizinduliwa rasmi mapema  Mei mwaka jana na imedhamiria kuleta mabadiliko chanya kwenye tasnia ya filamu hapa nyumbani Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Tulianza kwa kupeleka vijana wanne katika kambi maalum ya mafunzo ya uandaaji filamu katika akademia maalum kule Nairobi nchini Kenya, kisha mafunzo maalum kwa magwiji wa sauti yaliyofanyika Januari mwaka huu na hatimaye leo hii tumekuja tena na platform maalum yenye dhamira ile ile ya kuleta mapinduzi katika tasnia ya filamu barani Afrika”, alisema Mshana.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo alisema kuwa, anaishukuru sana Kampuni ya MultiChoice kwani imekuwa mstari wa mbele katika kuleta mapinduzi kwenye tasnia ya filamu hapa Tanzania.

 “Binafsi nilishuhudia uzinduzi wa programu ya MultiChoice Talent Factory mapema mwaka jana kule mjini Dodoma na leo hii tunazindua tena sehemu nyingine ya programu hiyo hiyo. Hakika ni fursa ya kipekee na ninapenda kuchukua nafasi hii kuwahamasisha wadau wote waliopo katika tasnia yetu kuitumia nafasi hii ipasavyo ili kuweza kujifunza, kubadilishana ujuzi na hatimaye kupata kazi zenye maudhui ya hali ya juu kutoka hapa hapa Afrika”,  alisema Fisoo.

Naye Ofisa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania Grace Mgaya alimalizia kwa kueleza kuwa ukurasa huu ni wa wazi kwa watu wote hususani wadau wa filamu waliopo hapa nyumbani na Afrika kwa ujumla.

 “Tunaamini kwa kupitia program hii tutaweza kuwafikia wadau wengi zaidi na tunatarajia kazi zenye ubora wa hali ya juu kutoka barani Afrika kwa siku zijazo kutokana na matokeo chanya yatakyoletwa na program hii ya MultiChoice Talent Factory”, alisema Grace.


Wednesday 6 March 2019

Tanzania Kinara Tena Tuzo za ‘DStv Eutelsat Star Awards’


Mkuu wa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania, Johnson Mshana akimkabidhi mshindi wa tuzo za Kimataifa za DStv Eutelsat Star Awards, Pricilla Marealle cheti cha ushindi wakati wa mahafali ya kidato cha sita katika shule ya St Mary Goretti hivi karibuni. Kulia ni Ofisa Uhusiano  wa MultiChoice Tanzania. Grace Mgaya. 

Na Mwandishi Wetu

KWA mara nyingine tena Tanzania imeibuka kinara  katika tuzo za kimataifa za wanafunzi zijulikanazo kama DStv Eutelsat Star Awards ambapo mwanafunzi Priscilla Marealle kutoka shule ya sekondari ya St. Mary Goreti mkoani Kilimanjaro ameweza kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa kunyakua nafasi ya kwanza katika kipengele cha uchoraji bango  ikiwa ni baada ya mchuano mkali baina ya mamia ya wanafunzi kutoka nchi zaidi ya 10 kote barani Afrika.

Kwa upande wa uandishi wa insha kijana Tanaka Chonyera kutoka  nchini Botswana aliweza kujinyakulia ushindi wa kwanza.

 Tuzo hizi ambazo huhusisha uandishi wa insha maalum au kuandaa bango yenye ujumbe kuhusiana na elimu ya anga hususan Setelait ni za wazi kwa wanafunzi wote wa shule za sekondari wenye umri kati ya miaka 14 – 19 kote barani Afrika ambapo kampuni ya MultiChoice inaendesha shughuli zake.
Mkuu wa shule ya  St Mary Goretti Sr. Lucrecia Njau akifurahi baada ya kupokea cheti kutoka kwa Mkuu wa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana mara baada ya shule hiyo kufanikiwa kutoa mshindi wa jumla wa wa tuzo za kimataifa za DStv Eutelsat Star Awards Pricilla Marealle. 
  Katika msimu huu wa nane, washindani walitakiwa kuandika insha au kubuni bango litakaloelezea licha ya Satelait kutumika katika shughuli mbalimbali, ni namna gani zitaweza kutumika zaidi ili kuleta maendeleo chanya ulimwenguni.

 Priscilla ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita wa mchepuo wa Sayansi katika shule ya Mtakatifu Maria Goreti alitangazwa rasmi kuwa mshindi mjini Accra nchini Ghana ambapo ndipo jopo la watahini liliongozwa na Paolo Nespoli, mwanaanga nguli kutoka European Space Agency (ESA) lilikaa kupitia kazi kutoka kwa wanafunzi walioshinda katika nchi mbalimbali.
Mshindi wa Jumla wa tuzo za kimataifa za DStv Eutelsat Star Awards Pricilla Marealle akikabidhiwa kikombe cha ushindi na Mkuu wa shule ya St Mary Goretti Sr. Lucrecia Njau baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa jumla wa wa tuzo za kimataifa za DStv Eutelsat Star Awards. Kulia ni Mkuu wa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana.
 Akiongea baada ya kukabidhiwa cheti cha uthibitisho wa ushindi wakati wa mahafali ya kidato cha sita ya shule ya Mtakatifu Mary Goreti iliyopo Moshi Kilimanjaro, Priscilla amesema amefurahi sana kwa ushindi huo mkubwa ambao umemletea yeye, shule yake na taifa zima kwa ujumla sifa kubwa. “Nimefurahi sana kupokea taarifa hizi nzuri. Naamini ushindi wangu utakuwa ni chachu kubwa kwa wanafunzi wenzangu kote nchini kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika tuzo kama hizi na mashindano mengine ya kitaaluma ya ndani na nje ya nchi, na kusisitiza  kuwa Ndoto huanza kufanya kazi pale unapojiamini” alisema Priscilla.
 
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo ya Mtakatifu Maria Goreti Sister Lucresia Njau alisema kuwa anaishukuru sana kampuni ya MultiChoice Tanzania kwa kuwapatia nafasi ya kushiriki katika Mashindano hayo na hatimaye kuweza kunyakua tuzo hiyo kupitia mwanafunzi wao Priscilla.

 “Huyu kijana ana jitahidi sana katika chochote kile anachokifanya, iwe ni darasani au hata katika majukumu mengine nje ya darasani. Ni msikivu mtiifu lakini zaidi ya yote ni mbunifu sana. Naamini haya ndiyo yaliyomfanya aweze kushinda tuzo hizi” alisema Sr. Lucrecia Njau.
  
Naye, Mkuu wa Uhusiano MultiChoice Tanzania Johnson Mshana alisema,” Huu ni msimu wa tatu mfululizo kwa Tanzania kuendelea kung’ara katika tuzo hizi za DStv Star Awards. Tulianza kupeperusha bendera yetu na kijana Davids Bwana msimu wa sita baada ya kushika nafasi ya pili Afrika katika kipengele cha uandishi wa insha, kisha tukaibuka kidedea baada ya kupokea taarifa za ushindi wa kwanza wa kijana Taheer Rashid katika msimu wa saba mwaka jana na leo hii tunayofuraha kubwa kuona kuwa tumeendeleza wimbi la ushindi.”