Na Mwandishi Wetu
BINGWA wa
Ngorongoro Race, Mkenya Joseph Mbatha aliifanya kweli baada ya kushinda
tena mbio za Heart Marathon zilizofanyika jijini Dar es Salaam na kutwaa Sh
milioni 2 leo.
Ngorongoro
Race zilifanyika mkoani Arusha Aprili 21 na Mbatha alishinda mbio hizo na
kuondoka na Sh milioni 1 baada ya kutumia saa 1:04:54.12 kabla ya kushinda tena
jana Heart Marathon kilometa 21 kwa kutumia saa 1:07.01.
Ushindi huo
mbali na kufanya Wakenya kuendelea katika mbio za Tanzania, pia unamfanya
mwanariadha huyo kuondoka na Sh milioni 3 ndani ya wiki moja tu na huenda
akawepo katika Tulia Marathon itakayofanyika Mbeya Mei 6 mwaka huu.
Katika Heart
Marathon, mshindi wa pili katika kilometa 21 kwa wanaume, alikuwa Gabriel
Gerald wa Arusha aliyemaliza kwa kutumia saa 1:07:02 wakati Mkenya mwingine
George Owaiyaki alimaliza watatu kwa kutumia saa 1:07:11 huku Joel Kimutae wa
Kenya alimaliza wanne kwa saa 1:07.18.
Kwa upande wa
wanawake katika mbio za kilometa 21, Faith Kipsum wa Kenya alimaliza wa kwanza
kwa kutumia saa 1:15:17 wakati wa pili alikuwa mwanariadha wa Arusha, Sarah
Rawiadhau aliyetumia saa 1:16.10 huku
Betrice Chelop wa Kenya alimaliza wa tatu kwa kutumia saa 1:17.33 na Failuna
Abdi alimaliza katika nafasi ya nne kwa kutumia saa 1:17.33.
Katika mbio
za kilometa 10 kwa wanawake, mwanariadha mkongwe wa Tanzania, Mary Naali
alializa wa kwanza kwa kutumia dakika 35:11.17 huku Fabiola William wa Singida
alimaliza wa pili kwa kutumia dakika 36:35.39 wakati Neema Paulo wa Arusha pia
alimaliza wanne kwa dakika 38:12.37.
Mbio hizo
ziliingia dosari baada ya baadhi ya wanariadha kukimbia bila namba licha ya
kusajiliwa na kulipa kiingilio na kuleta changamoto kwa waandaaji na
wasimamizi.
Katibu Mkuu
wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema kabla ya kutolewa kwa zawadi
kuwa mbio hizo zimekumbwa na changamoto kadhaa, ambazo zinatakiwa kurekebishwa
mwakani ili ziendelee kuwa kubwa.
Pia alitaka
wanariadha wa Tanzania kutowaogopa Wakenya licha ya kuja na kushiriki mbio
nchini na kuondoka na zawadi za washindi, ambapo aliwataka wanariadha wa
Tanzania kujiandaa vizuri ili kupambana na kuwashindana Wakenya.
Waandaaji
waliandaa jumla ya Sh milioni 16 kwa ajili ya zawadi za washindi, ambapo
mshindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake, kila mmoja aliondoka na kitita cha
Sh milioni 2.
No comments:
Post a Comment