Thursday 4 October 2018

BMT YAIGOMEA RUHUSA TIMU YA TAIFA YA RIADHA ILIYOPASWA KUSHIRIKI MASHINDANO YA NUSU MARATHON YA JUMUIYA YA MADOLA

Taarifa kwa vyombo vya habari

Ndg wanahabari,  

Bilashaka watanzania watapenda kujua sababu ya ukimya wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kuelekea mashindano Jumuiya ya Madola ya mbio za nusu marathon ambapo timu ilitarajiwa kuelekea Cardiff Uingereza  Oktoba 4 kwa ajili ya mashindano yanayo tarajiwa kufanyika Oktoba 7 2018, na timu zote zinazoshiriki kurejea makwao Oktoba 8 2018.

Tunasikitika kutoa taarifa rasmi kwamba RT ilipambana na changamoto za kifedha na hatimaye kufanikiwa kupata fedha kwaajili ya safari. Timu ya taifa ya riadha ilikuwa imejiandaa kwa utaratibu tuliojiwekea pamoja na makocha wetu waliopo Arusha. Pamoja na kuwepo na barua zote za mialiko na uhakikisho wa kugharimiwa gharama zote za kukaa uingereza, lakini Baraza la Michezo Tanzania (BMT) iliona ni busara kuinyima timu ya taifa ya riadha haki ya kushiriki mashindano hayo muhimu sana kwa nchi yetu.

“Sijapata kusikia hata siku moja kwamba timu iliyostahili kuagwa kitaifa na kukabidhiwa bendera na kiongozi wa ngazi ya kitaifa inanyimwa ruhusa kwa sababu zisizo za msingi”

Kwa mujibu wa barua iliyopokelewa na RT kutoka BMT imeainisha katazo ambalo halina mashiko yoyote ya kiufundi hadi kusababisha taifa kukosa nafasi muhimu kama ya kushiriki mashindano ya Nusu marathon ya Jumuiya ya Madola. Ni jambo la kushangaza kuona BMT inaingilia kati uteuzi wa wanariadha wa timu ya taifa wakati wao ni wasimamizi wa sheria na kanuni za michezo yote nchini. Lakini kwa barua hiyo inaonekana kana kwamba BMT inawamiliki wanariadha wetu wakati ni Dhahiri hawajasimamia  shughuli yoyote ile ya maandalizi wala kuchangia gharama yoyote ya kambi ya mazoezi hadi leo hii. Wanariadha waliochaguliwa kuwakilisha taifa ni nane. Kati ya hao wanariadha wawili wamo kwenye orodha ya wanariadha watakaokwenda Japan kwenye Nagai Marathon pamoja na msafara wa BMT. Chakushangaza barua ya BMT imeinyima ruhusa timu nzima ya taifa, ilikukidhi matakwa ya BMT yasio na weledi wala maono ya mbali. Wanariadha waliokuwemo kwenye msafara wa kwenda japan ni Fabiano Sullen na Marco Joseph.

Pamoja na jitihada za kuwaeleza BMT kwamba RT tunatumia busara na ufundi zaidi kuhakikisha kwamba nchi yetu inawakilishwa vyema katika mashindano yote mawili, pamoja na hayo BMT imekataa na kuamua kutumia mamlaka yao kibabe. Matokeo yake timu ya taifa ya riadha haitashiriki kwenye mashindano muhimu ambayo wanariadha wetu wangeweza kupata fursa ya kufuzu kwenda kwenye mashindano ya Olimpiki yam mwaka 2020 nchini Japan. Mashindano ya Cardiff yanatambuliwa na Shirikisho la Vyama vya riadha Duniani (IAAF) na hivyo watakaofanya vizuri wanafuzu moja kwa moja kwenda kwenye mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto. Kutokana na uamuzi wa BMT timu haiendi Cardiff kwasababu BMT wameamua kuonyesha kwamba wana nguvu na mamlaka.

Kimsingi BMT inadai kwamba zuio la safari ya Cardiff kwa timu ya taifa imewekwa eti kwa sababu ya Nagai Marathon. Zaidi ya hapo barua hiyo imeeleza kwamba RT haiheshimu msaada mkubwa tunaopata kutoka Japan! Sababu ambayo haina mashiko kwa mchezo wetu wa riadha na ni wazi ni ya kuchukua maamuzi bila ya kufikiria kwa mapana.

RT ingependa kupambanua umuhimu wa mashindano yote mawili (Nagai Marathon na Nusu Marathon ya Jumuiya ya Madola);

1)    Commonwealth Half Marathon inakimbiwa Oktoba 7 (wiki 2 kabla ya Nagai) ambapo wanariadha wangerudi na kuweza kuwahi hiyo mbio ya Nagai
2)    Commonwealth Half Marathon ni mashindano ya medali wakati mbio za Nagai siyo ya medali bali ni ya kujenga ushirikiano kati ya Tanzania na Japan kuelekea Tokyo Olimpiki 2020
3)    Kiufundi hakuna tatizo lolote kwa mwanariadha kukimbia nusu marathon kabla ya marathon. Nusu marathon ndiyo ingekuwa jaribio zuri kuelekea full marathon ya Nagai
4)   Wanariadha walioteuliwa kwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola wamefikia vigezo (sababu wameshawahi kushiriki mbio za 21km), hivyo hawaendi kubahatisha au kujaribu
6)    Wanariadha waliochaguliwa kwenda Nagai, ni wale ambao wanakimbia marathon ya km 42 kwa mara ya kwanza, hivyo wanakwenda kwenye majaribio ya mbio ndefu.
7)    Katika safari ya Nagai kuna viongozi watatu wa BMT wanakwenda na timu ya Riadha, huenda hiyo ndiyo sababu ya kuthamini Nagai kuliko Madola
8)    Kwa maana nyingine ni sawa na kusema wajumbe wa BMT wamegeuka kuwa viongozi wa RT. RT itawakilishwa na Naibu KM na Katibu Kamati Ufundi
9)    Madhumuni ya Nagai ni kuimarisha uhusiano hasa kwa wanariadha wanawake kufuatia mashindano yaliyofana ya JICA Ladies Championships, ni jambo la heri sana lakini siyo sababu ya BMT kunyanyasa Shirikisho lenye jukumu la kuendesha program zake kwa uhuru. Kwanini BMT wasiingilie shughuli za TFF? Kuna uhusiano gani kati ya mashindano ya Nagai na ya Cardiff?
Tanzania ni mwanachama wa nchi za Jumuia ya Madola, tunapatashida kumuelewa kiongozi wa michezo ambaye haelewi kwamba ushiriki wetu ni muhimu sana, katika mfumo mzima wa umoja wa nchi za Jumuiya ya Madola na michezo ndiyo jambo kubwa linalohusisha jamii moja kwa moja (The games are the Commonwealth's most visible activity). Je mtendaji mkuu wa BMT hilo halifahamu?

Utata mwingine huu hapa;

Mwanzoni kabisa Kamati ya Ufundi ilimchagua Ndg William Kallaghe (Makamu Rais RT) kuwa sehemu ya msafara wa Nagai, lakini ikaja hoja ya kuupinga uongozi wa juu wa RT kushiriki Nagai (sababu hatuifahamu sana), hoja yenyewe ilikuwa kwamba “hii ni issue inayowahusu wanawake zaidi, lakini tumeamua kutoa nafasi kwa wanariadha wanaume pia” hivyo ikasemekana waende viongozi wanawake ndiyo wanapaswa kuambatana na timu isipokuwa kocha 1 mwanaume.

Sasa mimi nahoji mambo machache;

1)    Katika msafara huo wa Nagai mkuu wa msafara ni Mohamed Kiganja; je yeye ni mwanamke?
2)    Pia kuna Benson Chacha; je yeye pia ni mwanamke?
3)    Kama swala ni la wanawake; BMT hakuna wanawake?
4)    Sina tatizo na Kanali Mstaafu (Juma Ikangaa) maana yeye ni balozi wa JICA lazima aende
5)    Uwepo wa Ombeni Zavala na Rehema Kilo upande wa RT ni sawa sababu wao ni wanawake
Lakini hayo yote tusingehoji kama tusingewekewa vikwazo vyenye dhamira ya kuingilia utendaji wa shughuli zetu za kusaka medali, jitihada za kujitegemea na jitihada za kimkakati kuelekea Tokyo Olympics 2020.

Hili swala la kutojali mipaka ya kiutendaji inahitaji kuangaliwa na Wizara yenye dhamana ya michezo, maana safari hii ni wazi kabisa kwamba watendaji wa BMT wanatumia madaraka yao vibaya. Tunayasema haya yote kwa kujiamini kabisa kwamba BMT wameinyima nchi haki yake ya kimsingi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za jumuia ya madola ambayo Tanzania ni wanachama. Hayati Baba wa Taifa aliona umuhimu wa kujiunga na Jumuia ya Madola, lakini watendaji wa BMT hawalioni.

Watendaji wa BMT wangekuwa makini wasingefanya uharibufu huu;

Agosti 14 hadi 31/2018 msafara ulioongozwa na BMT ulikwenda nchini Burundi, kwa upande wa riadha walikwenda wanariadha ambao wengi wao hawakushiriki, walikula na kulala kwa gharama za serikali, na hata posho walilipwa kila mmoja zaidi ya 700,000. Je kwanini walitumia gharama za serikali kuwagharimia watu ambao hawakushiriki? Unaondokaje kama hujui status ya Local Organizing Committee ya unakokwenda? Ni shilingi ngapi za walipa kodi zimetumika kwa uzembe huo? 

Wanariadha waliokwenda Burundi ni wafuatao;
  1. Michael Gwandu - Long Jump / Triple Jump (Hajashiriki)
  2. Ally Gulam - Mita 100 / 200 (Hajashiriki)
  3. Rose Seif – Mita 200 / 400 (Hajashiriki)
  4. Neema Gadiye - Mita 800 / 1500 (Hajashiriki)
  5. Natalia Sulle - Ameshiriki 21K
  6. Marco Joseph - Ameshiriki 21K
  7. Angelina Yumba - Ameshiriki 21K
Wanariadha watatu walioshiriki hawakwenda Burundi kukimbia Half Marathon, walikwenda kwa ajili ya 10K. Hapo ndipo utaona BMT wamevamia shughuli za RT kwa asilimia 100. Magufuli kasema asiyefanya kazi na asile; sasa kwanini wanariadha ambao hawakufanya kazi wamelipwa na kula bure? Mbaya zaidi wamepoteza muda wao wa kufanya mazoezi sababu wakiwa Burundi hawakua huru kufanya mazoezi kutokana na miundombinu hafifu na usalama wao pia.

Kwa kunyimwa ruhusa tayari RT tumeshawajulisha waandaaji wa Cardiff Commonwealth Half Marathon kwamba tumeshindwa kuja, tumewaomba radhi na kuwatakia mashindano mema kwa nchi zote zitakazoshiriki wakiwemo majirani zetu Kenya, Uganda na Rwanda.

RT tunatambua juhudi za kizalendo za mtanzania mwanariadha ANTHONY MWANGA, anayeishi Afrika Kusini, ambaye aliiwakilisha taifa katika mashindano ya Jumuia ya Madola huko Gold Cost Australia. Mtanzania huyu, alituandalia mazingira mazuri ya timu ya taifa ya riadha ipitie jijini Johanesburg ili kupata visa ya haraka (kama ilivyokuwa kwa mwanariadha Alphonce Simbu) wakati akielekea London Marathon mwaka jana.

Tunawaomba radhi wanariadha wetu ambao kwa mwezi mzima wamefanya mazoezi makali na kwa gharama wakitegemea kwenda kupeperusha bendera ya nchi yao; BMT imezima ndoto yao kwa sasa, waendelee kujiandaa maana kuna mashindano mengi makubwa yanakuja. Nawapongeza sana wanariadha wetu kwa kuahirisha mialiko yao binafsi kusudi waiwakilishe nchi yao ili Tanzania ipate medali na sifa.

Namshukuru Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania pamoja na Makamu Rais wote wawili, Naibu Katibu Mkuu na Kamati nzima ya Utendaji ya RT kwa hatua nzuri walioifikia kimkakati. Changamoto kama hizi za kuingiliwa kiutendaji hazitatukatisha tamaa.

Pamoja na yote yaliyotokea Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) linawatakia wote waliopo kwenye msafara wa Nagai Japan safari njema na yenye mafanikio, wanariadha wanaokwenda Nagai wamepata mafunzo kutoka kwa makocha wanaojitolea bila kudai fidia yoyote, nawapongeza na kuwaambia RT inatambua uzalendo wenu.

Asanteni sana kwa ushirikiano wenu wa mara kwa mara.
  
Imetolewa leo Oktoba 4 / 2018.  

No comments:

Post a Comment