Monday 15 October 2018

Vichekesho vya Mwantumu vyaongezwa Udambwi-dambwi

Lucas Mhuvile au Joti (mwenye miwani) wakati wa uzinduzi wa msimu wa pili wa vichekesho vya Mwantumu leo katika ofisi za DStv Jijini Dar es Salaam. Kulia ni msanii mkongwe Bafadhili.

 *Sasa Kuonekana Mara Mbili kwa Wiki

*Msimu wa Pili Waja kwa Kishindo Kikubwa

Na Mwandishi Wetu
MSIMU Msimu mpya wa vichekesho maarufu vya Mwantumu ambavyo huonekana kupitia chaneli ya DStv ya Maisha Magic Bongo,  unaanza rasmi Jumanne Oktoba 16,  huku vikiwa vimeongezewa manjonjo ili kuwahakikishia watazamaji na mashabiki wake burudani isiyo na upinzani.

 Vichekesho hivyo vinavyoongozwa na mchekeshaji maarufu nchini Lucas Mhuvile maarufu kwa jina la kisanii JOTI ambaye kwenye vichekesho hivi amevaa uhusika wa watu watatu tofauti.
Joti katikapicha za uhusika tofauti tofauti katika vichekesho vya Mwantumu.
Joti katika vichekesho hivyo anacheza uhusika wa Mzee Mrisho, Kaboba na Mwantumu Sahare,  ambapo vichekesho hivyo vimekuwa ni moja wa vipindi vinavyotazamwa sana na kupendwa na maelfu ya watu hapa nchini ambapo huoneshwa kupitia chaneli maarufu ya Maisha Magic Bongo – DStv 160. 

Majina maarufu pia katika tasnia ya uigizaji na uchekeshaji yatakuwepo msimu huu akiwemo Mzee Fungafunga (Mzee Mwalubadu), Mama Abduli (Mwantumu Mcharuko), Alex Wasponga(Kayombo) na wengineo wengi
  
Shumbana wakati wa uzinduzi wa vichekesho vya Mwantumu leo.
Akizungumza katika uzinduzi rasmi wa msimu wa pili wa vichekesho hivyo, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Alpha Mria amesema kuwa tangu kuanza kwa msimu wa kwanza wa vichekesho vya Mwantumu mnamo Oktoba 2017, vichekesho hivyo vimekuwa na msisimko wa aina yake na vimepokelewa vizuri sana na watazamaji na hivyo kuvifanya kuwa na mashabiki wengi sana.

 Amesema msimu huu wa pili, watazamaji wa Maisha Magic Bongo na mashabiki wa Mwantumu watashuhudia mikasa ya aina yake, ambapo baada ya Bahati kupata ujauzito, baba yake mzee Mwalubadu anaamua kumpeleka Kaboba katika vyombo vya sheria kwa kosa la kumpa Bahati ujauzito.
Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Alpha Mria akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mwantumu leo.
Hata hivyo suala hilo linafika kwa Babu yake Kaboba mzee Mrisho, ambaye wakati huohuo hataki Kaboba apate matatizo yoyote. Kinachotokea hapo ni drama ya aina yake itakayowaacha watanzamaji wakivunjika mbavu kwa kucheka!

 “DStv kupitia Chaneli yake pendwa ya Maisha Magic Bongo, siku zote imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunatoa msisitizo kwenye maudhui ya ndani na vichekesho hivi ya Mwantumu ni mfano halisi. Hii ni yetu, imetengenezwa hapa tanzania na wazalishaji, waandaaji na waigizaji wote wa hapa hapa nchini” alisema Alpha.
Joti akizungumza leo.
 Vichekesho vya Mwantumu vilianza msimu wa kwanza mnamo Oktoba 2017 Na kuendelea kwa muda wa mwaka mmoja ambapo vilikuwa vikionyeshwa mara moja kwa wiki. Katika msimu huu mpya vichekesho hivyo vitaonekana mara mbili kwa wiki siku ya  Jumanne na  Jumatano  saa moja na nusu usiku. 
Hii itawapa fursa mashabiki na watazamaji wa Maisha Magic Bongo kupata burudani zaidi kwani kumekuwa na maombi mengi ya kuongeza vipindi hivyo kutokana na umaarufu wake.


No comments:

Post a Comment