Thursday 4 October 2018

Naibu Waziri Kwandikwa Ataka TB3 Iishe Kwa Wakati


Jengo la Tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA Terminal 3) linavyoonekana kwa mbele.
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, amewataka wasimamizi na wakandarasi wa mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kumaliza kwa wakati kama inavyoelezwa kuwa ni Mei 2019.

Mhe. Kwandika ametoa kauli hiyo leo alipokamilisha ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ambao imeelezwa umeshafikia asilimia 83 kukamilika.

“Nimejionea mradi unaendelea vizuri kwani mara ya mwisho nilipita hapa wakati ukiwa na asilimia 56 lakini sasa maendeleo ni makubwa, lakini ninasisistiza mradi uishe kwa wakati ili uweze kutoa huduma bora kwa abiria, kwani ninauhakika watakuwa wengi tofauti na jengo la pili la abiria,” amesema Mhe. Kwandikwa.
Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja wa Tanroad Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama wakati Kwandikwa alipotembelea Jengo la Tatu la Kiwanja cha Ndege Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Kushoto ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, TAA, Richard Mayongela na Mhandisi Barton Komba.
Hatahivyo, amesema mkandarasi anaendelea kulipwa kulingana na madai yake kila anapowasilisha cheti cha madai na madeni wanayoidai serikali wataendelea kulipwa kwa kufuata taratibu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela amesema Mamlaka inaishukuru serikali kwa ujenzi wa jengo hilo, ambalo litatatua kero ya msongamano kwenye jengo la sasa.

“Tunalipokea jengo hili kwa mikono miwili na tunaishukuru sana serikali kwa miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege,” amesema Mayongela.

Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Naibu Waziri kabla ya kuanza ziara ya kukagua Jengo la Tatu la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA).
Hatahivyo, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangamia fursa za uwekezaji kwenye jengo la tatu la abiria na viwanja vingine vya ndege, ambapo kunamaeneo ya migahawa, maduka ya bidhaa mbalimbali vikiwemo vito na huduma ya usafiri.

Pia amewaaasa wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege kwa kufanya makazi na kufanya shughuli nyingine za kibinadamu kwa kuwa ni hatari kwa usalama.

Awali mmoja wa Wahandisi Wasimamizi wa JNIA-TB3, Mhandisi Barton Komba amesema mradi umekamilika kwa asilimia 73 upande wa jengo, huku asilimia 75 upande wa maegesho ya magari na asilimia 92 kwenye maegesho na viungio vya ndege.

Mhandisi Barton Komba akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa (wa pili kushoto) wakati Kwandikwa alipofanya ziara katika Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimatafa cha Julius Nyerere.. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela na kulia ni Meneja wa Tanoroads mkoani wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama. 
Hatahivyo, Mhandisi Komba amesema mradi unakumbwa na changamoto ya mkandarasi na Mhandisi Mshauri kutolipwa kwa wakati, hali kadhalika kutorudishiwa kwa kodi kiasi cha Euro. 4,904,000 ambapo awali kulikuwa na msamaha wa kodi, lakini sasa sheria imebadilika anapaswa kulipa.
Mkandarasi wa mradi huo wa Kampuni ya BAM International, Bw. Wolfgang Marchick amesema pamoja na mradi huo kuajiri Watanzania asilimia 95 lakini bado wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kulipa kodi, ambayo imekuwa ikiwaumiza.


Jengo hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita (6) kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment