Sunday 21 October 2018

Timu ya Tanzania Yafanya Maajabu Nagai Marathon

Katibu Mkuu wa Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday (kushoto) akiwa na timu ya Tanzania iliyoshiriki Nagai Marathon, wakati wa kuagwa wiki iliyopita. Timu hiyo imefanya `wonders'. Kulia ni Katinu msaidizi wa RT, Ombeni Zavalla.

Na Mwandishi Wetu
WANARIADHA wa Tanzania wameng'ara katika mbio za Nagai Marathon Japan baada ya kutwaa nafasi za juu.

Mtanzania Marco Joseph wa Talent Athletics Club ya Arusha aliweza kuibuka mshindi kwa upande wa wanaume kilomita 42 akitumia saa 2:21:13 akifuatiwa na Wilbardo Peter wa klabu ya Polisi kwa kutumia saa 2:32:12.

Tanzania pia iling'ara kwa upande wa wanawake km 42 baada ya Angelina John Yumba wa Talent Athletics Club aliyeshinda akitumia saa 2:43:21 muda ambao ni wa kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika Doha Qatar mwakani.

Moto wa watanzania haukuishia hapo tu kwani kwenye nusu marathon km 21 wanaume
Fabiano Nelson Sulle wa klabu ya Polisi alishinda kwa saa 1:02:53.

Kwa upande wa wanawake km 21 moto ulizidi baada ya nafasi zote nne za mbele kubebwa na watanzania ambapo Amina Mohamed Mgoo alishinda akitumia saa 1:16:08 akifuatiwa na Rozalia Fabian Duye 1:18:57 (wote wakitokea klabu ya JKT).

Sylivia Masatu wa Maranatha Athletics Club ya Arusha alishika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 1:32:52 huku Neema Paulo wa Talent Athletics Club akishika nafasi ya nne kwa muda wa saa 1:41:36.

Timu hiyo ya Tanzania inatarajiwa kurejea nchini Oktoba 24 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment