Monday, 9 April 2018

Mlandege Yapokea Kichapo Zanzibar


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
LIGI Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja iliendelea juzi kwa kupigwa michezo mitatu na miwili ikishindwa kuchezwa baada ya viwanja vilivyopangwa kuchezewa kujaa maji.

Michezo iliyochezwa ni ile ya Mlandege iliyocheza na White Bird katika Uwanja wa Amani , Kimbunga na Strongfire ambao ulichezwa Uwanja wa Tazari na Polisi Bridge ilicheza na Idumu  Mchangani.

Mlandege katika mchezo wake alifungwa mabao 2-1 wakati Kimbunga iliifunga Strong Fire mabao 4-2, huku Polisi Bridge in Idumu wakatoka sare ya kutokufungana.

Katika mchezo huo, White Bird iliyokuwa ugenini  ikajipatia ushindi huo kupitia kwa wafungaji wake Mussa Khamis na Januari Yona.

Mlandege ambayo licha ya kufungwa bado inaendelea kuongoza ikiwa na pointi 60, bao lake yalifungwa na Omar Makame.

Michezo ambayo haikuchezwa ni ile iliyopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Mwanakombo, ambako kulikuwa na mchezo kati ya Mahonda Kids na Ngome na Miembeni  na Mundu kwenye Uwanja wa Chukwani.

Kocha Lwandamila Awaonya Wachezaji Yanga


Na Mwandishi Wetu
LICHA ya ushindi mnono ulioiweka katika nafasi nzuri ya kukaribia kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa Yanga George Lwandamina, amewataka wachezaji wake kutowadharau wapinzani wao Welayta Dicha.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo kujiweka mguu moja mbele katika harakati za kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu Afrika.

Akizungumza na gazeti hili Lwandamina alisema Welayta Dicha na timu nzuri na wanapaswa kujiandaa kikamilifu ili kuweza kuwadhibi wakiwa kwao vinginevyo wanawezakujikuta katika wakati mgumu na ikiwezekaa kupoteza nafasi ya kucheza hatua ya makundi.

“Mbali na mbinu za kucheza ugenini, ambazo nimeanza kuwafundisha vijana wangu lakini kitu kingine cha muhimu nimekuwa nikiwakumbusha kwamba bado tuna kibarua kizito na ushindi tulioupata hapa nyumbani unapaswa tuulinde kwa kucheza kwa kushambulia ili tupate mabao mengine,” alisema Lwandamina.

Kocha huyo raia wa Zambia alisema kitu cha msingi ameamua kuanza nacho katika marekebisho yake kabla ya mchezo huo ni safu yake ya ulinzi, ambayo ilifanya makosa mengi ikifuatiwa na ile ya ushambuliaji ambayo nayo ilipoteza nafasi nyingi walizotengeneza.

Alisema kama wangeweza kuzitumia vizuri nafasi zote walizozipata kazi yao katika mchezo wa marudiano ingekuwa nyepesi lakini mabao mawili bado hayampi uhakika wa kusonga mbele kutokana na ubora wa wapinzani wao ambao watakuwa nyumbani Addis Ababa.

Yanga inatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa wiki hii kuelekea Ethiopia ambapo ndiko utakapofanyika mpambano huo na endapo watafanikiwa kusonga mbrele watacheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kama ilivyokua mwaka 2016 chini ya kocha Hans van der Pluijm.

Tanzania Yazidi Kupoteza Matumaini Madola

Failuna Abdi (kulia) aliyeshindwa kupata medali katika mbio za meta 10,000 katika Michezo ya Madola. Kushoto ni Jackline Sakilu.

Na Mwandishi Wetu
MATUMAINI ya Tanzania ya kupata medali katika Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola inayoendelea Gold Coast, Australia, yanazidi kufifia baada ya mwanariadha mwingine, Failuna Abdul kumaliza katika nafasi ya 12 katika mbio za meta 10,000.

Tayari mwanariadha mwingine wa Tamzania, Ali Rashid Gulam kumaliza wan ne katika kundi lake la mchujo na kushindwa kufuzu hatua inayofuata katika mbio za meta 100 zilizofanyika juzi mjini humo.

Failuna alimaliza mbio hizo za meta 10,000 kwa kutumia dakika 32:22.01 ikiwa ni sekunde 37 nyuma ya mshindi wa kwanza Stella Chegan wa Uganda aliyemaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 31:45.03 akifuatiwa na Mkenya, Stacy Ndiwa aliyemaliza kwa muda wa 31:46.04.

Mshindi watatu aliyepata medali ya shaba ni Mercline Chelangat wa Uganda aliyetumia dakika 31:48.04.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema jana kuwa, Failuna amejitahidi sana kwa kupishana na mshindi wa kwanza kwa sekunde 37 tu, ambapo alisisitiza kuwa mbio hizo zilikuwa za ushindani mkubwa.

Gidabuday amesema kuwa wanasubiri mbio za meta 5,000 ambazo atashiriki tena Failuna huku tegemeo lao kubwa liibaki kwa Said Makula na Sarah Ramadhani ambaowatashiriki marathon pamoja na Stephano Huche siku ya mwisho ya michezo hiyo, Aprili 15.

Wanafunzi Wawili Watanzania Wang'ara Mbio za Kusaka Tuzo za Kimataifa za DStv Eutelsat Star

Na Mwandishi Wetu
Tanzania imepata wawakilishi wawili watakaoshiriki katika msimu wa saba wa tuzo maarufu barani Afrika kwa wanafunzi wapenzi wa masomo ya Sayansi na Teknolojia ijulikanayo kama - DStv Eutelsat Star Awards. 

Wanafunzi hao Michael Ditrick wa shule ya Sekonday Ilboru – Arusha na Taher Rasheed wa Al-Madrasat Ussaifiyatul Burhaniyah ya jijini Dar es Salaam
 Michael ameshika nafasi ya kwanza katika uandishi wa insha maalum na Taher kwa mchoro maalum kuhusiana na sayansi ya Setelait ambapo wanafunzi zaidi ya 150 kutoka shule mbalimbali nchini walishiriki katika mashindano hayo ya mwaka huu. Washindi hao walipatikana kutakana na utahini uliofanywa na jopo la majaji sita.
 Kazi za washindi hao zimewasilishwa MultiChoice Africa ambapo zitapambanishwa na kazi kama hizo kutoka kwa washindi wa nchi nyingine kote barani Afrika na hatimaye kupatikana mshindi wa jumla katika kila kipengele yaani wale walioandika insha na wale walioandaa mchoro.
 Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Maharage Chande, amesema tuzo za mwaka huu zimekuwa na ushindani mkubwa ambapo shule kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Dodoma, Pwani zimeshiriki. 

“Kuongezeka wa idadi ya wanafunzi wanaoshiriki katika tuzo hizi ni ishara njema na tunaamini kwa viwango walivyoonyesha, bila shaka mwaka huu tutapata ushindi mkubwa kuliko hata ule wa mwaka jana” alisema Maharage.
 Amesema tuzo hizi zinalenga kuwajengea vijana wetu ari ya kushiriki katika masomo ya sayansi na pia kuhamasisha ubunifu na ugunduzi katika tasnia ya sayansi. 
Amewataka walimu kuwahimiza wanafunzi wao kushiriki katika tuzo kama hizi za kimataifa kwani ni kipimo kizuri kwa wanafunzi wetu na pia inajenga kujiamini kwa wanafunzi wetu.
 Tuzo hizi ambazo zinahusisha uandishi wa insha maalum au kuandaa bango vyenye ujumbe kuhusiana na elimu ya anga hususan Setelait ni za wazi kwa wanafunzi wote wa shule za sekondari wenye umri kati ya miaka 14 – 19.
 Mwaka huu, washindani walitakiwa kuandika insha au kubuni bango kuhusu manufaa yaliyoletwa na uvumbuzi wa setelaiti katika maisha ya kila siku hapa ulimwenguni na ni jinsi gani setelait imekuwa kama kiungo muhimu kwa shughuli zote zinazofanyika kote duniani.
 Kama kawaida tuzo hizi zina zawadi kabambe ambapo mshindi wa Insha atapata fursa ya kuzuru kituo cha Eutelsat nchini Ufaransa na pia kwenda Guiana kushuhudia mubashara urushwaji wa setelait angani.
 Mshindi wa bango atajishindia safari ya kwenda nchini Afrika Kusini na kutembelea kituo cha anga cha nchi hiyo na pia makao makuu ya MultiChoice Africa akiwa kama mgeni maalum.  Shule zitakazotoa washindi hao zitapata zawadi ya kufungia huduma ya DStv bure.

 Wanafunzi wengine waliofanya vizuri katika mchakato huo ni pamoja na Pio Mwita wa UWATA Sekondari ya Mbeya ambaye ameshika nafasi ya pili kwenye insha na Peter Kiama wa Feza Boys ya Dar es Salaam aliyeshika nafasi ya pili kwa upande wa bango.

Mwaka jana Tanzania iliibuka mshindi wa pili kwenye insha baada ya Davids Bwana wa FEZA Boys kunyakua nafasi hiyo nyuma ya mwanafunzi Leoul Mesfin kutoka Ethiopia.

Simba Yaendelea Kukaribia Ubingwa Ligi Kuu Bara

Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kunga bao wakati Simba ilipocheza dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jahmuri mjini Morogoro leo.
Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba wamezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, baada ya jana kuifunga Mtibwa Sugar kwa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

Kwa ushindi huo, Simba sasa imefikisha pointi 52 baada ya kushuka dimbani mara 22 ikimuacha mtani wake Yanga akiendelea kuwa katika nafasi ya pili kwa pointi 46, lakini akiwa na mchezo mkononi.

Yanga wenyewe wanacheza kesho dhidi ya Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba waliiuanza mchezo huo kwa kufanya mashmbulizi ya mara kwa mara ndani ya dakika 15 za mchezo huo kupitia washambuliaji wake Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na John Bocco na kuleta msukosuko, langoni mwa Mtibwa Sugar .

Katika mchezo huo, ``Simba iliandika bao la kuongoza katika dakika ya 23 lililofungwa na Emmanuel Okwi kufuatia krosi ya Kichuya aliyepiga krosi iliyomkura John Bocco aliyetoa pasi ya kichwa kwa Okwi aliyeukwamisha mpira kirahisi wavuni.

Dakika ya 37 Mtibwa walipata kona mbili mfululizo, lakini zote hazikuzaa matunda na hizo zilitokana na timu hiyo kufanya mashambulizi ya nguvu langoni mwa wapinzani wao.

Hata hivyo vijana wa Simba waliimarika zaidi kipindi cha kwanza, licha ya mvua kunyesha katika kipindi hicho,  ambapo Bocco na Okwi walikuwa wakibadilisha nafasi kucheza kipindi hicho cha kwanza.

Azam FC ambao walicheza juzi na kutoka suluhu Mbeya City na hivyo kendelea kuchechemea katika nafasi ya tatu akiwa na pointi 45 lakin akiwa amecheza mchezo mmoja zaidi.

Simba mchezo unaofuata itacheza dhidi ya Mbeya City mwishoni mwa wiki katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Nyota Kibao Kushiriki Ngorongoro Race 2018

Mbio za Ngorongoro Race kabla ya kuanza mwaka jana.

Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA nyota wamethibitisha kushiriki mbio za mwaka huu za Ngorongoro Race zitakazofanyika Aprili 21,  imeelezwa.

Mkurugenzi wa mbio hizo, ambazo zinafanyika kwa mwaka wa 11 sasa, Meta Petro alisema jana kwa njia ya simu kuwa, tayari wanariadha wengi nyota wamethibitisha kushiriki mbio hizo.
Wanariadha wakichuana katika mbio za mwaka jana mjini Karatu.
Baadhi ya wanariadha nyota waliothibitisha kushiriki ni pamoja na Fabian Joseph, Said Makula, Fabian mdogo, Dickson Marwa, Sarah Ramadhani, Jaquline Sakilu, Stephano Huche, Failuna Abdi na wengine.

Makula, Sarah na Huche wamo katika timu ya Tanzania iinayoshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola iliyoanza Gold Coast, Australia kuanzia Aprili 4 hadi 15.
Ofisi ya Ngorongoro Race iliyopo Karatu mkoani Arusha.
Petro alisema kuwa tayari zaidi ya wanariadha 200 wamejiandikisha kutaka kushiriki mbio hizo, ambazo zimekuwa zikifanyika katika kipindi cha masika na kuanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro na kumalizikia katika viwanja vya Mazingira Bora mjini Karatu.
Mkurugenzi wa Ngorongoro Race, Meta Petro akimvisha medali Mkurugenzi wa Ufundi wa mbio hizo, Filbert Bayi kama shukrani kwa kazi nzuri ya kuandaa mbio hizo mwaka jana katika Uwanja wa Mazigira Bora.
Mshindi wa kwanza wa mbio za kilometa 21 ataondoka na Sh milioni 1 wakati mshindi wa pili atapata Sh 500,000 wakati watatu atapewa Sh 250,000 huku kukiwa pia na mbio za kilometa tano na 2.5 kwa watoto.
Mwanariadha wazamani wa Tanzania, Mzee John Stephen Akhwari akizungumza na Mkurugenzi wa Ngorongoro Race, Meta Petro baada ya mbio za mwaka jana kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu mkoani Arusha.

Sunday, 8 April 2018

Mabondia Wote wa Tanzania Wadundwa Madola

Mabondia wa timu ya Tanzania walioshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola wakiwa na kocha wao, Moses Oyombi  (katikati mbele) wakati wa mazoezi Kibaha, Pwani kabla ya kwenda Gold Coast kwa michezo hiyo, Mabondia wote wamepigwana kutolewa.

Na Mwandishi Wetu
MABONDIA wa Tanzania wote wametolewa katika Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola inayoendelea Gold Coast, Australia baada ya kudundwa.

Ezra Mwanjwango naKassim Mbundwike walipoteza mapambano yao katika uzito wa bantamweight na welterweight katika ukumbi wa Oxenford.  Mabondia hao walikuwa wakicheza katika hatua ya 16 bora ili kufuzu kwa robo fainali.

Mwanjwango alipoteza pambano lake hilo lilichezeshwa na mwamuzi wa Italia Maria Rizzardo kwa majaji 5-0 dhidi ya bondia Mzambia Everisto Mulengain.

Kama hilo halitoshi, bondia mwingine wa Tanzania, Mbundwike alipoteza pambano lake dhidi ya Manoj Kumar wa India kwa pointi 5-0 na kuhitimisha mbio za Tanzania kusaka medali kwa upande wa mchezo huo.

Ijumaa mabondia wengine wa Tanzania, nahodha wa timu ya ndondi, Selemani Kidunda na Haruna Mhando walipoteza mapambano yao.
Timu ya taifa ya ndondi siku ya kuagwa kwa timu ya Tanzania iliyoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Bondia aliyekuwa wa kwanza kupoteza pambano lake ni Mhando aliyepoteza kwa bondia wa India, Naman Tanwar katika uzito wa juu wakati Kidunda alichapwa na kwa pointi 2-3 dhidi ya Mkenya Edwin Owuor katika pambano la middle.

Sasa Tanzania matumaini yake katika medali ni katika mchezo wa riadha, kuogelea nampira wa meza.

Mwanariadha wa Tanzania Ali Khamis Gulam leo asubuhi alikimbia katika mbio za meta 100 na kumaliza katika nafasi ya nne katika kundi lake la mchujo, na hivyo naye ameungana na mabondia wa Tanzania kuiaga michezo hiyo, lakini amebakiwa na mchezo wa mbio za meta 200.

Muda bora wa Gulam ni sekunde 10:72, ambao ni wa chini ukilinganisha na rekodi ya michezo hiyo wa sekunde 9.58 unaoshiiliwa na Mjamaica Usain Bolt, ambaye sasa amestaafu mbio.

Rekodi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa mchezo huo ni sekunde 9.88 uliowekwa na Ato Boldon huko Kuala Lumpur, Malaysia mwaka 1998.

Wachezaji wa mpira wa meza wataanza kampeni zao Jumanne, wakianza na wanawake na wanaume kwa mchezo wa mchezaji mmoja mmoja.

Saturday, 7 April 2018

Ngorongoro Marathon; Mbio za Kukimbiza Jangili


Na Mwandishi Wetu
MBIO za Ngorongoro Marahon zenye lengo la Kukimbiza Jangili, ambazo mwaka huu zitafanyika Aprili 21 zimefikia katika hatua nzuri.

Kauli Mbiu yam bio hizo mwaka huu ni `Kukimbiza Jangili’, ambapo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA) ndio mdhamini mkuu ikisaidia na Bonite Bottlers ya mjini Moshi, ambayo hutengeneza maji ya Kilimanjaro na soda jamii ya Coca Cola.

Tayari wanariadha zaidi ya 200 wamejisajili kwa ajili ya kushiriki mbio hizo, ambazo waandaaji wanasema kuwa mwaka huu zitakuwa na msisimko mkubwa katika maeneo tofauti tofauti.

WAANDAAJI WANENA
Mkurugenzi wa mbio hizo, Meta Petro akizungumza na gazeti hili anasema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na ni matarajio yao makubwa kuwa mwaka huu msisimko utakuwa mkubwa zaidi tofauti na mwaka jana.

Alisema kuwa ni mataraji yao kuwa mwaka hadi mwaka mashindano hayo yatakuwa yakibadilika na kushirikisha washiriki kibao kutoka ndani na nje ya nchi.

Petro ambaye ni mwanariadha wazamani wa kimataifa wa Tanzania, anasema kuwa wakimbiaji nyota karibu wote nchini wamethibitisha kushiriki mbio hizo, ambazo huanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

Anasema kuwa hivi karibuni watamtangaza mgeni rasmi wa mbio hizo, ambazo mbali na kupiga vita ujangili wa wanyama pori, pia zinatumika kuinua vipaji vya wanariadha nchini wa rika tofauti tofauti.

KUONGEZWA ZAWADI
Anasema kuwa ili kuongeza msisimko na ushindano wa mbio hizo wameandaa zawadi, ambapo sasa washindi wengi watazawadi tofauti na huko nyuma, ambapo watu wachache wa kwanza ndio walizawadiwa.

Alisema kuwa baada ya kutafakari sasa washindi wengi wa mbio za kilometa 21 watapata zawadi ili kuongeza ushindani na kuvuta washiriki wengi.

Mshindi wa kwanza ataondoka na kitita cha Sh milioni 1 huku wa pili Sh 500,000 wakati yule watatu atapata Sh 250,000, ambapo zawadi zitatolewa hadi kwa mwanariadha wa 10 bora.

Huku kwa watoto wadogo, ambao watashiriki mbio za kilometa 2.5 zawadi zitatolewa hadi tano bora wakati huko nyuma walikuwa wakipata zawadi washindi watatu tu wa kwanza.

Kingine kikubwa katika mbio nyingi washindi wa kilometa tano hawapati zawadi, lakini Ngorongoro Marathon hutoa kifuta jasho kwa washindi wa mbio hizo, ambazo huitwa za kujifurahisha.

ADA ZA USHIRIKI
Kwa washiriki wakilometa 21 kila mshiriki atatakiwa kulipia Sh 10,000 kwa Raia wa Watanzania wakati raia wakigeni akila mmoja atalipa mkiasi cha dola za Marekani 50 wakati watoto watakimbia bure.

Wale watakaoshiriki mbio za kilometa tano watalipia kiasi cha Sh 10,000 kwa watanzania wakati wagemi watalipa dola 10 na timu, yaani kampuni kama itapeleka wafanyakazi wake kushiriki, basi itatakiwa kulipia dola za Marekani 500.

MBIO ZA MWAKA HUU
Wanyama kama tembo, kifaru wamekuwa wakiuawa na majangili kwa ajili ya meno yao wakati twiga na pundamilia wanauawa kwa ajili ya nyama zao huku simba na chui wanapata majanga kutokana na ngozi zao, hivyo mbio za mwaka huu zinaendeleza kampeni ya kupiga vita ujangili huo.

Waandaaji wameamua kupambana na ujangili huo ili kuwaepusha wanayama hao na janga la kuawa kwani wakimalizika, taifa litakosa fedha za kigeni kupitia katika utalii wa kuangalia wanyama.

Mbio hizo zilianza tangu mwaka 2008 na lengo likiwa ni kupiga vita tatizo la taifa na dunia la kuuawa ovyo wanyama kwa ajili ya pembe na ngozi zao.

Huko nyuma lengo lilikuwa kupiga vita malaria katika eneo la Karatu na vitongioji vyakle pamoja na gonjwa hatari la ukimwi, lakini baada ya kupungua kwa tatizo hilo, 

Wamekua wakipiga vita ujangili, ambao umekithiri katika mbuga zetu hapa nchini.
Mbio hizo mwaka huu zinatimiza miaka 11 tangu kuanzishwa kwake na zimekuwa zikiandalia kwa umakini mkubwa chini ya Petro pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi, Filbert Bayi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Friday, 6 April 2018

TFF Yatupa Tena Rufaa ya Michael Wambura


Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Rufaa ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetupa rufaa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura kufungiwa maisha kujihusisha na shughuli za soka.

Akisoma hukumu hiyo jana Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Ebenezer Mshana alisema kamati yake ilipitia hukumu tatu, ambazo zilikatwa kwa kamati hiyo dhidi ya TFF.

Mshana alisema baada ya kupitia hukumu zote tatu na hoja za rufaa, rufaa moja ya Edgar Chibula ilishinda na rufaa mbili ambazo ni ya Wambura na Dustan Mkundi, kamati imejiridhisha na maamuzi ya awali yaliyotolewa na Kamati ya Maadili kuwafungia maisha.

“Upande wa utetezi wa Wambura ambao ulikuwa na mawakili watatu ukiongozwa na Masumbuko Lamwai, ulileta mbele ya kamati hoja nne za kupinga mteja wao kufungiwa maisha kujihusisha na soka na upande wa TFF uliwakilishwa na wanasheria wawili ikiongozwa na Allan Kiluvya,” alisema Mshana.

“Katika barua yake ya Desemba 4, 2016 Kamati ya Maadili ya Rufaa imejiridhisha kuwa Wambura alipewa nafasi ya kujieleza kwani alitakiwa kufanya na Kamati ya Ukaguzi na ushahidi wa video uliwasilishwa mbele ya kamati hiyo,” alisema Mshana.

Katika hoja za rufaa kamati ilisikiliza pande zote mbili za rufaa na upande uliokatiwa rufaa ambao ni TFF baada ya kusikiliza pande zote mbili kamati ilijiridhisha na maamuzi ya kamati ya maadili.

Kamati ya TFF ilimfungia kujihulisisha na soka maisha Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura  baada ya kumkuta na hatia katika tuhuma tatu zilizokuwa zinamkabili kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013 kama zilivyofikishwa kwenye kamati na sekretarieti ya TFF.

Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF kwa makosa ya kupokea/kuchukua fedha za TFF kwa malipo yasiyo halali na kughushi barua ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”

Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015).

Kamati ya Rufaa ya Maadili imeiagiza TFF kulifikisha suala la Wambura na Danstun Mkundi kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zingine za kisheria na imebariki kifungo cha maisha cha kutojihusisha na soka maisha.

Kwa upande wa wakili wa Wambura, Muga alisema mteja wake hajaridhishwa na hukumu hiyo, hivyo atakata rufaa katika ngazi nyingine.

Wababe wa Yanga Wakiona Chamtema Kuni


Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Singida United ambao Jumapili iliyopita iliifunga Yanga kwa penalti 4-2 na kuitoa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam, jana walikiona cha moto baada ya kufungwa 3-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar imefikisha pointi 30 na kuendelea kuwa katika nafasi ya sita huku wanyonge Singida wawakibajki katika nafasi ya tano na pointi zao  35.

Kelvin Sabato ndiye aliyekuwa wa kwanza kuifungia bao Mtibwa katika katika dakika ya 22 katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Bao la pili la Mtibwa Sugar lilifungwa na  Kihimbwa katika dakika ya 53 wakati la tatu, liliwekwa kimiani na Hassan Dilunga kwa penalti katika dakika ya 71 baada ya mchezaji mmoja wa Mtibwa kuchezewa vibaya katika eneo la hatari.

Man United Yashikilia Ubingwa wa Man City EPL


MANCHESTER, England
MANCHESTER City inaweza kupunguza maumivu ya kufungwa na Liverpool katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya England kesho wakati itakapocheza dhidi ya majirani zao wa Manchester United.

Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Etihad, ambako ni nyumbani kwa Man City, utaanza kuanzia saa 1:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Man City Jumatano ilipokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Liverpool katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield na hivyo ushindi wa leo utaipa faraja kubwa timu hiyo inayofundishwa na kocha Mhispania, Pep Guardiola.

Endapo Man City itashinda leo itakuwa imefikisha jumla ya pointi 87, ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote ikiwemo Manchester United iliyopo katika nafasi ya pili yenye pointi 68, ambapo ikishinda mechi zote zilizobaki itafikisha pointi 86 tu, ambazo zitakuwa tayari zimepitwa na City.

Vijana wa Guardiola watakuwa timu ya kwanza katika historia ya miaka 26 ya Ligi Kuu ikitwaa ubingwa huku ikiwa imebakisha mechi sita mkononi, endapo leo itaibuka na ushindi katika mchezo huo.

Man City ina pointi 16 mbele ya Jose Mourinho, ambaye timu yake iko katika nafasi ya pili, na endapo watashinda leo litakuwa taji la kwanza kwa kocha Guardiola tangu aanze kufundisha soka England.

Vinara  hao wa Ligi Kuu wamekatishwa tamaa na kipigo cha 3-0 kutoka kwa Liverpool katika mchezo huo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwenye Uwanja wa Anfield.

Mpambano huo unakuja ikiwa ni siku tatu kabla ya kupigwa kwa mchezo wa marudiano wa Ulaya na Guardiola anakabiliwa na kibarua cha kubadili matokeo watakaporudiana kwenye Uwanja wa Etihad.

Wednesday, 4 April 2018

Barcelona, AS Roma Kuonekana Ndani ya DStv

Na Mwandishi Wetu 
Michuano ya UEFA champions League hatua ya robo fainali raundi ya pili inaendelea leo siku,

Jana usiku tulishuhudia hatua ya kwanza ya robo fainali, ambapo Juventus walipigwa 3-0 na Real Madrid hivyo Madrid kuwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele wakisubiri mchezo wa marudiano utakaofanyika wiki ijayo.

Katika mchezo mwingine jana usiku, mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sevilla ya Hispania.

REal Madrid na Bayern Munich wako katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya nusu fainali.


Leo usiku michuano inaendelea, ambapo Barcelona inaikaribisha AS Roma, Barcelona ina rekodi nzuri kwenye michuano  hii ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Timu hiyo ya Hispania imeshiriki mashindano hayo mara 11 tangu na kutwaa mataji mara kadhaa.

Timu hiyo imecheza robo fainali ya Ulaya mara nne, nusu fainali mara nne huku ikicheza fainali idadikama hiyo na kutwaa ubingwa mara mbili.
Leo Jioni wanashuka Dimbani kwa mara nyingine tena wakicheza dhidi ya Roma. Je unaitabiria nini Barcelona kwenye mechi hii dhidi ya Roma?

Usikubali kukosa Uhondo huu Soka utakaorushwa Mubashara na DStv pekee, saa 3 usiku kwenye Supersport 10 kupitia kifurushi chake cha DStv Bomba kinachopatikana kwa Sh. 19,000 pekee!

Jiunge na DStv sasa kwa Sh. 79,000 tu, wasiliana nao kwa 0659 07 07 07, kujihudumia bonyeza *150*46#


Social media:

Leo usiku tunaendelea na michuano ya #UEFA Champions League hatua ya robo fainali,ambapo Barcelona inaikaribisha Roma.

Inakua ni rekodi nzuri ya 11 kwa Barcelona ndani ya #UEFA  tangu 2007, Hii ikiwa ni kufika katika robo fainali mara 4 nusu Fainali mara 4 pamoja na  Ushindi mara 2,Je unaitabiria nini Barcelona katika Mchezo wao wa leo dhidi ya Roma?

Je, Utabiri wako ukoje?  Usikubali kukosa Uhondo huu wa Soka kwenye @DStvTanzania pekee! Mechi hii itaruka LIVE kupitia  SS10 saa 3 usiku kwenye  kifurushi cha DStv Bomba kwa sh.19,000 tu!

Monday, 2 April 2018

Bayi Apewa Tuzo Iliyotukuka Michezo ya Madola

Rais wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF), Louise Martin (kushoto) akimkabidhi mwanariadha wazamani wa Tanzania, Filbert Bayi tuzo iliyotuka katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Sheraton Grand Mirage mjini Gold Coast, Australia.

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF) limempatia tuzo ya Utumishi Uliotukuka gwiji wa riadha wa Tanzania, Filbert Bayi kutokana na mchango wake katika mchezo huo.

Bayi, alitwaa medali ya dhahabu, ambapo mbali na kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za meta 1500 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola Chrischurch, New Zealand mwaka 1974, aliweka pia rekodi mpya ya Jumuiya ya Madola, ambayo amedumu nayo hadi sasa, ikiwa ni miaka 44.

Kwa upande wa rekodi ya dunia ya mbio hizo, Bayi ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), alidumu nayo kwa takribani miaka mitano, kabla haijavunjwa na  Sebastian Coe, ambaye kwa sasa ni Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha, IAAF.
Tuzo hiyo, Bayi alikabidhiwa na Rais wa CGF, Louise Martin katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Sheraton Grand Mirage mjini Gold Coast, Australia wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CGF, Ben Nichols, Bayi alipewa tuzo hiyo pamoja na viongozi wengine wa mashirikisho ya michezo kutoka nchi mbalimbali duniani.

Bayi aliliambia Habari Leo jana kwa njia ya simu kuwa, pamoja na jambo la kushtua, lakini kwake jambo muhimu na kubwa ni kutambuliwa kwa juhudi zake.
Alisema jambo jema kama hilo daima ni furaha kubwa na linamkubusha mazuri, ambayo ameyafanya wakati wake akiwa mwanariadha wa kitaifa na kimataifa.

“Mafanikio daima hayaji kirahisi, juhudi binafsi, nidhamu kujituma ni muhimu sana na tuzo hiyo ni kwa ajili ya familia yangu, wanamichezo pamoja na mashabiki wangu, “alisema Bayi.

Akitoa rai, Bayi aliwaomba Watanzania kuwa na utamaduni na kutambua wanamichezo walioliletea taifa heshima katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika michezo pamoja na utendaji mzuri wa kazi.
Alisema kuwa hatua hiyo itahamasisha wanamichezo wadogo na watendaji katika vyama na mashirikisho ya michezo.

Singida United Yaiondoa Yanga Kombe la Shirikisho


Na Mwandishi Wetu
PASAKA imekuwa chungu kwa Yanga baada ya kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Singida United kwa kuchapwa mikwaju ya penalti 4-2.

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida, ilimalizikakwa timu hizo kufungana bao 1-1 katika muda wa kawaida na ndipo ilipoamuliwa ipigwe mikwajua ya penalti na Yanga kulala kwa matokeo hayo.

Papy Tshishimbi na Emanuel Martin ndio waliokosa  penalti hizo kwa upande wa Yanga, huku nahodha Kelvin Yondani na Gadiel Michael wakipata mikwaju yao.

Kipa wa Yanga, Youthe Rostand alipangua mkwaju wa Malik Antil, lakini akashindwa kufanya hivyo kwa mikwaju iliyopigwa na Shafiq Batambuze, Tafadzwa Kutinyu, Kenny Ally na Elinyeswia Sumbi au Msingida.

Katika mchezo huo uliokuwa mgumu kwa timu zote mbili kutokana na kila upande kuwa na uhitaji wa kutinga hatua inayofuata, kipa upande ulitawala katika kila kipindi, Yanga ikitawala kipindi cha kwanza na Singida cha pili.

Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 23 bao lililofungwa kwa kichwa na winga Yusuph Mhilu baada ya kutumia kona safi iliyopigwa na Ibrahim Ajib.

Hali ya uwanja kujaa maji ilisababisha timu zote kucheza mpira wa pasi ndefu ambazo  hata hivyo haikuwa na faida kwa timu zote mbili ingawa kwa Singida ilionekana kuwanufaisha kwa mipira ya kona ambazo hata hivyo hazikuwa na faida kwao.

Bao la Yanga lilidumu mpaka mapumziko na Singida ilisawazisha dakika ya kwanza ya kipindi cha pili  kupitia kwa  kiungo Kenny Ally baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Kigi Makasi.

Baada ya hapo Yanga ilionekana kutulia na kutafuta bao ambalo lingeweza kuwavusha katika hatua nyingine hata hivyo pamoja na kufanya mabadiliko kadhaa hawakufanikiwa na kadri muda ulivyokuwa ukienda Singida walionekana kuimarika zaidi na kujipanga kuongeza bao.

Singida ilitaka kudhihirisha uimara wake kufuatia mashambulizi mfululizo waliyokuwa wakifanya langoni mwa Yanga,ingawa umahiri wa  Yondani na Andre Vincent uliwapa faida Yanga baada ya kutulia dakika zote 90.

Dakika ya 78 Yanga ilianza kutulia tena baada ya kufanikiwa kudhibiti mashambulizi wa wapinzani wao ambapo dakika tano baadaye Juma Abdul alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa Hassan Kessy, hata hivyo bado ngoma ilikuwa ngumu mpaka dakika 90.

Kwa matokeo hayo Singida itacheza hatua ya nusu fainali na JKT Tanzania wakati Stand United iliyoitoa Njombe FC itaumana na Mtibwa Sugar iliyoitoa Azam, katika nusu fainali nyingine.

Zawadi Zaongezwa Ngorongoro Marathon 2018


Na Mwandishi Wetu
WAANDAAJI wa Ngorongoro Marathon 2018 wameongeza zawadi kwa washindi wa mbio hizo, zitakazofanyika Aprili 21, imeelezwa.

Mkurugenzi wake, Meta Petro alisema juzi kwa njia ya simu kuwa, sasa wameandaa zawadi kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa 15 katika mbio za kilometa 21 wakati awali wanariadha wanne bora ndio walikuwa wakipewa zawadi.
 
Petro alisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanatoa zawadi hadi kwa mwanariadha akayemaliza katika nafasi ya 50 ili kuhakikisha mbio hizo zinakuwa na ushindani wa hali ya juu zaidi kutoka kwa washiriki.

Alisema zawadi hizo zitatolewa kwa washindi wakike na kiume huku katika mbio za kilometa tano, ambazo katika mbio nyingi huwa ni za kujifurahisha na hazina zawadi, wenyewe watatoa zawadi hadi kwa washindi 15 wa kwanza.

Akielezea maboresho hayo, Petro alisema kuwa, kwa upande wa watoto wadogo, ambao watachuana katika mbio za kilometa 2.5, zawadi zimeongezwa hadi kwa mtu atakayemaliza katika nafasi ya 15 badala ya wale wanne wa kwanza.

Alisema kuwa kwa uoande wa kilometa 21 kwa wanaume na wanawake, mshindi wa kwanza ataondoka na Sh milioni 1, wakati wa pili Sh 500,000 wa nne Sh 100,000, watano Sh 80,000, wa sita Sh 70,000, wa saba Sh 60,000, wa nane 50,000, wa tisa Sh 40,000 na wa 10 Sh 30,000.
 
Washindi wa 11 na 12 kila mmoja atapewa Sh 30,000 wakati wa 13 hadi 15 kila mmoja ataondoka nakifuta jasho cha Sh 20,000.

Alisema kuwa kwa upande wa kilometa tano, mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 200,000 wakati wa pili atapewa 100,000 huku yule atakayemaliza watatu atapata Sh 50,000 huku wa nne Sh 30,000 na watano Sh 20,000, na wa sita hadi wa 15 kila mmoja atapewa Sh 10,000.
 
Kwa watoto, mshindi wa kwanza atapewa Sh 50,000 wakati yule wa pili ataondoka na Sh 40,000 huku wa tatu atabeba Sh 30,000, wa nne na tano kila moja atapata Sh 20,000, wa sita Sh 15,000, wa saba hadi wa 12 kila moja atajiondokea na Sh 10,000, wa 13 hadi wa 15 kila moja atapewa Sh 5,000.

Mbio hizo zinadhaminiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  (NCAA) pamoja na Bonite Bottlers, ambapo Petro amezitaka taasisi binafsi pamoja na zile za Serikali na watu binafsi kujitokeza kudhamini mbio hizo zenye kauli mbiu ya `Kimbiza Jangili’.