Na Mwandishi Wetu
SARE ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City
imemkatisha tamaa kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Nasoro ‘Cheche’ na kusema nivyema
wakajipanga upya kwa ajili ya msimu ujao.
Sare hiyo imeifanya Azam kubaki nafasi ya tatu kwenye
msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi zao 43, katika michezo 23, huku Simba na
Yanga zikichuana kwenye mbio za ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.
Akizungumza na gazeti hili, Cheche, alisema sare ya
juzi dhidi ya Mbeya City imevuruga kabisa malengo yao ya ubingwa na kwa mtazamo
wake nivyema wakajipanga upya kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu ambao
wataweza kutimiza malengo ya timu.
“Sisemi kwamba wachezaji waliopo hawana uwezo bali
tunahitaji kuongeza baadhi kutoka ndani na nje ili kuimarisha zaidi kikosi
chetu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma,” alisema Cheche.
Kocha huyo alisema kitu kikubwa ambacho
kinawakwamisha msimu huu ni baadhi ya wachezaji wao wakutumainiwa kuwa majeruhi
huku waliobaki wakiwa hawana zoefu wa kutosha kwa ajili ya mapambano ya ndani
ya uwanja.
Azam imebakiwa na michezo saba kabla ya kumaliza
msimu huu na matarajio yao hivi sasa ni kuhakikisha wanamaliza kwa heshima ligi
hiyo kama ilivyokuwa misimu minne nyuma.
No comments:
Post a Comment