Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Ligi Kuu
ya Wanawake Tanzania Bara, JKT Queens wanatarajia kushuka dimbani Aprili 21
kucheza na Simba Queens kwenye Uwanja wa Mbweni nje kidogo ya jijini la Dar es
Salaam.
Akizungumza jana,
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Cliford Ndimbo alisema hatua ya
Nane Bora, inatarajia kuendelea Aprili 21 kwenye viwanja vinne tofauti.
“Ligi ya wanawake
hatua ya Nane Bora ilisimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake
(Twiga Stars) iliyokuwa kambini kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Africa
kwa Wanawake, hivyo sasa itaendelea katika mzunguko wa Tano kuanzia Aprili 21,”
alisema Ndimbo.
JKT Queens inaongoza
ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo minne na kushinda yote, huku Simba
Queens ikishika nafasi ya sita ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza michezo
minne na kufungwa mitatu.
Kigoma Sisters
inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa itaikaribisha Baobab ya Dodoma
kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Baobab inashika nafasi ya tano ikiwa na
pointi tano baada ya kucheza michezo minne, ikishinda mmoja, sare mbili na
kufungwa mmoja.
Mabingwa watetezi,
Mlandizi Queens watakuwa ugenini kucheza na Panama kwenye Uwanja wa Samora
Iringa. Mlandizi ina pointi sita katika michezo minne iliyocheza na Panama, inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi mbili katika
michezo minne iliyocheza.
No comments:
Post a Comment