Monday, 30 April 2018

Yanga Wamuangushia Jumba Bovu Kessy


Na Mwandishi Wetu
KOCHA msaidizi wa Yanga, Shedrack Nsajigwa ameeleza kuwa kipigo walichokipata juzi Jumapili kutoka kwa mahasimu wao Simba SC kimesababishwa na beki wao Hassan Kessy kutolewa kwa kadi nyekundu.

Kessy alimchezea rafu mbaya Asante Kwasi dakika ya 48 na kulazimika kuoneshwa kadi ya pili ya njano na kuifanya Yanga iliyokuwa kwa bao 1-0 kucheza pungufu mpaka mwisho wa mchezo.

Bao pekee lililoipa ushindi Simba kwenye mchezo huo, lilifungwa na Erasto Nyoni dakika ya 37 akimalizia kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na Shiza Kichuya.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, Nsajigwa alisema kuwa licha ya kuwa nyuma ya bao hilo moja lakini kabla ya Kessy kutolewa walikuwa wamefanikiwa kuwadhibiti wapinzani wao na walikuwa na uwezo wa kusawazisha bao hilo na kuongeza lingine.

Alisema kuwa walifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kumtoa Raphael Daud na kumuingiza Juma Mahadhi ili kuongeza nguvu safu yao ya ushambuliaji lakini mipango yao hiyo ikafeli.

Aliongeza kuwa licha ya kufungwa lakini mchezo umeshapita hivyo akili zao zote kwa sasa wanazielekeza kwenye michezo yao yote iliyombele yao ikiwemo ile ya michuano ya kimataifa.

“Tulimuingiza Mahadhi ili kumsogeza Yusuph Mhilu juu kuongeza mashambulizi, lakini haikusaidia kutokana na kadi nyekundu, ilikuwa ni kadi ya pili ya njano hivyo ilikuwa lazima kadi nyekundu.

“Kabla ya kadi nyekundu tulikuwa tumebalansi lakini baada ya kutolewa ndio wakatuzidi ila kikubwa sasa tunaangalia m ichezo yetu ijayo,” alisema Nsajigwa.

No comments:

Post a Comment