Thursday 11 October 2018

SBC Kuwapeleka Lebanon Washindi Rotary Marathon 2018

Meneja Masoko wa SBC, Roselyne Bruno akizungumza na waandishi wa habari wakati wakitangaza ofa ya wanariadha wa Tanzania watakaoshinda mbio za Dar Rotary Maratthon kupata ofa ya kwenda Lebanon.

Na Mwandishi Wetu
WASHINDI wawili wa Dar Rotary Marathon zitakazofanyika mwishoni mwa wiki hii, watapata ofa ya kwenda kushiriki Beiruti Marathon nchini Lebanon mwezi ujao.

Meneja Mafunzo na Uwezeshaji wa Kampuni ya Peps nchini, SBC, Rashid Chenja alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, wanariadha wa Tanzania watakaoshika nafasi ya kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake katika Rotary Marathon 2018 kilometa 42, watapata ofa ya kushiriki Lebanon Marathon 2018.
Meneja Mafunzo na Uwezeshaji wa Kampuni ya Peps nchini, SBC, Rashid Chenja katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za Riadha Tanzania (RT). Kushoto ni kiongozi wa wanariadha, Jilala.
   Beirut Marathon itafanyika Novemba 11 nchini Lebanon, ambapo washindi hao wa Tanzania watawezeshwa kila kitu ili kwenda na kushiriki mbio hizo, ikiwemo viza, tiketi ya kwenda na kurudi, bima na mambo mengine ili washiriki vizuri mbio hizo.

Chenja akifafanua alisema kuwa hata kama mwanariadha wa Tanzania atamaliza katika nafasi ya tano katika washindi wa jumla, atakuwa amekidhi vigezo vya kupata ofa hiyo kwa kuwa atakuwa ni Mtanzania wa kwanza katika matokeo hayo ya Rotary Marathon 2018.
Rashid Chenja akizungumza.
Alisema lengo la SBC ni kuhakikisha wanariadha wa Watanzania wanapata motisha zaidi na kuwawezesha kufanya vizuri ili washindie mbio hizo, ambazo kampuni hiyo imedhamini kwa miaka 10 sasa.

Mbio hizo mbali na kupita katika mitaa mbalimbali ya jijini la Dar es Salaam, zitaanzia katika Uwanja wa The Green au Farasi uliopo Oysterbay, ambako washindi watakabidhiwa zawadi zao.
Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla alishukuru kwa SBC kutoa ofa hiyo kwa wanariadha wa Tanzania kushiriki mbio Lebanon, lakini aliwataka kujitahidi kuvunja rekodi ya njia ili kuongeza msisimko katika mbio hizo.

Alisema kwa miaka takribani 10 mbio hizo zimekuwa zikifanyika, lakini rekodi ya njia hiyo hajawahi kuvunjwa, hivyo aliwataka wanariadha kuhakikisha wanaivunja rekodi hiyo ili kuboresha zaidi mbio hizo.
Jilala akizungumza kuhusu ofa hiyo ya SBC kuwapeleka wanariadha Lebanon.
Mbali na mbio za kilometa 42, pia kutakuwa na zile za kilometa 21, 10 na zile za kilometa 5, ambazo ni za kujifurahisha.

No comments:

Post a Comment