Na Mwandishi
Wetu
SIMBA SC
tayari wapo mjini Dares Salaam tangu jana mchana kwa maandalizi ya mwisho ya
pambano dhidi ya mahasimu wao, Yanga litakalofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa,
Jijini Dar es Salaam.
Baada ya
mazoezi yao asubuhi tu Uwanja wa Highland, Morogoro, wachezaji wa Simba na
benchi lao zima la ufundi wakapanda basi lao kurejea Dar es Salaam ambako
wamefikia katika hoteli ya SeaScape, eneo la Mbezi Beach, pembezoni mwa Bahari
ya Hindi.
Simba ilikuwa
Morogoro tangu Jumapili kwa kambi ya maandalizi ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania
Bara dhidi ya mahasimu wao, Yanga keshokutwa Jumapili,
Wekundu hao
wa Msimbazi waliwasili Morogoro wakitokea Iringa, ambako Jumamosi walitoka sare
ya kufungana bao 1-1 na wenyeji wao, Lipuli katika mchezo uliopigwa kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora.
Watani wao,
Yanga nao wapo Morogoro tangu Jumatatu, siku moja tu baada ya kulazimishwa sare
ya 1-1 na wenyeji wao, Mbeya City katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania
Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine.
Matarajio ni
Yanga, ambao ndiyo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu kuingia Dar es Salaam mapema
kesho tayari kwa mchezo huo wa Jumapili.
Jumapili inatarajiwa
kuwa siku kubwa mno katika soka ya Tanzania, miamba hiyo ya soka nchini
ikimenyana vikali katika mbio za kuwania ubingwa.
Simba SC
iliyo chini ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Aymen
Mohamed Hbibi, Mrundi, Masoud Juma na mzawa Muharami Mohamed ‘Shilton’, inaongoza
Ligi Kuu kwa pointi zake 59 baada ya kucheza mechi 25, wakati Yanga inafuatia
kwa mbali kidogo ikiwa na pointi zake 48 baada ya kucheza mechi 23.
Yanga
inazidiwa pointi 11 na Simba SC na ina viporo viwili, maana yake ili kutetea
ubingwa wao, itabidi washinde Jumapili na washinde mechi zao zote zilizobaki za
Ligi Kuu, huku wakiwaombea mahasimu wao hao wapoteze mechi nyingine, jambo
ambalo ni gumu.
No comments:
Post a Comment