Na Mwandishi Wetu
JOHN Bocco na Emmanuel Okwi walizidi kuipeleka Simba jirani na taji la Ligi Kuu Bara baada ya kuiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Ushindi huo
unaifanya Simba izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, kwani sasa
inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 58 juu ya mabingwa watetezi Yanga
walio na pointi 47 na mechi mbili kibindoni.
Mabao ya Simba
yalifungwa katika kila kipindi kwenye mechi hiyo hiyo ambayo vinara hao
walitawala katika vipindi vyote.
Prisons
ilionekana kuibana Simba katika dakika za mwanzo kabla ya kusalimu amri na
kuruhusu bao la Bocco dakika ya 35 kabla ya kujikuta wakicheza mchezo wa
kujilinda zaidi katika kipindi cha pili.
Bocco alifunga
bao hilo la kuongoza kwa kuuwahi kwa kichwa mpira wa krosi wa Erasto Nyoni
uliogonga mwamba kabla ya kuujaza wavuni.
Okwi
aliifungia Simba bao la pili katika dakika ya 80 na kuendelea kukifukuzia kiatu
cha dhahabu kwa kufikisha mabao 18 kwenye ligi.
Penalti ya
Okwi ilitolewa na mwamuzi Shomari Lawi wa Kigoma baada ya Jumanne Elifadhili
kumfanyia madhambi Bocco akiwa kwenye eneo la hatari, Elifadhili alioneshwa
kadi nyekundu.
Katika mechi
hiyo Simba ilikosa mabao mengi hasa kupitia kwa mchezaji wake Shizza Kichuya
aliyekosa mabao dakika ya kwanza, 50, 62 na 70.
Mechi nyingine za ligi hiyo ni Ndanda ikiwa nyumbani Nangwanda Sijaona imeshindwa kutamba
kwa kukubali ‘kupapaswa’ na Ruvu Shootinga kwa mabao 3-1, huku Kagera Sugar
ikishinda 2-1 dhidi ya ndugu zao Mtibwa Sugar kwenye uwanja wake wa nyumbani
Kaitaba.
No comments:
Post a Comment