Beki wa Yanga, Hassan Kessy (kushoto) akijaribu
kuwatoka wachezaji wa Singida United, Kiggi
Makasi (kulia) na Mudathir Yahya wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania
Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana na kumalizika kwa sare ya
1-1.
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga jana
walipunguzwa kasi katika mbio za kutetea taji hilo baada ya kulazimishwa sare
ya 1-1 na Singida United, katika mchezo wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 47 na
kuifanya sasa kupitwa na watani zao Simba kwa pointi tano.
Kwa matokeo hayo ni dhahiri kuwa Yanga imeendelea kuwa
mnyonge wa Singida kwa kushindwa kuifunga kwa mara ya tatu. Mchezo wa raundi ya
kwanza kwenye Uwanja wa Namfua walitoka suluhu, wakati katika Kombe la
Shirikisho (FA), walifungana 1-1 kabla ya Yanga kutolewa kwa penalti 4-2.
Sare hiyo inazidi kuisafishia Simba nafasi ya kuwania
taji la ligi ikiendelea kubaki kileleni kwa pointi 52 na Yanga ikiendelea kuwa
katika nafasi ya pili kwa pointi 47 zikitofautiana pointi tano, huku Singida
United ikifikisha pointi 37.
Singida ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la uongozi
dakika ya kwanza lililofungwa na Salita Kambale baada ya kupata krosi nzuri ya Kigi
Makasi .
Katika mchezo huo, dakika 45 beki Abdallah Shaibu
‘Ninja’ aliisawazishia Yanga kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Ibrahim
Ajibu.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Yanga 1-1. Kipindi
cha pili Yanga walikuja kwa kushambulia zaidi lakini tayari Singida United
walionekana kama wanaitaka sare baada ya kuonekana kuzuia zaidi.
Awali, kipindi cha kwanza Singida ilifanya mabadiliko
kwa kuwatoa kipa Mustapha Barthez na kuingia Peter Manyika dakika ya 38. Pia,
dakika ya 42 Shafiq Batambuze alitolewa na kuingia Salum Chuku na dakika ya 68
alitoka Nizah Khalifan na kuingia Yusufu Kagoma.
Yanga ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga na
kushindwa kuzitumia kupitia kwa Yusufu Mhilu, Ajibu na Chirwa kwa vipindi
tofauti.
Pia, ilifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuwatoa
Pius Buswita na kuwaingiza Juma Mahadhi dakika ya 73, Ajibu na kuingia Geofrey
Mwashiuya dakika 78 lakini haikusaidia chochote kwani hadi mpira unaisha
matokeo yaliendelea kubaki sare ya bao 1-1.
Vikosi
vilikuwa: Yanga; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Haji
Mwinyi, Abdallah Shaibu, Kelvin Yondani, Papy Kabamba, Yusufu Mhilu, Pius
Buswita, Obrey Chirwa, Raphael Daud na Ibrahim Ajibu.
Singida
United; Ally Mustapha, Miraji Adam, Shafik Batambuze, Malik
Antir, Kennedy Juma, Mudathir Yahya, Deus Kaseke,Kenny Ally, Kambale Salita,
Nizah Khalifan na Kigi Makasi.
No comments:
Post a Comment