Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Rufaa ya Maadili ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) imetupa rufaa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael
Wambura kufungiwa maisha kujihusisha na shughuli za soka.
Akisoma hukumu hiyo jana Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili
ya TFF, Ebenezer Mshana alisema kamati yake ilipitia hukumu tatu, ambazo
zilikatwa kwa kamati hiyo dhidi ya TFF.
Mshana alisema baada ya kupitia hukumu zote tatu na
hoja za rufaa, rufaa moja ya Edgar Chibula ilishinda na rufaa mbili ambazo ni
ya Wambura na Dustan Mkundi, kamati imejiridhisha na maamuzi ya awali
yaliyotolewa na Kamati ya Maadili kuwafungia maisha.
“Upande wa utetezi wa Wambura ambao ulikuwa na
mawakili watatu ukiongozwa na Masumbuko Lamwai, ulileta mbele ya kamati hoja
nne za kupinga mteja wao kufungiwa maisha kujihusisha na soka na upande wa TFF
uliwakilishwa na wanasheria wawili ikiongozwa na Allan Kiluvya,” alisema
Mshana.
“Katika barua yake ya Desemba 4, 2016 Kamati ya Maadili
ya Rufaa imejiridhisha kuwa Wambura alipewa nafasi ya kujieleza kwani alitakiwa
kufanya na Kamati ya Ukaguzi na ushahidi wa video uliwasilishwa mbele ya kamati
hiyo,” alisema Mshana.
Katika hoja za rufaa kamati ilisikiliza pande zote
mbili za rufaa na upande uliokatiwa rufaa ambao ni TFF baada ya kusikiliza
pande zote mbili kamati ilijiridhisha na maamuzi ya kamati ya maadili.
Kamati ya TFF ilimfungia kujihulisisha na soka maisha
Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura
baada ya kumkuta na hatia katika tuhuma tatu zilizokuwa zinamkabili kwa
mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013 kama
zilivyofikishwa kwenye kamati na sekretarieti ya TFF.
Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti
ya TFF kwa makosa ya kupokea/kuchukua fedha za TFF kwa malipo yasiyo halali na
kughushi barua ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za
TFF Toleo la 2013.”
Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho
ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa
2015).
Kamati ya Rufaa ya Maadili imeiagiza TFF kulifikisha
suala la Wambura na Danstun Mkundi kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zingine
za kisheria na imebariki kifungo cha maisha cha kutojihusisha na soka maisha.
Kwa upande wa wakili wa Wambura, Muga alisema mteja
wake hajaridhishwa na hukumu hiyo, hivyo atakata rufaa katika ngazi nyingine.
No comments:
Post a Comment