Sunday 16 February 2020

TAKUKURU Kubaini Mamluki Michezo Mei Mosi 2020


Wajumbe wa Kamati ya Michezo ya mashindano ya Mei Mosi wakiwa kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro

 Na Bahati Mollel, Morogoro
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) mkoa wa Mwanza itashirikishwa kwenye Michezo ya Mei Mosi inayotarajiwa kuanza Aprili 16-29, 2020 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo, endapo kutakuwa na timu za Wizara, Taasisi za Umma  na Binafsi zitawatumia wachezaji wasiokuwa watumishi wao halali.

Katibu wa Kamati ya michezo hiyo, Moshi Makuka, alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro, ambapo suala hilo limewekwa kwenye kanuni namba 13 kati ya 15 zilizopitishwa na wajumbe wote walioshiriki kwenye kikao hicho.

Makuka alisema mbali na Takukuru kushirikishwa kubaini uhalali wa mchezaji aliyesajiliwa na timu iliyomchezesha, pia viongozi wote walioshiriki kumsajili mchezaji huyo wataripotiwa kwenye taasisi hiyo, ili sheria za nchi zichukue mkondo wake.

       Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo ya mashindano ya Mei Mosi, Moshi Makuka  (aliyenyoosha mikono) akisisitiza jambo kwenye kikao cha Kwanza cha maandalizi ya michezo hiyo kilichofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani Morogoro


“Haya mashindano yanajumuisha watumishi halali wa taasisi na wizara hivyo hairuhusiwi kuwachezesha wachezaji ambao sio watumishi halali, kwa lengo la kujipatia ushindi, hili ni katazo na kanuni yetu ipo wazi kabisa, hivyo timu zisithubutu kuja na wachezaji hao kabisa,” alisisitiza Makuka.

Alizitaja adhabu ambazo timu itakayobainika kumtumia mamluki ni pamoja na viongozi wake watafungiwa kushiriki michezo hiyo kwa muda wa miaka miwili na nakala ya barua itawasilishwa kwa Mwajiri wake; timu itatozwa faini  ya Tshs. 500,000; timu husika itapokonywa ushindi endapo itakuwa imeshinda; timu itaondolewa kwenye mashindano.

Kamati imesema mamluki wanadhibitiwa kwa wanamichezo kuwa na vitambulisho halisi vya kazi, Kadi ya Bima ya Afya, Kadi ya Mfuko wa Jamii na hati ya Malipo ya mshahara za miezi miwili ‘salary slip’.

Hatahivyo, Makuka alisema timu zote shiriki zinatakiwa kuwahi mkoani Mwanza tarehe 14 Aprili, 2020 ambapo ndipo sherehe za Sikukuu za wafanyakazi zitafanyika Kitaifa kama ilivyotangazwa awali, ambapo timu itakayochelewa hadi tarehe 20 Aprili, 2020 itakuwa imejiondoa kwenye michezo hiyo.

“Timu ikichelewa inawapa shida na kuwaumiza wachezaji kwa kuwa watacheza mfululizo ili kwenda na ratiba, hadi kufikia michezo yao iliyosalia, hivyo hii hatutaki kwani michezo itakuwa haina ushindani kwa kuwa wachezaji wa timu moja watakuwa wamechoka kwa kucheza mfululizo wa mechi mbili au tatu kwa siku, hivi huu ni mwezi wa pili muanze kufuatilia ruhusa za wachezaji wenu,” alisema Makuka.

Kamati inategemea ushiriki wa timu zaidi ya 25, kwa kuwa zinaongezeka kila mwaka ambapo mwaka jana zilishiriki timu 23. Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na soka, netiboli, kuvuta kamba, baiskeli, riadha, karata, bao na draft.

Pia Makuka amesisitiza timu shiriki kulipa ada ya ushiriki kwa wakati, ili fedha hizo zitumike katika ulipaji wa gharama mbalimbali za uendeshaji wa mashindano hayo.

Ada ya ushiriki ni Tshs. 1,000,000 ambapo kila timu inatakiwa kulipa mapema kabla ya tarehe 6 Aprili, 2020, ili timu ziweze kupewa kadi za ushiriki zitakazofanikisha usajili wao.

Halikadhalika Makuka amesema timu zote zilizotwaa vikombe kwa kuwa washindi wa Kwanza hadi wa tatu wanatakiwa kurejesha vikombe walivyoshinda kabla yatarehe 29 Machi, 2020 na timu itakayochelewa utatozwa faini ya Tshs. 200,000.

Wakati huo huo, Makuka amesema timu zinaruhusiwa kushiriki kwenye michezo ya mashirikisho mbalimbali yakiwemo ya Shimiwi, Shimmuta na Mei Mosi, na sio kusubiri michezo ya shirikisho moja, ambayo kwa wakati huo inakuwa haijafanyika kwa sababu mbalimbali.

TAA WATAKIWA KUTUMIA VIZURI MFUMO WA TANEPs


Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), akimkabidhi cheti cha kufuzu mafunzo ya mfumo wa Manunuzi kwa njia ya Mtandao (TANEPs),  Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wa Bi. Irene Sikumbili (wa pili kushoto). Mafunzo hayo yaliendeshwa na Mwezeshaji Kenneth Nnembuka kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) (kulia)

Na Bahati Mollel
KAIMU Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdi Mkwizu amewataka wahitimu wa mafunzo ya mfumo wa Manunuzi kwa njia ya mtandao (TANEPs), kuutumia vyema mfumo huo ili kuongeza ufanisi katika taratibu za ununuzi wa Umma kwa maslahi ya taasisi na Taifa kwa ujumla.

Akifunga mafunzo hayo ya siku tano jana yaliyokuwa yakifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Watu Mashuhuri wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Mkwizu alisema tayari Mamlaka imeanza kutumia mfumo huo ulioagizwa na serikali kupitia Mamlaka ya udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Ofisa Manunuzi na Ugavi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Honest Mushi (mwenye fulana) akipokea cheti cha kufuzu mafunzo ya mfumo wa Manunuzi kwa njia ya Mtandao (TANEPs), kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Abdul Mkwizu. Kulia ni Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Bw. Kenneth Nnembuka kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA)

Mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Kenneth Nnembuka kutoka PPRA, aliwataka wahitimu kuanza haraka kutumia maarifa waliyoyapata ili wasije wakasahau. Pia aliwasihi kutosita kuomba msaada mara wapatapo mkwamo kuhusu mfumo huo mpya.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi cha TAA, Bw. Josephat Msafiri alishukuru uongozi wa juu wa TAA kukubali kufanyika kwa mafunzo hayo muhimu yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji wa ndani wa taasisi.

Aliahidi kuendelea kutumika bila kuharibu kada hiyo.


Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Josephat Msafiri (wa pili kulia) akiandika mambo mbalimbali yanayofundishwa na Mwezeshaji Kenneth Nnembuka kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), katika mafunzo ya mfumo wa manunuzi kwa njia ya mtandao (TANePs), yanayoendelea kwenye ukumbi wa Mikutano wa Watu Mashuhuri wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (VIP -JNIA-TB2).
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani ya Taasisi, Bi Irene Sikumbili aliweka msisitizo kwenye matumizi sahihi ya mfumo kwa mujibu wa miongozo, taratibu, kanuni na sheria za serikali.

Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Paul Rwegasha, alisisitiza mapendekezo ya TAA na wadau mbalimbali kuhusu changamoto za kimfumo yafanyiwe kazi ili kuepusha uwezekano wa ukwamishaji wa huduma viwanjani.
Naye mratibu wa mafunzo hayo, Bw. Soud Saad amesema mafunzo hayo yalishirikisha watendaji wakuu wa TAA; Wakaguzi wa ndani; wataalam wa TEHAMA na Wataalam wa Ununuzi na Ugavi kutoka Makao Makuu na JNIA.

Wednesday 5 February 2020

Kamwelwe Ataka MAB Kuweka Uzalendo Mbele

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Mshauri, Julius Ndyamukama (aliyesimama kulia) akitoa taarifa fupi kwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe (mbele), wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya TAA, (MAB) uliofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Jengo la TPA (One Stop Centre) jijini Dar es Salaam. 

Na Bahati Mollel,TAA
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe ameiasa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), kutanguliza Utaifa na Uzalendo mbele katika majukumu yao.

Kauli hiyo ameitoa mwishoni mwa wiki katika halfa ya uzinduzi wa Bodi hiyo, ambao umefanyika kwenye Jengo la Bandari nchini (TPA One Stop Centre) lililopo jijini Dar es Salaam.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwaasa kwamba, nafasi hizi mlizopewa ni kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa huku mkitanguliza maslahi mapana ya taifa na uzalendo mbele”. Amesema Waziri Kamwelwe
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe (mbele) mwishoni mwa wiki akiongea na Walioteuliwa kuunda Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), pamoja na Menejimenti ya TAA wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo katika Jengo la TPA (One Stop Centre) jijini Dar es Salaam.
Pia Waziri Kamwelwe ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha inashirikiana bega kwa bega na menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na taasisi za serikali hususan Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika ujenzi wa viwanja vingi zaidi ya wanavyovisimamia 58 kwa lengo ya kuviongeza, ili ndege za Shirika la ndege Tanzania (ATCL) na mashirika mengine yaweze kupanua wigo wa safari.

Halikadhalika amesema ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege ukaimarishwe, ingawa bado kunachangamoto ya kukosekana kwa uzio wa ndani na nje ya viwanja vya ndege, ambapo pia suala la ugonjwa wa homa ya virusi vya Corona ulioanzia nchini China lipewe kipaumbele kwa kuzingatiwa maslahi mapana ya Taifa yazingatiwe.

“Hili la ugonjwa wa Corona liangaliwe kwa ukaribu zaidi ili viwanja vya ndege visiwe ndio njia ya kuingiza ugonjwa huu, pia usalama wa watendajikazi uangaliwe pia,” amesema na kuongeza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe (wa nne kulia), akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti Dkt Masatu Chiguma (wa nne kushoto) na Wajumbe ya Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), baada ya kuizindua Bodi hiyo mwishoni mwa wiki kwenye Jengo la TPA.
“... Vilevile mkahakikishe kuwepo na usimamizi mzuri wa wa ardhi na miundombinu ya viwanja vyetu ikiwemo Jengo la Tatu la abiria –JNIA na utoaji wa huduma bora zaidi kwa wateja, ukiangalia kwa sasa ni viwanja vichache tu ndio vina hati na hili sio jambo jema, hakikisheni viwanja vyote vinapimwa na hati kupatikana, kwani itasaidia kuongeza uhalali na kuongeza mapato ya TAA kwa kutumia ardhi hiyo,” amesema Waziri Kamwelwe.

Pia ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha TAA inapata “control number” ili malipo mbalimbali yatafanyika kupitia huko, ambapo pia ameitaka kubuni njia mbalimbali za kuendesha viwanja vya ndege kibiashara, wakati sasa suala la TAA kuwa Mamlaka zaidi badala ya sasa kuwa Wakala pamoja na kwamba lipo chini ya Wizara linahitaji msukumo wa Bodi hiyo.
   Menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe (wanne kutoka kushoto), na Mwenyekiti, Dkt Masatu Chiguma na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (MAB), iliyozinduliwa mwishoni mwa wiki kwenye Jengo la TPA.
Hatahivyo, Waziri Kamwelwe amesema pamoja na TAA kuwa na mafanikio bado inakabiliwa na changamoto za kushindwa kuboresha miundombinu mbalimbali iliyopo viwanjani.

Bodi hiyo inaundwa na Mwenyekiti Dkt. Masatu Chiguma na wajumbe ni Mhandisi Ven Kayamba, Dkt. Paschal Mugabe, Mhandisi Daniel Kiunsi, Mhandisi Christopher Mukoma na Alex Haraba.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAA,  Mhandisi Mshauri, Julius Ndyamukama amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikikua tangu kuanzishwa kwake hadi sasa, na kutolea mfano wa mapato kuongezeka kutoka Shilingi Bilioni 6.3 hadi kufikia Bilioni 105.2 kwa mwaka, ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 1,570.

Pia amesema Mamlaka ilianza na ikiwa na miruko na mituo ya ndege 62,221 kwa mwaka na sasa imefikia 146,593 kwa mwaka ni sawa na ongezeko la asilimia 135.6.

Kwa upande wa abiria, amesema ilianza ikiwa na idadi ya abiria 846,906 kwa mwaka na sasa imefikia 3,473,658 kwa mwaka ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 310.

Naye Mwenyekiti wa MAB, Dkt. Masatu Chiguma, alimuahidi Waziri kuwa atafanya kazi bega kwa bega na TAA, ili kufanikisha malengo yalilowekwa.