Friday, 27 October 2017

Fifa yaongeza zawadi Kombe la Dunia

ZURICH, Uswisi

MATAIFA 32 yatakayoshindana katika fainali za Kombe la Dunia 2018 yatagawana kiasi cha dola za Marekani milioni 400 (sawa na sh bilioni 898) katika zawadi ikiwa ni ongezeko la asiliia 12 ya fedha za mashindano ya mwaka 2014, Fifa imesema.

Katika taarifa yake jana Shirikisho hilo la Kimataifa la Soka limesema kuwa fedha zawadi katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika Brazil zilikuwa dola za Marekani milioni 358.

Imeelezwa kuwa Ujerumani ambaye ni bingwa wa Kombe la Dunia alindoka na kitita cha dola za Marekani milioni 35, huku mshindi wa pili Argentina alipata dola milioni 25.

Tofauti, nchi ambazo zitashindwa kuvuka hatua ya makundi kila moja itapokea kiasi cha dola za Marekani milioni 8.

Katika mkutano wa Fifa uliofanyika Kolkata, bodi hiyo ya Fifa pia imepitisha taratribu za kuomba uenyeji wa Kombe la Dunia kwa ajili ya mwaka 2026.

Huku ikithibitisha tarehe za mashindano mbalimbali, yakiwemo ya Kombe la Dunia yatakayofanyika Falme za Kiarabu na yale ya wanawake ya mwaka 2019 yatakayofanyika Ufaransa.


Fainali za Kombela Dunia za mwaka 2018 zitafanyika kuanzia Desemba 12 hadi 22, wakati yale ya wanawake ya mwaka 2019 yamepangwa kufanyika kuanzia Juni 7 huku fainali ikifanyika Julai 7.

Wednesday, 25 October 2017

TB Three kutumia mitambo ya Visa ya Elektroniki

Kaanankira Mbise, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akieleza namna abiria anavyopata huduma ya viza mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela.

Na Mwandishi Wetu

JENGO la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) linalotarajiwa kukamilika Desemba 2018, litafungwa mfumo wa huduma ya viza kwa njia ya mtandao (e-visa), ambao utarahisha na kuharakisha upatikanaji wake.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji cha JNIA, Bw. Kaanankira Mbise amemwambia jana Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye alipotembelea eneo la uombeaji viza kwa abiria wa kimataifa wanaowasili, kuwa wanatarajia kutumia huduma hiyo ambayo ni rahisi na haraka.

“Tayari mkakati umeanza wa kuanzisha huduma hii ya e-visa hivyo tukifanikiwa utafungwa katika jengo hili jipya, ambapo itasaidia kwa abiria kuipata huduma hiyo kwa haraka kwani itatumia mtandao,”  amesema Bw. Mbise.

Hata hivyo, Bw. Mbise amesema kwa sasa wameboresha huduma hiyo kwa wasafiri wanaowasili katika jengo la pili la abiria (JNIA-TBII) , ambapo tayari wamepatiwa mashine nne za kisasa zinazosaidia kupunguza msongamano wa abiria wenye kuhitaji huduma hiyo, hususan kipindi cha mchana chenye ujio wa ndege nyingi za nje ya nchi.

“Hizi mashine zimeharakisha upatikanaji wa huduma kwani tumeweza kuhudumia abiria wengi kwa wakati mmoja, na msongamano umepungua kiasi tofauti na awali mashine zilikuwa chache.” amesema Mbise.

Naye Mhe. Mhandisi Nditiye amesema baada ya ziara yake amegundua mashine za viza ni za muda mrefu na zinahudumia abiria mmoja kwa mrefu, na tayari ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuwasilisha kwa maandishi mapendekezo yao ya namna ya kuharakisha huduma hiyo, ili serikali iyafanyie kazi kwa kusaidia kuondoa kero hiyo.

“Nimegundua kuna baadhi ya mashine za viza zimeongezwa lakini pia zilizopo zimechoka kwani ni za muda mrefu na zinahudumia abiria mmoja kwa muda mrefu na hii inaharibu sifa ya kiwanja chetu kwa wageni wanaokuja hapa nchini,” amesema Mhandisi Nditiye.

Hata hivyo, amesema wanampango wa kuongeza madirisha ya benki yanayolipia viza hizo ili kuharakisha huduma hiyo, ambapo sasa ni machache kulinganisha na idadi kubwa ya abiria wanaowasili kwa ndege kubwa. Ndege hizo ni Emirates, Etihad, Oman Air, Qatar, South Africa Air na Ethiopia, ambazo zimekuwa zikipishana kwa muda mfupi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),  Richard Mayongela (aliyenyoosha mkono), akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kulia) wakiwa kwenye eneo la abiria wanaowasili kutoka nje ya nchi, katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA).

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Richard Mayongela amesema tayari wanampango wa kuongeza upana wa eneo hilo la wasafiri wanaowasili wa kimataifa, ambapo sasa kumekuwa na msongamano kutokana na ufinyu wake.

“Hili jengo linazaidi ya miaka 30 na ukiangalia abiria waliokuwa wamekadiriwa wakati ule lilikuwa likikidhi mahitaji, lakini sasa abiria wameongezeka na eneo limekuwa dogo, hivyo tayari tumeanza kwa kuondoa baadhi ya ofisi ili kuongeza upana wake, ninaimani litapunguza msongamano uliopo sasa,” amesema Bw. Mayongela.  

Lakini pia Bw. Mayongela amesema sasa wapo katika mazungumzo na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), ili kuangalia namna bora ya kuzipangia muda ndege zinazopishana muda mdogo kwa wakati wa mchana ili ziachiane muda mrefu, ambapo kutasaidia kupunguza msongamano


Awali eneo hilo linakumbwa na changamoto kubwa ya msongamano wa abiria wanaohitaji huduma ya viza baada ya uchache mashine zinazosimamiwa na Idara ya Uhamiaji zilizokuwepo na kufanya abiria wanaohitaji huduma hiyo kutumia muda mrefu kuipata.  

Tuesday, 24 October 2017

Chaneta walivyokabidhiana `ofisi' Uwanja wa Taifa

Mwenyekiti mpya wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Devota Marwa akizungumza baada ya kukabidhiwa nyaraka mbalimbali za chama hicho na mwenyekiti wazamani Annie Kibira kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wazamani wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) akizungumza kabla ya kukabidho `ofisi' kwa mwenyekiti mpya wa chama hicho, Dk Devota Marwa. Kulia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji Kilongozi Mohamed. Makabidhiano hayo yalifanyikia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Makamu mwenyekiti wazamani wa Chaneta, Zainabu Mbiro akipanda katika gari la Chama jhicho aina ya Noah wakati akilikabidhi kwa uongozi mpya wa Chaneta kwenye Uwanja wa Taifa. 

Mwenyekiti Mpya wa Chaneta, Dk Devota Marwa akikagua garia aina ya Noah baada ya kukabidhia nyaraka mbalimbali na uongozi uliopita pamoja na gari hilo.
Mwenyekiti wazamani wa Chaneta, Annie Kibira (kushoto) akimkabidhi Katiba mwenyekiti mpya wa chama hicho, Dk Devota Marwa wakati wa makabidhiano ya `ofisi' yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia katikati ni Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa, Bahati Msofe.

Ronaldo, Zidane wang'ara tuzo za Fifa 2017

LONDON, England

CRISTIANO Ronaldo ametangazwa kuwa ndiye mchezaji bora wa dunia wa kiume katika tuzo za Shirikisho la Kimataifa la Soka 2017 zilizofanyika jijini hapa.

Mshambuliaji huyo wa Real Madrid na Ureno aliwapiga kumbo mwenzake wa Barcelona Lionel Messi na yule wa Paris St-Germain, Neymar katika mbio za kutwaa tuzo hiyo.

Ronaldo, 32, aliisaidia Real Madrid kutwaa mataji mawili, likiwa lile le La Liga, ambalo walilitetea na La Liga msimu wa mwaka 2016-17.

Lieke Martens wa Barcelona na Uholanzi alishinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia wakike, huku kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane alitangazwa kuwa kocha bora wakiume na Mholanzi Sarina Wiegman amekuwa kocha bora wakike.

Mchezaji wa Arsenal Olivier Giroud alipokea tuzo ya Puskas kwa ajili ya bao lake bora 2017 walipocheza dhidi ya Crystal Palace Januari.

Tofauti ya Ballon d'Or na Fifa?

 

Hii ni mara ya pili kufanyika tuzo hizo za Fifa za soka, ambazo ni tofauti na zile za Ballon d'Or.

Tuzo ya Ballon d'Or ilikuwa ikitolewa na jarida la Soka la Ufaransa tangu mwaka 1956, lakini Fifa ilijitenga na tuzo hizo na kuanzisha zake.

Badala yake, ilianzisha tuzo za tuzo za mchezaji bora wa Fifa, ambapo Ronaldo ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo hiyo Januari.

Kura za kumpata mchezaji na kocha bora zinapigwa na manahodha wa timu za taifa na makocha, waandishi wa habari walioteuliwa, na kwa mara ya kwanza, kura za katika mtandao zilipigwa na mashabiki. Kila kundi lilikuwa na asilimia 25 ya kura.

Cristiano Ronaldo

Ni mwaka mwingine wa kuvutia kwa Ronaldo, ambaye aliyetwaa tuzo ya kwanza ya mchezaji bora wa Fifa wa Dunia baada ya kuiongoza Ureno kutwaa taji la Euro 2016.

Mwaka huu alifunga mabao mawili wakati Real Madrid ikishinda 4-1 dhidi ya Juventus katika fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na pia alizifumania nyavu mara 25 katika mechi 29 alizoichezea klabu yake katika La Liga ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika miaka mitano.

 

"Tuko England kwa mara ya kwanza, na tumeshinda kwa mara ya pili mfululizo. Huu ni wakati mzuri kwangu, “alisema Ronaldo alipokuwa akizungumza wakati wa kukabidhiwa tuzo hiyo.

Wachezaji watatu wakiume

Cristiano Ronaldo - 43.16 %  Lionel Messi - 19.25 %           Neymar - 6.97%

Messi alimpigia kura mchezaji mwenzake wa Barcelona Luis Suarez kama mchezaji bora, wakati Ronaldo naye pia alimpigia mchezaji mwenzake wa Real, Luka Modric.

Kocha wa England Gareth Southgate alimpigia kura Ronaldo.

 

Mchezaji bora wakike

Martens, 24, alikuwa mhimili wa timu ya taifa ya Uholanzi katika ushindi wa timu hiyo katika mashindano ya Mataifa ya Ulaya, ambapo alishinda tuzo ya mashindano hayo.

Fifpro World XI

 

Fifa imefanya mabadiliko matatu katika kikosi cha mwaka 2016. Kipa Gianluigi Buffon alimbadili Manuel Neuer, wakati mchezaji wa AC Milan Leonardo Bonucci alimbadili mchezaji wa Barcelona, Gerard Pique katika nafasi ya beki bora na mchezaji wa PSG Neymar ameshika nafasi ya ushambuliaji bora hiyo badala ya Luis Suarez.

Orodha ya wachezaji hao watano ni kutoka Real Madrid, wawili Barcelona, wawili PSG, mmoja Juventus na mmoja AC Milan. Hakuna mchezaji wa Ligi Kuu ya England aliyomo katika kikosi hicho.

Kocha bora

Real ilimaliza msimu uliopita ikiwa bingwa wa Hispanuia na kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012 na kutwaa ubigwa wa Ulaya kwa mara ya pili mfululizo.

Zidane alishinda tuzo hiyo akimshinda kcha wa Chelsea Antonio Conte, ambaye alitwaa taji la Ligi Kuu katika msimu wake wa kwanza England, na yule wa Juventus, Massimiliano Allegri, aliyeiongoza timu yake kutwaa mataji mawili ya Serie A na lile la Coppa Italia.

 Makocha watatu wakiume

Zinedine Zidane - 46.22%      Antonio Conte - 11.62%           Massimiliano Allegri - 8.78%

Kocha bora wakike

Mholanzi Wiegman alioongoza timu yao ya taifa kutwaa taji la Euro 2017 katika ardhi ya nyumbani, ambapo timu hiyo ilicheza soka safi la kuvutia.

Hilo lilikuwa taji lao la kwanza kubwa la kimataifa kwa timu ya wanawake baada yakuifunga Denmark katika fainali.

Tuzo ya Puskas

Bao bora la mwaka 2017 ni lile lililofungwa na mchezaji wa Arsenal, Giroud.

Bao hilo lilifungwa katika mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Palace siku ya mwaka mpya, ambapo mshambuliaji huyo Mfaransa alifunga bao safi aliunganisha krosi ya Alexis Sanchez niliyopigwa nyuma yake.

Kipa bora

Bingwa wa Kombela Dunia, na mshindi mara 10 wa taji la Serie A, Gianluigi Buffon ndiye mshindi wa kwanza wa tuzo ya kipa bora.

Kipa huyo mkongwe aliisaidia Juventus kutwaa mara sita mfululizo taji la Serie A na kucheza dakika 600 bila kuruhus bao katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.


Buffon, 39, alitwaa tuzo hiyo akiwashinda Keylor Navas, Manuel Neuer, aliyeisaidia Bayern Munich kutwaa Bundesliga.

Naibu Waziri aridhishwa na Ujenzi Terminal Three

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasilian) (kushoto) , Atashasta Nditiye  akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Johannes Munanka wakati alipotembelea kiwanja hicho leo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela. Mwingine ni Ofisa Usalama wa JNIA, Imani Mwakiyarangwe.

 Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amesema kuwa ameridhika na maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya tatu (Terminal III) ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Nditiye ambaye yuko upande wa sekta ya Uchukuzi na Mawasiliani aliyasema hayo leo baada ya kutembelea sehemu zote za JNIA kuanzia Terminal One hadi Three na kujionea mambo mbalimbali.

Ofisa wa zamu wa Uhamiaji kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Kaanankila Mbise akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye (kushoto) wakati alipotembelea kiwanja hicho leo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA),  Richard Mayongela.

Amesema kuwa ameridhishwa jinsi ujenzi huo unavyoendelea, ambao unatarajia kukamilika Septemba mwakani.

Amesema kuwa ujenzi unaendelea vizuri tena kwa kasi kubwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto katika mradi huo, ambazo zinafanyiwa kazi.

Alimtaka mkandarasi, ambaye ni Kampuni ya BAM International kuendelea na kazi bila kusita, kwani Serikali imeshatoa fedha za ujenzi huo.

Amesema kuwa pia amefurahishwa na mipango ya biashara baada ya kumalizika kwa kiwanja hicho, ambapo kutakuwa na migahawa, mahoteli jirani na sehemu hiyo ya Terminal Three.

Amesema amegundua changamoto ndogo ndogo kama suala la mpango wa biashara kuwepo na mahoteli kuzungunguka eneo hilo, ambapo tayari amewaagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kushughulikia hilo.

Kingine ni uchakavu wa mashine za kupozea hewa na mashine za viza kutumia muda mrefu katika Terminal Two, mfano viza ya Ujerumani inakuwa ngumu kushughulikiwa na mashine hizo.

Pia alitaka mlolongo mrefu wa malipo katika benki ya NMB pale kiwanjani cha JNIA Terminal Two kutatuliwa haraka ili kuwapunguzia muda wasafiri.

Mkandarasi anataka kufanya vitu vya ziada na tayari wameshaelekezana naye na atavifanya, kwani viko ndani ya mkataba.

Amesema mikataba mipya katika eneo hilo la Terminal Three litakapokamilika, kipaumbele watapewa wafanyabiashara wazalendo, lakni wale wasafi wasiokuwa wababaishaji.

Naye  Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela amesema kuwa sehemu hiyo ya Termila Three itakapokamilika itahudumia Abiria milioni 6 kwa mwaka, ambao watakuwa wakihudumiwa kwa haraka na kwa nafasi na kuwepo sehemu bora ya kufanya biashara kuliko Terminal Two.

Huduma kwa abiria itakuwa bora zaidi kuliko kule kwa sababu eneo hilio ni la kisasa zaidi.

"Kutokana na huduma bora na ukubwa wa eneo tunatarajia kupata abiria wengi zaidi, "amesema.

Alisema kuwa jengo chakavu la Terminal Two litafanyiwa ukarabati ili kuwa la kisasa, ambapo mifumo mbalimbali itaboreshwa ili kuwahudumia abiria kwa haraka zaidi.

Amesema anaishukuru Serikali kwa kuisaidia TAA katika shughuli mbalimbali kama alivyoahidi Naibu Waziri.

"Kupitia Wizara, huduma mbalimbali zitaboreshwa kama alivyosema Naibu Waziri tupeleke bajeti yetu ili waweze kutusaidia, "amesema.


Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Johannes Munanka amesema kuwa kutakuwa na programu maalum ya kuutangaza uwanja huo kwa wananchi, ambapo aliwataka kuutembelea ili kuona shughuli zake na kujifunza mambo mbalimbali.




Ofisa Usalama wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Imani Mwakiyaragwe akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasilian) (kushoto) , Atashasta Nditiye  . Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Richard Mayongela.

Monday, 23 October 2017

Kozi ya awali ya mafunzo ya Anga yafunguliwa leo

 Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), (wa pili kushoto waliokaa), Johannes Mnaka, mkuu wa chuo cha Anga, Enirisha John (katikati waliokaa). Kushoto waliokaa mkufunzi  Thmarat Abeid, Kulia waliokaa mkufunzi na wa pili kulia ni Fatuma Makimba, ambaye ni Meneja Rasilimali Watu wa JNIA, akiwa pamoja na viongozi wengine na wanafunzi wa kozi ya awali ya Anga leo jijini Dar es Salaam.
 Wanafunzi wa kozi ya awali ya Anga wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo leo jijini Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), Johannes Mnaka akifungua kozi ya awali ya anga katika Chuo cha Anga jijini Dar es Salaam mapema leo.

Lulu akana kusababisha kifo cha Steven Kanumba


Na Mwandishi Wetu

MUIGIZAJI wa Filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa hakusababisha kifo cha mpenzi wake Steven Kanumba na badala yake yeye ndiye angeuawa baada ya kupigwa na panga.

Lulu ambaye amebainisha wazi kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa miezi minne na Kanumba, alikuwa akienda mara kwa mara nyumbani kwake na kwamba walikuwa wanaficha mahusiano yao ili kukwepa mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Akiongozwa na Wakili wake, Peter Kibatala, Lulu alidai mbele ya  Jaji Sam Rumanyika kuwa Aprili 6, 2012 alikuwa nyumbani kwao Tabata na jioni alitaka kwenda kwa marafiki zake Mikocheni kwa ajili ya kwenda klabu.

Alidai walikuwa wakiwasiliana na marehemu Kanumba kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi licha ya kwamba hakutaka kumwambia kama anataka kutoka na marafiki zake kwa sababu alikuwa hapendi atoke.

"Marehemu alikuwa akinipigia simu mara nyingi kujua nipo wapi ndipo nilimwambia kuwa nataka kutoka ili asinisumbue nikamueleza kuwa nitapita nyumbani kwake kumuaga, lakini sitokaa sana. Kabla ya kufika alinipigia na kunambia kuwa ataacha mlango wazi hivyo nipite mpaka chumbani..nyumba niliizoea hata asipokuwepo nilikuwa naenda," alidai Lulu.

Aliendelea kudai kuwa alimkuta Kanumba chumbani akiwa na taulo huku akipaka mafuta kichwani, ambapo yeye alikaa kitandani na kusalimiana.

"Kama tunavyojua marehemu alikuwa anajipenda sana hivyo alikuwa ameweka superblack kwenye nywele zake na kwamba alikuwa na mafuta maalum ili zing'ae. Tulisalimiana na muda kidogo simu yake iliita na alipokea alikuwa ni Chaz Baba  akamwambia anakuja. Wakati huo alikuwa anakunywa pombe aina ya Jack Daniel na Sprite na ameshaanza kulewa," alidai.

Pia alieleza kwa kuwa marehemu Kanumba alikuwa hapendi atoke, alimtaka waende sehemu moja ambapo mara nyingi akilewa huwa  anampiga hivyo hakutaka kumbishia kutoka naye.

Lulu alidai hupendelea kwenda disco wakati marehemu Kanumba alikuwa anapenda kwenda kwenye bendi ambazo alidai kwake  ni za kizee wakati huo aliwaahidi marafiki zake kuwa atarudi.

Alidai baadae marafiki zake walianza kumpigia kumuuliza ulipo ambapo aliogopa kupokea simu mbele ya Kanumba kukwepa kuulizwa  anakwenda wapi, hivyo alimuaga na kumueleza kuwa anakwenda kuchukua maji jikoni na alipofika kwenye korido  Kanumba alimfuatilia kwa nyuma na kumuuliza anaongea na nani.

"Nilijua utani huku nikiwa nacheka nikamjibu kuwa naongea na rafiki yangu kwa sababu nilizoea anapenda kujua naongea na nani  lakini baadae nilianza kuogopa baada ya kuona sura yake imebadilika hivyo nikawa natoka nje naye alianza kunifuata na hii sio mara ya kwanza kunipiga na hufanya hivi akiwa amelewa maana hata mtu alinipigia au kumkumbatia alikuwa hapendi," alieleza na kuongeza;

"Nilikimbia hadi nje wakati huo marehemu alikuwa na taulo hivyo nikadhani kwamba ataona aibu kutoka nje hivyo huku akiwa kifua wazi lakini alinifuata hadi nje umbali wa hatua 28 lakini aliendelea kunikimbiza hadi getini akatoka nje ya geti ambapo kuna barabara ya Sinza Kijiweni na Tandale..tuliendelea kukimbizana hadi nikajificha lakini aliniona na kunipiga vibao na kunifunga mikono yangu kwa mkono wake mmoja."

Muigizaji huyo pia alidai Kanumba alianza kumpiga mateke na kumburuza huku akiwa na taulo lake na kwamba mdogo wake, Seth Bosco alikuwepo lakini hakutoka kumsaidia.

Alidai baada ya kuburuzwa alinyanyuka na alipelekwa moja kwa moja hadi chumbani na mlango ulifungwa kwa funguo kwa ndani na kutupwa kitandani kwa sababu alihisi simu aliyokuwa anaongea naye ni mwanaume mwingine.

Lulu alidai marehemu Kanumba alitoa panga na kwa sababu walikimbia alikuwa anahema sana na kumwambia kuwa atamuua hivyo alianza kumpiga kwa mabapa ya panga kwenye mapaja naye alikuwa akikinga asikatwe usoni.

Vile vile, alidai  Kanumba alikuwa anapumua kwa kasi na kutupa panga chini na kuwa kama mtu anayekabwa baadae alinguka na kujigonga kwenye ukuta muda huo yeye alikuwa kitandani.

"Alipokuwa anataka kuamka nilihisi anataka kunifuata tena nikitoka nikajifungia chooni wakati huo yeye   alianza kutapatapa. Nilijaribu kupiga kelele kupata msaada lakini hakuna, baadaye nilisikia kishindo cha mtu kuanguka au mlango uliobamizwa na kusikia ukimya.

Sikujuwa za kama ameanguka nilihisi hasira zake tu kwani nilipofungua mlango  wa bafuni nilimkuta amelala na wakati huo kulikuwa na mwanga wa mshumaa kwani umeme ulikatika," alidai.

Lulu alidai kwa akili zake aliwaza kuwa Kanumba alijifanyisha kuzimia ili isiwe tatizo kwake ambapo alianza kumwambia kuwa hata mtu akija atamwambia kila kitu kilichotokea lakini akawa hajibiwi.

Alidai alichukua maji chooni na kumgusisha machoni kuona kama ataamka na baadaye alifungua mlango na kumuita Seth na kumueleza kuwa Kanumba ameanguka ambaye naye alijaribu kumuamsha lakini hakuamka na kumpigia simu daktari wake.

Lulu anasimulia kuwa alimwambia Seth hawezi kubaki nyumbani hapo badala yake akitoa naye atatoka kwani akiamka atamuua  hivyo aliondoka na gari hadi Coco Beach.

Aliendelea kudai kuwa alimpigia simu daktari wa familia Paplas  ambaye alikuwa anajua mahusiano yao na wakati akiumwa alikuwa anamtibu na kwamba alimueleza kuwa rafiki yake amempiga sana na iwe mara ya mwisho kumtafuta kwa sababu alimshikia panga na siku nyingine atamuua.

Alieleza kuwa alikuwa haruhusiwi kutoka nyumbani kwao usiku hivyo alikuwa anabeba nguo za ziada na anaporudi nyumbani asubuhi hudanganya kama alitoka kuosha vyombo wakati anatokea klabu.

"Nilipokea simu nyingi kuniuliza kama kweli Kanumba amekufa nilimpigia simu Seth, ambapo alikuwa hapokei nilimpigia Dk Paplas nikamuuliza kuhusu masuala ya nyumbani imekuwaje kwa sababu amepigiwa simu kuuliza naye akamwambia kuwa hajafa ila wapo hospitali na kukata simu. Baadaye Dk Paplas alinipigia kuniuliza niko wapi tukutane," alidai

"Kwa sababu nilijua Kanumba na huyu daktari ni marafiki, nilijua anamtumia rafiki yake waweze kukutana tena  mara ya kwanza nilimkatalia na nikamuuliza kama amezidiwa yupo hospitali gani niende. Nilitaka anihakikishie alipo na asije na Kanumba na wala hakunambia kama ameshakufa," alieleza Lulu.

Alidai walikutana Bamaga na Dk Paplas na ndipo askari walimkamata bila ya kumwambia sababu na walipofika Kituo cha Polisi, Oysterbay Polisi akakutana na watu wengi akiwemo msanii Vincent Kigosi 'Ray' na kuhisi kwamba Kanumba amekamatwa.

Alidai alichukuliwa maelezo na kuonesha sehemu alizojeruhiwa kwa kipigo na askari wa kike ndiye aliyethibitisha na kwamba alichukuliwa maelezo mara nne ambapo alipata taarifa za kifo cha Kanumba akiwa selo.

Siku inayofuata, Lulu alidai alimueleza Afande Ernatus kwamba anaumwa hivyo alipelekwa hospitali ya Mwananyamala akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na kuandikiwa dawa.

"Sijasababisha kifo chake yeye ndiyo alikuwa ananishambulia kwa silaha pengine asingeanguka mimi ndio ningekuwa marehemu kwa sababu sikuwa na njia yoyote ya kujitetea kwa sababu ya umbile langu dogo," alidai Lulu.

Hata hivyo, Jaji Rumanyika alimtaka Lulu kueleza kama wakati huo anaendesha gari alikuwa na leseni, ambapo alidai kuwa hakuwa nayo mpaka baada ya matatizo hayo ndio aliomba leseni.


Kesi hiyo imeahirishwa mpaka leo ambapo upande wa utetezi utakuwa na shahidi mmoja Josephine Mushumbus ambaye wanadai kuwa yupo nje ya nchi.

TFF yatangaza kuziona Yanga, Simba ni sh 10,000

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru kuwa ni sh. 10,000 majukwaa ya mzunguko wakati jukwaa kuu ni sh. 20,000.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana kuwa utaratibu maalum umewekwa kuhakikisha idadi inayotakiwa ya watu 22,000 ndiyo wanaoingia uwanjani.

Alisema  mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, kwa kuwa uwanja mkubwa wa Taifa upo kwenye ukarabati.

Katika hatua nyingine, Lucas alisema Kamati mpya ya Uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) ya TFF itafanya kikao chake cha kwanza mjini Dar es Salaam, Alhamis ya wiki hii na kubwa likiwa ni maandalizi ya mchezo huo.

Alisema  ajenda nyingine katika kikao hicho ni kuteua Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi na Kamati nyingine mbalimbali.


Hiyo ni baada ya uchaguzi wa TPLB uliofanyika Jumapili Oktoba 15 mwaka huu na kupata uongozi mpya chini ya mwenyekiti wake Clement Sanga na makamu wake Shani Mlingo. Wajumbe ni Hamisi Madaki, Ramadhani Mahano, Almasi Kasongo na Edgar Chibura.

Neymar atolewa wakati PSG ikitoka sare

Neymar  akioneshwa kadi nyekundu wakati PSG ilipocheza dhidi ya Olympique de Marseille.

PARIS, Ufaransa

NEYMAR alitolewa nje kabla ya mchezaji mwenzake Edinson Cavani akithibitisha thamani yake kwa mara nyigine tena kwa kufunga bao la kusawazisha katika dakika za mwisho wakati Paris St Germain (PSG) ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya wapinzani wao wakubwa Olympique de Marseille.

Mshambuliaji huyo wa Uruguay alisawazisha dakika moja ndani ya muda wa nyongeza kwa shuti kali la umbali wa kama meta 20 baada ya Neymar kutolewa nje katika dakika ya 87 kwa kadi ya pili ya njano.

Neymar ndiye alikuwa wa kwanza kuipatia timu yake bao la kusawazisha katika dakika ya 33 kufuatia lile la kuongoza la Olympique de Marseille lililofungwa na Luiz Gustavo katika dakika ya 16.

Awali, Marseille walifunga bao la pili katika dakika ya 78 lililowekwa kimiani na Thauvin, ambalo baadae PSG walisawazisha kupitia kwa Cavan na kunusurika kupata kipigo cha kwanza.

Kimsimamo, PSG ina pointi 26 baada ya kucheza mechi 10 ikiwa kileleni pointi nne zaidi ya Monaco iliyopo katika nafasi ya pili.

 

"Ni bao muhimu kwani mchezo ni kama ulikuwa umemalizika, lakini angalau tumeondoka na pointi, “alisema Cavani.


Monaco wako nafasi ya pili, pointi nne nyuma wakiwa na pointi 22 baadaya kuifunga Caen 2-0 Jumamosi.

Real Madrid yaifukuza Barcelona kimya kimya

MADRID, Hispania

MABINGWA watetezi wa La Liga Real Madrid imefanya kweli baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Eibar na kupunguza tofauti ya pointi na vinara Barcelona, huku Karim Benzema akianzia benchi.

Marco Asensio aliing’arisha Real Madrid baada ya kufunga mabao mawili na kuiwezesha timu yake hiyo kuibuka na ushindi huo.

Kwa ushindi huo, Real Madrid sasa imepunguza tofauti ya pointi na Barcelona hadi kufikia tano katika mbio hizo za kusaka ubingwa.

Mshambuliaji huyo alilazimisha bao la kujifunga na kufunga la pili wakati Madrid ikipanda hadi katika nafasi ya pili ikifikisha pointi 20, moja nyuma ya Valencia na moja mbele ya Atletico Madrid, ambayo iliifunga Celta Vigo 1-0 ugenini.

Bao hilo pekee lililoipatia ushindi Atletico Madrid liliwekwa kimiani na Kevin Gameiro.

Barcelona wenyewe waliwafunga Malaga 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wao wa Nou Camp Jumamosi wakati Valencia ilipoisambaratisha Sevilla 4-0.

Paulo Oliveira aliijaza katika wavu wao krosi ya Asensio katika dakika ya 18, kabla mshambuliaji huyo hajawafungia wenyeji bao la pili dakika 10 baadae kufuatia mpira wa Isco.

Mchezaji aliyeingia akitokea benchi Marcelo aliongeza la tatu katika dakika 82.


Zinedine Zidane alifanya mabadiliko matano kutoka katika kikosi chake, ambacho kilitoka sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Tottenham Hotspur katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Jumanne iliyopita.

SuperSport uso kwa uso na TP Mazembe Shirikisho

Kikosi cha mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika,TP Mazembe

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

TIMU ya SuperSport United ilikuwa imekamilika karibu katika kila idara wakati ikifuzu kwa fainali ya Kombe la Shirikisho 2017 baada ya kushinda mabao 3-1 dhidi ya Club African.

Kwa ushindi huo, SuperSport ya Afrika Kusini imetinga fainali kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya mchezo huo wa nusu fainali ya pili uliofanyika kwenye Uwanja wa Stade Olympique Radès Jumapili.

Mchezo wa kwanza wa nusu fainali ulifanyikia kwenye Uwanja wa Lucas Moripe, ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Kwa matokeo hayo, SuperSport itakutana na bingwa mtetezi TP Mazembe, ambayo iliifunga FUS Rabat ya Morocco, katika fainali ya mechi mbili za nyumbani na ugenini mwezi ujao.


Wachezaji wa SuperSports United.

Bradley Grobler aliwafungia wageni, huku Jeremy Brockie naye pia alizifumania nyavu wakati Saber Khalifa aliwafungia wenyeji bao la kufutia machozi.

Al Ahly yaichapa Etoile sasa kucheza fainali Ligi ya Mabingwa wa Afrika 2017 na Wydad Casablanca

CAIRO, Misri

KLABU ya Misri ya Al Ahly (pichani) sasa itakutana na Wydad Casablanca ya Morocco katika fainali ya mwaka huu ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kuichapa Etoile du Sahel ya Tunisia kwa mabao 6-2.

Kwa ushindi huo, Al Ahly imetinga fainali baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 7-4 katika mechi mbili za nusu fainali.

Katika mchezo wa marudio wa nusu fainali uliofanyika jijini Alexandria, Al Ahly ilionekana kuizidi kabisa safu ya ulinzi ya wapinzani wao hao wa Tunisia wakati wakikata tiketi hiyo ya kucheza fainali ikiwa ni mara yao ya 11.

Baada ya Ali Maaloul kufunga bao la kwanza kwa wenyeji dakika mbili baada ya kuanza mchezo huo, Walid Azarou alifunga bao la pili na kuifanya Etoile kutoka kabisa nje ya mchezo.

Bao la kujifunga lililofungwa na Rami Rabiaa liliipeleka Al Ahly katika fainali ya kwanza tangu mwaka 2013, huku Etoile ikijibu kupitia kwa Rami El Bedwi na Ihab Msakni kwa maba waliyofunga baadae.

 

Miaka minne iliyopita, Al Ahly iliifunga timu ya Afrika Kusini ya Orlando Pirates katika fainali wakati walipofanikiwa kutetea taji lao waliloshinda miezi 12 iliyotangulia.

Mchezo huo wa Jumapili ulipigwa mbele ya karibu mashabiki 40,000 jijini Alexandria, ambao walisaidia kuiongezea nguvu Al Ahly baada ya mechi nyingi za Misri kuchezwa bila ya mashabiki kutokana na sababu za kiusalama.

Kikosi cha kocha Hossam El Badry sasa kitakutana na Wydad katika mechi mbili za fainali, baada ya Wamorocco hao kuwafunga USM Alger ya Algeria kwa mabao 3-1 katia mchezo uliofanyika Jumamosi.

Wakati huohuo, Ahly sasa wanaweza kuongeza rekodi yao ya kutwaa taji hilo mara nane na hadi kufikia mara tisa endapo watafanikiwa kuifunga Wydad.

Mchezo wa kwanza wa fainali utafanyika wikiendi ijayo huku ule wa marudiano unatarajia kufanyika Novemba 3-5.


Timu yoyote itakayoshinda italiwakilisha bara la Afrika katika mashindano ya Fifa ya Kombe la Dunia kwa klabu yatakayofanyika Japan Desemba.

Mkurugenzi TAA ataka Tughe kutetea wafanyakazi

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (katikati mstari wa mbele), akinyanyua mikono juu kuashiria mshikamano daima na baadhi ya viongozi wa matawi wa chama cha wafanyakazi mahala pa kazi (TUGHE) matawi ya Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipokutana nao.

Na Mwandishi Wetu

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewataka viongozi wa Chama cha Wafanyakazi kusikiliza malalamiko

ya wafanyakazi bila kubagua.

 

Bw.Mayongela alisema viongozi wa Wafanyakazi kupitia matawi mawili ya Chama cha Wafanyakazi, TAA Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kutenda haki kwa kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi wote na kuyawasilisha kwa wasilisha kwa mwajiri ili yafanyiwe kazi.

Alitoa kauli hiyo juzi wakati viongozi wa matawi hayo walipokwenda kujitambulisha ofisi kwake TAA Makao Makuu, ambapo alisisitiza kuwa wafanyakazi wa chini ndio wenye matatizo makubwa, lakini hawasikilizwi na kutatuliwa matatizo yao kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (katikati mstari wa mbele), akinyanyua mikono juu kuashiria mshikamano daima na baadhi ya viongozi wa matawi wa chama cha wafanyakazi mahala pa kazi (TUGHE) matawi ya Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipokutana nao jana.

“Ninashukuru uongozi mmekuja kuonana nami, ninahitaji ushirikiano wenu kama Chama cha Wafanyakazi, muwatumikie wafanyakazi kwa kutenda haki mkisikiliza matatizo ya kila mmoja na kufikisha sehemu husika na ninawaahidi kuwa nanyi bega kwa bega kutatua matatizo ya wafanyakazi kwani wao ndio wanafanya TAA iwepo, “alisema Mayongela.

Alisema wafanyakazi endapo wakifanya kazi bila manung’uniko wala makundi, mamlaka itasonga mbele kwa kuwa na uongozi sio kupigana vita bali unatakiwa kujijenga na kuwa kitu kimoja.

Hatahivyo alisema kwa sasa yupo mbioni kuangalia namna ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi  kwa kupitia makusanyo yatakayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi ili kuongeza ari kwa wafanyakazi.

Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi mahala pa Kazi (TUGHE) matawi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Makao Makuu (TAA HQ) na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bw. Richard Mayongela (kushoto) alipokutana nao.

Aliendelea kusema kuwa inaonekana wafanyakazi wengi wa TAA wamekata tamaa kutokana na kufanya kazi nyingi na wakati mwingine kupitiliza muda wa kazi wa kawaida bila kupata stahiki yeyote.

“Kwa msaada wa Mungu nina imani atanionyesha wapi fedha zilipo na jinsi ya kuzitumia ipasavyo kwa masuala ya msingi, na ninakusudia hadi kufika Desemba mwaka huu niweze kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Watu wanafanya kazi sana lakini maslahi ni madogo, unaona kabisa jinsi mtu anavyoitumikia taasisi kwa moyo, lakini sura inaonesha jinsi alivyokata tamaa, ninaamini kwa kufanya hivi itaongeza tija na bidii ya kazi.” Alisema Bw. Mayongela.

Halikadhalika, Bw. Mayongela amesema atahakikisha wafanyakazi wanapata vitendea kazi vya uhakika kulingana na kazi zao, zikiwemo bajaji, pikipiki na magari kwa ajili ya doria na shughuli za uendeshaji ndani ya Viwanja vya Ndege.

Pia amewataka viongozi hao kuwa karibu na wafanyakazi ili kuhakikisha wanawahamasisha wanafanya kazi kwa bidii, uaminifu na uadilifu ili kuondoa mianya na tabia za upokeaji wa rushwa, kwa kuwa TUGHE ni daraja kati ya mwajiri na wafanyakazi.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE tawi la TAA Makao Makuu, Bw. Nasib Elias mbali na kumshukuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwa kuwapa fursa ya kukutana naye, lakini alimuomba kuendelea kudumisha mahusiano baina ya mwajiri na Tughe.

Pia alimuomba aitake menejimenti yake kuwa na utaratibu wa kuweka milango wazi kwa wafanyakazi kama yeye ili waweze kusikiliza na kutoa majibu sahihi kwa baadhi ya masuala ya kiofisi yanayowasilishwa na wafanyakazi kwao na sio kila jambo liwasilishwe kwake.

“Tunakuombea kwa Mungu akutie nguvu kwa haya unayotaka kufanya likiwemo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuwa litasaidia kuamsha morali ya kazi kwa wafanyakazi, lakini hii sera yako ya kuwacha milango wazi, tunaomba nayo itekelezwe katika ngazi ya menejimenti yako kwani kuna mambo ambayo yanaweza kumalizwa na Wakurugenzi na Mameneja wenyewe na sio lazima yafike kwako, “ alisema Bw. Elias.


Katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi ambacho kimeonekana ni kipaumbele cha Kaimu Mkurugenzi mkuu kwa wafanyakazi, Bw. Elias amemuomba kuangalia namna bora ya kusimamia maslahi hayo ikiwemo kuuasili mkataba wa hali bora (SBA) kama inavyotekelezwa na taasisi nyingine za serikali.