Monday, 9 April 2018

Nyota Kibao Kushiriki Ngorongoro Race 2018

Mbio za Ngorongoro Race kabla ya kuanza mwaka jana.

Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA nyota wamethibitisha kushiriki mbio za mwaka huu za Ngorongoro Race zitakazofanyika Aprili 21,  imeelezwa.

Mkurugenzi wa mbio hizo, ambazo zinafanyika kwa mwaka wa 11 sasa, Meta Petro alisema jana kwa njia ya simu kuwa, tayari wanariadha wengi nyota wamethibitisha kushiriki mbio hizo.
Wanariadha wakichuana katika mbio za mwaka jana mjini Karatu.
Baadhi ya wanariadha nyota waliothibitisha kushiriki ni pamoja na Fabian Joseph, Said Makula, Fabian mdogo, Dickson Marwa, Sarah Ramadhani, Jaquline Sakilu, Stephano Huche, Failuna Abdi na wengine.

Makula, Sarah na Huche wamo katika timu ya Tanzania iinayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola iliyoanza Gold Coast, Australia kuanzia Aprili 4 hadi 15.
Ofisi ya Ngorongoro Race iliyopo Karatu mkoani Arusha.
Petro alisema kuwa tayari zaidi ya wanariadha 200 wamejiandikisha kutaka kushiriki mbio hizo, ambazo zimekuwa zikifanyika katika kipindi cha masika na kuanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro na kumalizikia katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.
Mkurugenzi wa Ngorongoro Race, Meta Petro akimvisha medali Mkurugenzi wa Ufundi wa mbio hizo, Filbert Bayi kama shukrani kwa kazi nzuri ya kuandaa mbio hizo mwaka jana katika Uwanja wa Mazigira Bora.
Mshindi wa kwanza wa mbio za kilometa 21 ataondoka na Sh milioni 1 wakati mshindi wa pili atapata Sh 500,000 wakati watatu atapewa Sh 250,000 huku kukiwa pia na mbio za kilometa tano na 2.5 kwa watoto.
Mwanariadha wazamani wa Tanzania, Mzee John Stephen Akhwari akizungumza na Mkurugenzi wa Ngorongoro Race, Meta Petro baada ya mbio za mwaka jana kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu mkoani Arusha.

No comments:

Post a Comment