Monday 15 October 2018

Waeleza Umuhimu wa Kutoa Taarifa za Miradi ya Maendeleo

Na Mwandishi wetu
IMEELEZWA kuwa kuna umuhimu wa kutoa taarifa kwa wananchi zinazohusu utekekezaji wa miradi ya maendeleo.
  
Wakizungumza katika mkutano wa kuandaa taarifa kwa wadau wa maji katika kata za Kwembe, Msigani na Kibamba, washiriki wamesema sheria na taratibu zilizo wekwa taarifa ni muhimu ili wananchi wawe na mrejesho wa miradi inayowahusu.

 Mwezeshaji wa mkutano huo ulioandaliwa na  Asasi ya Pakacha na kufadhiliwa na The Foundation For Civil Society, Bumija Moses amesema wananchi wanaweza kuleta msukumo wa kiutendaji kwa viongozi kama wakishirikishwa kupata taarifa   za miradi inayojengwa na utekelezaji
wake.
Mkutano huo ulikutanisha wananchi na viongozi kutoka katika katika kata tatu za Kwembe, Msigani na Kibamba.

Mkutano huo ulifanyika Ijumaa mjini Kibaha.

Diwani wa viti maalumu (Chadema) wa kata ya Msigani,mheshimiwa Vicky Mchome amesema ushirikishwaji wa wananchi katika sehemu nyingi, ikiwemo kata yake haupo akitoa wito kwa wananchi kupewa taarifa.

 Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kwembe, Peter Chawala amesema wananchi wasisubiri kushirikishwa, wana haki ya kuuliza viongozi wao ili kupata taarifa zinazowahusu.
  
Adam Kingu, mkazi wa Maramba Mawili amesema licha ya wananchi, wapo
pia baadhi ya viongozi ambao hawapati taarifa za utelekezaji wa miradi ya Maji.

“Unaweza kwenda kumuuliza mtendaji lakini cha kushangaza hajui bajeti  iliyotengwa au hata mradi unaotekelezwa”, amesema Kingu.

Kata za Kwembe, Msigani na Kibamba zina changamoto za upatikanaji wa maji, hivyo kupelekea Pakacha kuunda kamati maalumu iliyowashirikisha wananchi na kupita katika kata zote ili kujua kuna miradi ipi ya maji iliyotengewa bajeti na hatua iliyofikia katika utekelezaji wake.

Mmoja wa mjumbe wa kamati hiyo, Almas Mohamed amesema wamepata malalamiko mengi ya wananchi kutojua utekelezaji wa miradi ya maji iliyopo katika kata zao.

Miongoni ya miradi hiyo ni ujenzi wa kisima cha maji cha Kibamba kilichotengewa milioni 280 kwa utekelezaji wa kuanzia mwezi April mwaka jana mpaka june mwaka huu na ujenzi wa tanki la maji lililopo Kwembe Kingazi B uliotengewa  milioni 55, ukiwa katika hatua za mwisho.

Katibu wa Pakacha, Haroun Jongo amesema serikali inafanya jitihada kubwa kuleta maendeleo kwa wananchi, ndio maana asasi kama Pakacha zinapata fursa ya kuelimisha wananchi.

“lengo la mkutano huo ni kuandaa taarifa kwa kuwashirikisha wananchi, baada ya kufanya upembuzi yakinifu ya miradi iliyopo.

Ufuatiliajia unafanywa kupitia Pets, amesema Jongo

No comments:

Post a Comment