KUNDI la
wachezaji 15 na viongozi kadhaa la timu ya Tanzania itakayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola, limeondoka leo kwenda Gold Coast, Australia tayari kwa
michezo hiyo itakayoanza Aprili 4 hadi 15.
Tanzania katika
michezo hiyo inawakilishwa na timu za riadha, ngumi, mpira wa meza na kuogelea.
Timu hiyo
ikiongozwa na meneja wao, Nasra Juma iliondoka kwa ndege ya Emirates huku
nahodha wake, Masoud Mtalaso akitamba kuwa wako tayari kwa kuiletea nchi
medali.
Kwa mara ya
mwisho Tanzania ilipata medali kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka
2006 Melbourne, Australia, ambako Samson Ramadhani na Fabian Joseph walirudi na
medali ya dhahabu na shaba katika mbioza marathon na meta 10,000.
Rais na Katibu
Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid na Filbert Bayi wenyewe
waliondoka Jumatano mara baada ya timu hiyo kuagwa na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe huku kiongozi wa msafara,
ambaye ni Mkurugenzi wa Michezo Dk Yussuf Singo aliondoka tangu Jumapili.
“Tumekuwa tukifanya mazoezi ya nguvu kwa muda mrefu na ni matarajio yetu kuwa tutafanya vizuri katika michezo hiyo, “alisema Kidunda.
Naye
Mtalaso alisema kuwa timu ya mpira wa meza imejiandaa vizuri hasa ukizingatia
kuwa walipiga kambi nchini China kwa takribani miezi mitatu wakijifua kwa ajili
ya michezo hiyo kabla ya kurejea nchini na kupiga kambi kwa mwezi mmoja Mkuza,
Kibaha mkoani Pwani.
Australia
imekuwa sehemu ya bahati kwa timu ya Tanzania, ambapo ilifanya vizuri mwaka 1982
wakati ilipotwaa medali sita: Moja ya ngumi, tatu za riadha na mbili zilitoka katika
mbio za uwanjani.
Gidamis
Shahanga alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za meta 10,000, wakati Zakaria
Barie, ambaye amesafiri na timu hiyo kama kocha, alishinda medali ya fedha
katika mbio kama hizo. Juma Ikangaa alirudi na medali ya fedha katika marathon,
huku ile ya shaba ikiletwa na bondia wa uzito wa juu, Willy Isangura na mtupa
mkuki Zakayo Marekwa naye alileta medali ya shaba.
Mwanariadha
wazamani wa Tanzania, Bayi ikiwa ni miaka 44 sasa anaendelea kushikilia rekodi
ya Jumuiya ya Madola aliyoiweka mwaka 1974 ya meta 1500 michezo hiyo
ilipofanyikia Christchurch, New Zealand. Bayi pia aliweka rekodi ya dunia,
ambayo ilikuja kuvunjwa miaka mitano baadae na Sebastian Coe, ambaye sasa ni
Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAAF).
Ikiwa
ni miaka 12 sasa tangu kufanyika kwa Michezo ya Melbourne, timu ya Tanzania
yenye wachezaji 16 inarejea tena Australia, ikiwa pia na micezo ambayo
haikuwepo walipofanya vizuri nchini humo kama mpira wa meza na kuogelea.
Timu
ya riadha inaundwa na wanariadha wa marathon, Stephano Huche, Said Makula na Sarah
Ramadhani.
Wakati
Failuna Abdul atashindana katika mbio za meta 10,000, huku Ali Khamisi Gulam, atafanya
vitu vyake katika mbio za meta 100 na 200, akiwa ni mwanariadha pekee wa mbio
fupi katika timu ya riadha.
Anthony
Mwanga ambaye anasoma Afrika Kusini, yeye atachuana katika michezo ya uwanjani
ya miruko na mitupo katika timu hiyo ambayo iko chini ya Barie na Lwiza John.
Kikosi
cha timu ya ngumi kinaundwa na Ezra Paulo (bantam), Kassim Mbutike (welter),
Seleman Kidunda (middle) na Haruna Swanga (heavy). Timu hiyo iko chini ya kocha
Mkenya, Benjamin Oyombi.
Awali
kulikuwa na waogeleaji wawili, Hilal Hilal na Sonia Franco, chini ya kocha Khalid
Yahya Rushaka. Wacheza mpira wa meza wako wanne, ambao ni Amon Tumaini, Masoud
Mtalaso, Neema Mwaisyula na Fathiya Paz, ambao wako chini ya kocha Ramadhani
Othman Suleiman.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Juliana Shonza, anatarajia kujiunga na timu hiyo baadae.
No comments:
Post a Comment