Tuesday 6 September 2016

bonanza la uzinduzi wa mashindano ya Shimiwi kufanyika jumamosi huku mashindano yakifanyika dodoma kuanzia Oktoba 14 hadi 27


Baadhi ya watazamaji wakifuatilia mashindano ya Shimiwi yaliyofanyika mkoani Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Na Mwandishi Wetu
BONANZA la uzinduzi wa Michezo ya Watumishi wa Serikali (Shimiwi), litafanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mkuu wa Shimiwi Moshi Makuka, bonanza hilo linatarajia kuanza saa 12:30 asubuhi na kushirikisha watumishi wote wa Serikali kutoka katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema kuwa mgeni rasmi katika bonanza hilo atakuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Watumishi wa Umma Balozi John Kijazi.

Michezo ya mwaka huu ya Shimiwi itafanyika mkoani Dodoma kuanzia Oktoba 14 hadi 27.

Makuka alizitaja sababu zilizopelekea kufanyia michezo hiyo mkoani Dodoma ni pamoja na kuunga mkono agizo la Rais Dkt John Pombe Magufuli la Serikali kuhamia katika Makao Makuu Dodoma.

Sababu nyingine ni kuwapa nafasi Watumishi wa Umma ambao hawajawahi kufika Dodoma kufahamu mazingira na kufanya maandalizi muhimu kwa ajili ya kuhamia.

Tarehe 14 Oktoba, 1999 siku ambayo Mwalimu Nyerere alipoaga Dunia Watumishi wa Umma tulikuwa katika michezo hii mkoani Morogoro, hivyo sisi (Watumishi wa Umma) tahrehe hiyo ni kumbukumbu muhimu ya kifo chake, pia ni ni kuenzi agizo lake la kuhamia Dodoma, alisema Makuka.

Alisema kuwa michezo ya mwaka huu itaanza kwa ibada maalum kwa ajili ya kumuombea Baba wa Taifa pia kumtakia afya njema Rais Magufuli pamoja na wasaidizi wake.

Pia Shimiwi itatumika kupanda miti katika maeneo yatakayoelekezwa na Serikali ya mkoa wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment