Monday, 16 April 2018

RC Iringa Kuzindua Michezo ya Mei Mosi Aprili 21

Baadhi ya wachezaji wa timu ya wanaume na wanawake ya kuvuta kamba ya Uchukuzi leo wakifanya mazoezi katika shule ya msingi ya Mlandege wakijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yanayoanza kesho kwenye uwanja wa Samora mkoani Iringa.

Na Bahati Mollel-TAA,Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza Aprili 21, 2018 anatarajiwa kuzindua rasmi michezo ya Kombe la Mei Mosi kwenye uwanja wa Samora mjini hapa.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi, Award Safari amesema leo kuwa michezo ya ufunguzi itafanyika leo kwenye uwanja wa Samora, lakini uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanywa na Mkuu wa mkoa.

Safari amesema michezo hiyo inatarajiwa kushirikisha wanamichezo 1,000 kutoka katika timu 20 za wizara, taasisi na idara za serikali ambazo baadhi ni Ofisi ya Rais Ikulu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Tumbaku ya Morogoro, Tanesco, Wizara ya Mali Asili na Utalii, Chuo cha Mipango Dodoma, Wakala wa Taifa wa Chakula.

Nahodha msaidizi wa timu ya Kamba ya wanawake, Tabu Cosmas (mwenye ushungi) akiwa na wachezaji wengine wa timu ya wanaume ya kamba ya Uchukuzi wakiwa kwenye mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Mei Mosi katika uwanja wa shule ya msingi Mlandege. Mashindano hayo yatafunguliwa rasmi Aprili 21, 2018 na Mkuu wa mkoa wa Irimnga, Mhe. Amina Masenza katika uwanja wa Samora.

Baadhi ya timu nyingine ni Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Chuo Kikuu cha Mkwawa, timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Hifadhi ya Ngorongoro.

Safari amesema mashindano hayo ambayo mabingwa wake watakabidhiwa zawadi ya kombe na Mhe. Rais John Pombe Magufuli siku ya sherehe za Wafanyakazi Mei Mosi, yatashirikisha michezo ya netiboli, soka, kuvuta kamba, baiskeli, karata, draft, mbio za marathon na bao.

Daktari wa timu ya Uchukuzi, Hawa Senkoro (wa pili kushoto) akijumuika katika mazoezi ya timu ya kamba katika yaliyofanyika leo kwenye uwanja wa shule ya Msingi Mlandege wakijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yanayoanza kesho katika uwanja wa Samora, na yatazinduliwa rasmi April 21, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza.

Naye Katibu Mkuu wa timu ya michezo ya Uchukuzi, Mbura Tenga ametamba timu yake kuendeleza wimbi la ushindi kwa kutetea vyema ubingwa wao kwenye michezo ya kuvuta kamba, kuendesha baiskeli, netiboli na karata kwa wanawake na wanaume.

Tenga amesema timu hiyo ambayo tayari imeshafika Iringa ikiwa na wachezaji 78 imejiandaa vyema kwa kufanya mazoezi ya nguvu na kupata mechi za kirafiki katika viwanja vya shule ya sekondari ya Airwing jijini Dar es Salaam.

Kocha Suleiman Kingsley (mwenye trucksuit), akielekeza mazoezi kwa wachezaji wa timu ya soka ya Uchukuzi yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa, wakijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza leo kwa kushirikisha michezo mbalimbali. Michuano hiyo itazinduliwa rasmi Aprili 21, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza.

“Wachezaji wetu wote wapo katika hali nzuri kiafya na hakuna anayeumwa na tayari tupo hapa Iringa kuanza mashindano, kwa kweli tumejiandaa vizuri na tupo tayari kwa mashindano haya, ambayo baadhi ya michezo tulitwaa ubingwa wa kwanza, pili na tatu na tunaahidi tutarejesha vikombe vyetu tumekuja kikazi zaidi,” amesema Tenga.

  Kipa Kennedy Mwamteto (kushoto) wa timu ya Uchukuzi akifanyishwa mazoezi na kocha wake Alter Mollel (kulia) huku kipa mwenzake Willy Barton (mwenye namba 17 mgongoni), wakifanya mazoezi kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Mkwawa ya kuijiandaa na mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza leo kwenye uwanja wa Samora.     


No comments:

Post a Comment