Tuesday 24 March 2020

Makonda apongeza TAA kwa kujidhatiti kwa corona

·       Ataka wananchi kufuata masharti yaliyotolewa
·       Asema kuanzia kesho mitaa kupuliziwa dawa
 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akipimwa joto alipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam (JNIA). 
Na Bahati Mollel,TAA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kujipanga vyema kwa kushirikiana na wahudumu wa afya kwa kuweka maji yenye dawa maalum ya kunawa mikono na kupima joto la mwili kwa watu wote wanaoingia na kutoka maeneo ya viwanja vya ndege, ili kuzuia kuingia zaidi kwa watu walioambukizwa ugonjwa wa homa kali ya Mapafu inayosambazwa na virusi vya corona (COVID19).

RC Makonda ametoa pongezi hizo leo alipofanya ziara kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, ambapo alianzia jengo la Tatu la abiria ambalo linahusisha zaidi ndege zinazotoka nje ya nchi, na baadaye kwenda Jengo la Pili la abiria lenye ndege zenye safari za ndani ya nchi na pia nje ya nchi.

Amesema ameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na TAA kwa kuhakikisha hakuna ongezeko la watu walioambukizwa wanaoweza kuingia nchini kupitia Kiwanja hiki.

“Nimejionea mwenyewe kila kona kumewekwa sanitizers, na pale nje lipo tanki kubwa lenye maji yenye dawa lazima kila mtu anawe, na hata huku ndani abiria wanaowasili na wanaoondoka wanapimwa joto la mwili kwa mashine ya mkono na ile ya scanner, hivyo ninaimani kwa udhibiti huu hakuna maambukizi zaidi yanayoweza kutokea,” amesema Mhe. Makonda.

Hatahivyo, amesema pia kuanzia tarehe 25 Machi, 2020 asilimia 98 ya ndege zenye safari za nje hazitaingia nchini baada ya zenyewe kufuta safari zao kutokana na kukosekana kwa abiria, hivyo itasaidia kwa asilimia 80 ya abiria kupungua kuingia kwa kuwa ni nchi nyingi zimeweka makatazo na kufunga mipaka yao.

“Sisi hatujafunga mipaka lakini hadi sasa idadi ya abiria wakigeni imeshuka kwa kiasi kikubwa mfano ndege yenye kubeba abiria 250 sasa inabeba abiria 20, hivyo asilimia 80 ya abiria aidha wenyewe kutokana na elimu waliyopata kutokana na huu ugonjwa wameona hakuna sababu ya kusafiri na wengine baada ya kuona masharti yaliyowekwa ya kwenda nchi moja ama nyingine wakaamua kukaa majumbani mwao, na hii inadhihirisha jinsi gani Mhe. Rais John Pombe Magufuli aliposema kuwa kama unaona safari haina ulazima basi usiende,” amesisitiza Mhe. Makonda.

Pia amesema mashirika ya ndege yamekuwa na ushirikiano na JNIA kwa kutoa taarifa kabla ya kutua endapo wanaabiria mwenye kuhisiwa anaugua ugonjwa huo, na ikifika taratibu za kumpeleka katika kituo kilichoteuliwa zinachukuliwa.

“Tunashukuru sana tena na tena hapa JNIA wamesema hata idadi ya wasindikizaji imepunguzwa ili kuondoa kabisa msongamano katika majengo ya abiria, maana wakiwa wengi itakuwa shida zaidi endapo yupo ambaye anamaambukizi,” amesema.

Pia amesema kwa sasa abiria wote wanaowasili kutoka kwenye nchi zilizokuwa na maambukizi wanapekelekwa kwenye hoteli na hosteli zilizoteuliwa na mkoa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa siku 14 kwa gharama zao wenyewe. Katika hatua nyingine amesema leo abiria 200 wa nchi ya Comoro wamezuiwa kuondoka baada ya nchi yao kufunga mpaka kutokana na kuzuia maambukizi ya corona.

Pia amewataka watu wote wanaoingia na kutoka nchini kwa kutumia usafiri wa ndege, mabasi na meli kufuata utaratibu uliowekwa na Mamlaka za juu ili kuepukana na maambukizi, ambapo pia amesema katika usafiri wa umma (Daladala) watu wasipande likiwa limejaa kupita kiasi na amesisitiza kuwa ugonjwa huu hauna umri kuwa vijana hawafi,  hivyo wanajidanganya na wachukue tahadhari zilizowekwa.

Hali kadhalika amesema wananchi na watu wote kutokuwa na hofu kuanzia kesho Jumatano tarehe 25 Machi, 2020, Ofisi yake kwa kushirikiana na Maafisa Afya watapulizia dawa kwenye mitaa ili kuua wadudu mbalimbali; na ofisi yake itaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maradhi ya corona.

Naye Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha amesema wameendelea kutoa elimu kwa watu wote wanaoingia na kutoka kwenye kiwanja hicho kwa kuweka mabango yanayoelekeza namna ya kujikinga, na pia wameweka sabuni maalum za kunawa mikono wanapoingia na kutoka maeneo hayo.
  

Wednesday 18 March 2020

Corona Yazidi Kutikisa Soka la Ulaya


ZURICH, Uswisi

 SHIRIKISHO la Soka la Ulaya (Uefa) limeahirisha mashindano ya Mataifa ya Ulaya, Euro 2020 hadi Juni na Julai mwaka 2021, kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Hatua hiyo ya kusogeza mbele mashindano hayo makubwa barani Ulaya kwa timu za taifa, ilifikiwa jana Jumanne katika kikao cha dharura kilichofanyika kwa njia ya video.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema jana na Chama cha Soka cha Norway, mpango huo mpya umepanga mashindano hayo kufanyika kwa mwezi mmoja kuanzia Juni 11 hadi Julai 11.

Uamuzi huo wa Uefa umetoa nafasi kwa ligi Ulaya kote kupata nafasi ya kumaliza misimu yao pamoja na mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Ligi ya Ulaya, baada ya kuodolewa kwa vikwazo ambavyo sasa wanaruhusiwa kufanyika kwa mashindano hayo.

Hadi sasa hakuna utaratibu uliowekwa wa jinsi ya kufanyika kwa mashindano hayo ambayo yamepangwa kufayika katika miji 12 ya Ulaya: Amsterdam, Baku, Bilbao, Budapest, Bucharest, Copenhagen, Dublin, Glasgow, London, Munich, Romena Saint Petersburg.

Nusu fainali za Ero zimepangwa kufanyika jijini London.

Tuesday 17 March 2020

BMT yapongeza Kilimanjaro Premium Lager kwa Udhamini


Mshindi wa mbio za Kilometa 42 za Kilimanjaro Marathon 2020, Kiplagat akimaliza mbio hizo Moshi hivi karibuni.
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limesema Kilimanjaro Premium Lager ni mfano pekee wa kuigwa katika udhamini wa mchezo wa riadha hapa nchini.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro, imekuwa mdhamini mkuu wa mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon mfululizo toka zilipoanzishwa hadi sasa zinatimiza miaka 18.

Kauli hii inakuja siku chache baada ya kumalizika mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2020 mjini Moshi ambazo zilihusisha washiriki zaidi ya 11,000 na idadi kama hiyo ya watazamaji.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha, ambaye alishuhudia msimu wa 18 Kili Marathon Machi Mosi mwaka huu, aliwapongeza wadhamini hao huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kudhamini mashindano mbalimbali katika kukuza mchezo wa Riadha Tanzania.

Msitha, alisema kwa miaka yote hiyo 18 kumekuwa na mabadiliko makubwa Kilimanjaro Marathon na leo limekuwa tukio kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo Kilimanjaro Premium Lager wanapaswa kupongezwa na kuigwa na wengine pia.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla akikabidhi hundi kwa mshindi wa mbio za Km 42 upande wa wanawake, Lydia Wafula (kulia) huku Mkurugenzi wa Masoko wa TBL Group, Doreen Tumubeebire akishuhudia. Kilimanjaro Premium Lager imekuwa mdhamini wa mbio hizi kwa miaka 18 sasa.
Aliongeza kuwa, mashindano kama hayo husaidia pia kuleta umoja kwa jamii.

“Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali wanaohitaji kutoa udhamini katika matukio kama haya, kujitokeza kwani husaidia katika kuleta umoja wa kipekee kwa jamii,” alisema.

Hivi karibuni, BMT ililiagiza Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kupunguza tozo kwa waandaaji wa mbio za barabarani kutoka Sh. Milioni 3 hadi Sh. Milioni 1.5 ili kuwasaidia waandaaji katika kuandaa matukio yenye uhakika.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi amewashukuru watanzania na washiriki wote kwa kujitokeza kwa wingi katika mbio za mwaka huu ambapo namba za mbio za km 42 na 21 ziliisha mapema kabla ya muda wa mwisho uliotangazwa.

“Hii ni dhahiri kuwa mbio hizi zimekuwa maarufu sio nchini tu ila hata nje ya nchi ndio maana sisi kama wadhamini tumekuwepo kwa miaka 18 sasa tangu mbio ghizi zianzishwe,” alisema.

Wadhamini wengine waliofanikisha mbio za mwaka huu ni TPC Limited, Simba Cement, Unilever, Absa Bank Tanzania Limited na watoa huduma rasmi ni Kibo Palace Hotel, Keys Hotel, GardaWorld Security, Precision Air na CMC Automobiles.
  

Corona Yasimamisha Michezo Yote



Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetangaza kusimamisha kwa mwezi mmoja michezo yote inayokusanya watu wengi, ikiwa ni tahadhari ya kujikinga na virusi vya ugonjwa wa corona, ambao tayari umeshaingia nchini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (pichani) alitangaza hayo wakati akilihutubia taifa kwa njia ya radio na televisheni, kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya janga hilo la corona.

Kwa tamko hilo, kuanzia mechi za mchangani hadi zile za Ligi Kuu Tanzaia Bara na ile ya Zanzibar, zitakuwa zimesimamishwa kwa mwezi mmoja, kwani ligi hizo zinahusisha mkusanyiko wa watu wengi.

 “Tunatangaza kusimamishia rasmi michezo yote inayokusanya idadi kubwa ya watu, makundi ya watu kama Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la pili na Umishumta, Umisseta na mashindano ya mashirika ya umma na michezo mingine kwa kipindi cha mwezi mmoja,” alisema Majaliwa.

Alisema baada ya tamko hilo wizara yenye dhamana na michezo ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo watasambaza barua kwa mashirikisho yote nchini wakitakiwa kufanya hivyo.

Kabla ya kutolewa tamko hilo la jana, tayari Ofisi ya Rais, Tawala za  Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia  waziri wake, Selemani Jafo ilifuta Mashindano ya Shule za Msingi na Sekondari kuanzia hatua ya mashule, ambayo yalitarajia kuanza hivi karibuni.

Nchi kadha zikiwemo zile zenye ligi tano kubwa kama England, Hispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa zimesimamisha ligi zao hadi mwanzoni mwa mwezi ujao ili kuamgalia mwenendo wa jango hilo la corona, ambalo tayari limewakumba baadhi ya wachezaji wa ligi hizo.

Mbali na kusimamishwa kwa ligi kubwa Ulaya, Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) limesogeza mbele fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2020 hadi mwakani kuanzia Juni 11 hadi Julai 11, 2021.

Pia Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Ijumaa lilitangaza kusimamisha mechi zote za kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2021) na jana ilitangaza kusimamisha fainali za Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan 2020), ambazo zingefanyika Cameroon mwezi ujao.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana lilitangaza kikao cha dharura ambacho kitafanyika leo jijini Dar es Salaam kuzungumza hatma ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuhusu janga la corona.

Kikao hicho pia kitajadili kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars inayoendelea kujiandaa na fainali za Kombe la Chan nchini Cameroon pamoja na mechi za majaribio za timu hiyo.

Rais wa TFF, Wallace Karia aliagiza Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuitisha kikao cha dharula leo kujadili mustakabali wa michuano hiyo wakati huu wa mlipuko wa virusi vya corona.

Karia alisema kikao hicho kitakachoanza saa 3:00 asubuhi kitafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Golden Tulip, Dar es Salaam.

“Ajenda kubwa katika kikao hicho ni kuangalia mustakabali wa ligi kutokana na mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona ambao umeingia nchini,”alisema Karia.

Friday 6 March 2020

MAB Yaridhishwa Ukaguzi Corona JNIA TB-3


Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Dkt Masatu Chiguma akipimwa joto la mwili na Afisa Afya, Yusta Malisa wakati bodi hiyo ilipotembelea Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kwa ziara ya kikazi.

Na Bahati Mollel, TAA

BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeridhishwa na ukaguzi wa abiria wanaotoka nje ya nchi wanaotumia Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3).

Mwenyekiti wa MAB, Dk Masatu Chiguma amesema leo mara baada ya kumalizika kwa ziara yao ya kwanza ya kikazi tangu kuteuliwa kwao hivi karibuni ya wametembelea jengo hilo kuwa maafisa afya waliopo kwenye Jengo hilo wanafanya ukaguzi kulingana na taratibu zilizowekwa, ili kuzuia maambukizi ya Homa Kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi aina ya Corona, isiingie nchini.

Dkt Chiguma amesema tahadhari ya kuzuia ugonjwa huo ulioanzia nchini China na kusambaa kwenye nchi mbalimbali Duniani, imefanyika ipasavyo kwenye Jengo hilo, baada ya kulitembelea na kuona, vifaa na utendaji wa watumishi hao wa afya.
 
Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha (wa kwanza kulia), akiwasilisha taarifa fupi ya Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kwa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ilipotembelea jengo hilo leo. 

“Matayarisho ya kujihadhari na huu ugonjwa wa Corona yamefanyika kwa hali ya juu na wajumbe wa Bodi tumeridhika baada ya kuona vifaa vinavyohitajika kuvaliwa na watendaji wa kitengo cha afya na pia watumishi wa TAA waliopo maeneo ya kuwasili na maeneo mengine,” amesema.

Akizungumzia jengo hilo, Dkt Chiguma amesema anaipongeza serikali kwa ujenzi wa jengo hili la kisasa lenye vifaa vya kimataifa, ambapo uendeshaji wake ni wa hali ya juu.

“Tumepita kuanzia mwanzo wa jengo hadi mwisho wa jengo na tumejionea namna lilivyo bora na zuri, hata vifaa vyake ni vya kitaalam sana, ukiangalia eneo la mizigo ni mashine tu zinafanyakazi  pamoja na kuwa na Watumishi wachache lakini kila kitu kinaongozwa na mashine za kisasa,” amesema.

Kaimu Meneja wa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), Mhandisi Barton Komba (kulia), akitoa maelezo mbalimbali kwa Bodi ya Ushauri (MAB) iliyotembelea jengo hilo leo. Aliyevaa tai ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Masatu Chiguma.
Hatahivyo, amesema Bodi imebaini bado katika jengo hili kuna upungufu mkubwa wa watumishi, ambapo sasa waliopo wengi ni wanaofanya kazi kwa mikataba mifupi na wale wanaendelea kujifunza (Internship), ambapo ni hatari kwa kuwa sio wakutegemewa zaidi kutokana kuweza kuondoka wakati wowote watakapopata ajira ya kudumu.

Pia ameitaka menejimenti ya TAA kuhakikisha inaboresha maslahi ya watumishi ili waendelee kulitunza jengo hilo kwa kufanya kazi kwa bidii.

Halikadhalika amesema ulinzi na usalama wa abiria na mizigo yao kwenye Jengo hilo ni wa hali ya juu na uliopangiliwa vyema, kwa kuanzia abiria anapoingia wakati akisafiri hadi kufika kwenye ndege, hata mizigo inavyokaguliwa kwa kupitia hatua tano napo panaridhisha.

Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiangalia ramani ya jengo hilo wakati wakilitembelea katika ziara ya kikazi iliyofanyika leo.
Katika hatua nyingine, Dkt Chiguma amewaita Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye jengo hilo, pale TAA itakapotangaza zabuni mbalimbali, maana bado yapo maeneo mengi ya uwekezaji.

Awali akiwasilisha ripoti ya ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha amesema wanakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za uendeshaji, ambapo jengo zima kwa asilimia 100 linatumia umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), na ukikatika hutumika jenereta ambazo zinatumia mafuta mengi.

Ofisa Afya, Yusta Malisa (mwenye koti jeupe), akiwapa maelezo ya Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), namna anavyowakagua abiria wanaowasili kutoka nchi mbalimbali, kuzuia virusi vya Corona vinavyosambaza homa kali ya mapafu visiingie nchini, walipotembelea jengo hilo leo.
Pia amesema wanakabiliwa na upungufu wa watumishi, ambapo wanalazimika kutumia zamu fupifupi na wengine waliotoka asubuhi kurudi jioni kuongeza nguvu (supporting).
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiangalia moja ya begi likipita kwenye mkanda ikiwa ni hatua ya tatu kwa ukaguzi kabla halijafika hatua ya mwisho tayari kupelekwa kwenye ndege, walipotembelea jengo hilo leo katika ziatra ya kikazi.