Thursday, 24 May 2018

DStv Kutangaza Kombe la Dunia Kwa Kiswahili

Wadau mbalimbali wa michezo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface (watatu kushoto) wakipata futari jana katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
ZIKIWA zimebaki siku kadhaa kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi, Kampuni ya Mult-Choice kupitia king’amuzi chake cha DStv, itatangaza mechi zote za Kombe la Dunia kwa lugha ya Kiswahili.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua  wa mashindano hayo, Mkuu wa Uendeshaji wa Mult’Choice Tanzania Ronald Selukindo alisema kuwa wametenga chaneli sita, ambazo zitakuwa maalum kwa Kombe la Dunia, ambalo linaanza Urusi kuanzia Juni 14 hadi Julao 15.
Alisema chaneli hizo zote zitaonekana kwa kiwango cha hali ya juu, ambacho ni cha HD, ambacho kitawawezesha wateja kuona mechi zote za Kombe la Dunia kwa picha zenye ubora wa hali ya juu.
Mwenyekiti wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga (wa pili kushoto) wakati wa kufuturu futari iliyoandaliwa na MultChoice Tanzania jana katika hoteli ya Serena.
 
“Hii ni zaidi ya ofa” alisema Ronald Shelukindo, “Sasa tunataka Watanzania waweze kupata burudani ya Kombe la Dunia 2018 kwa namna tofauti kabisa. Kwanza kwa wateja wapya wataweza kujiunga kwa Sh 79,000 tu na kupata seti ya DStv pamoja na kifurushi cha miezi miwili bure!” alisema Shelukindo.

Pia alisisitiza kuwa mbali na kutangaza kwa kugha ya Kiswahili kwa kutumia watangazaji wa michezo waliobobea wa hapa nchini pamoja na wachambuzi wake, ambao watakuwa nchini wakitangaza na kuchanbua mechi hizo kwa Kiswahili.
 

Alisema pia wateja wa DStv sasa wataweza kutazama chaneli hizo popote kupitia katika simu zao za mkononi, na tablet
Akitoa maelezo kuhusu jinsi DStv ilivyojizatiti kuwahakikishia Watanzania burudani isiyo na kifani msimu huu wa Kombe la Dunia, Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania, Alpha Mria, amebainisha kuwa DStv itaonesha michuano hiyo katika vifurushi vyake vyote,
 “Kwakeli msimu huu wa Kombe la Dunia, kila atakayekuwa na DStv atakuwa anapata kile anachostahili, kwani mechi zote zitaonekana live, kwenye HD na kwenye vifurushi vyote, huku pia zikitangazwa kwa lugha mbalimbali, ikiwemo lugha ya Kiswahili,” alisema Alpha.
Alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha kila mtu anapata matangazo kupitia lugha anayoitaka kama Kifarasa, Kiingereza na lugha zingine ikiwemo lugha adhimu ya Kiswahili.
 “Tumejipanga, kuwapa Watanzania burudani ya aina yake msimu huu wa Kombe la Dunia,” alisisitiza Alpha.
Katika uzinduzi huo, DStv iliwatambulisha rasmi watangazaji wa soka, ambao watakuwa wakiwaletea Watanzania matangazo ya Kiswahili, ambao ni Aboubakary Liongo, Maulid Kitenge, Ephaim Kibonde, Edo Kumwembe, Ibrahim Masoud - Maestro na Oscar Oscar.
Wakiongea baada ya kutambulishwa, watangazaji na wachambuzi hao mahiri wa soka wamesema wamejizatiti kikamilifu kuhakikisha kuwa wanawaletea matangazo na uchambuzi wa kina ili kuhakikisha kuwa kila mpenda soka anafurahia na kuyaelewa vizuri mashindano hayo.

Aidha, MultChoice ilifurisha wadau mbalimbali wa michezo jana jioni katika hoteli ya Serena kabla ya kufanyika kwa uzinduzi rasmi wa Kombe la Dunia 2018 kwa kiswahili.


Tuesday, 22 May 2018

TAA Yaandaa Mikakati Kudhibiti Viashiria Hatarishi

Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Ndani wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Irene Sikumbili (aliyenyoosha mkono kulia), akitoa ufafanuzi kwa washiriki wa mafunzo ya Viashiria hatarishi (Risk Management) yanayohusisha Watumishi wa Mamlaka hiyo, yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Veta jijini Dar es Salaam.
 
Mwandishi Maalum
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeanza mikakati ya kujiwekea mfumo wa viashiria hatarishi (Risk Management) kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wake, ambayo yameanza jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) uliopo Kipawa jijini Dar es Salaam.
 Mkaguzi Mkuu wa Ndani kutoka ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Bw. Dickson Austin (aliyesimama) akifundisha washiriki wa mafunzo ya viashiria hatarishi (Risk Management) kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), jana kwenye ukumbi wa VETA Kipawa jijini Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, ambayo yanashirikisha washiriki kutoka Idara mbalimbali, Bw. Lawrence Thobias ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala,  amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatatumika kama sehemu ya kazi, hivyo washiriki wote wazingatie na kujifunza kwa bidii.

“Ninajua wote waliopo kazini wanauwezo na nyie mmechaguliwa wachache na hamuwezi kuja wote katika mafunzo haya, ila ninachowaomba mjifunze kwa bidii na mshirikishane yale mnayoyafahamu, kwani wote hapa ni wazoefu ili kuleta ufanisi bora na mzuri katika Taasisi yetu,” amesema Bw. Thobias.
  Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Lawrence Thobias (aliyesimama) akifungua mafunzo ya siku tano ya kutambua viashiria hatarishi (Risk Management) yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Veta Kipawa jijini Dar es Salaam.
Bw. Thobias amesema kuwa baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo,  TAA itatengeneza nyaraka za viashiria hatarishi kwa kutumia wataalamu watakaochaguliwa miongoni mwa washiriki, ambazo zikikubalika kwa viwango vinavyotakiwa, basi itatakiwa kusimamiwa na kuendeshwa vyema na Mamlaka.

Naye Naibu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali (Usimamizi wa Viashiria Hatarishi, Mfumo na Udhibiti wa Ndani), kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu Bw. Emmanuel Subbi kutoka Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu, amesema wameamua kutoa mafunzo ya viashiria hatarishi (Risk Management) kwa Taasisi za Serikali ili waweze kuishauri Serikali namna ya kuvizuia na kuvidhibiti kabla ya kutokea.
      Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi anayeshughulika na Usimamizi wa Viatarishi hatarishi, Mifumo na Udhibiti wa Ndani, Bw. Emmanuel Subbi kutoak ofisi ya Mkaguizi Mkuu wa Hesabu, akionesha Mwongozo wa serikali wa mwaka 2012 kwa washiriki wa mafunzo ya siku tano ya Viashiria hatarishi (Risk Management) wanaotoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Bw. Subbi amesema kila Taasisi inatakiwa kuwa na mwongozo wa viashiria hatarishi wa mwaka 2013 na pia Waraka wa Hazina namba 12 wa mwaka 2013, ambapo zote zinaonesha namna na jinsi ya kuzuia viashiria hatarishi.

“Mfumo huu una faida kubwa kwa Taasisi za Umma kwani unasaidia kuaminika na hata kupata mikopo kutoka katika Taasisi mbalimbali Duniani, pia mfumo huu utakupa nafasi nzuri ya kufanya maamuzi kwa upana ikiwa unaangalia na mfumo wako wa kazi,” amesema Bw. Subbi.
 Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Lawrence Thobias (wa kwanza kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki na wakufunzi wa mafunzo ya viashiria hatarishi (Risk Management) yanayofanyika kwenye ukumbi wa Veta-Kipawa, jijini Dar es Salaam. (Picha zote Bahati Mollel wa TAA)
Pia Bw. Subbi amesema mfumo huu utasaidia kuepuka matatizo katika ununuzi, sheria, viwango na udhibiti, ambapo miaka ijayo itapunguza kupatikana kwa hati chafu kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), ambapo mfumo ukizingatiwa hakutakuwa na matatizo hayo kwani watagundua viashiria hatarishi kabla havijatokea na kuleta madhara.


Saturday, 19 May 2018

Wanausalama Viwanja vya Ndege Waimarika



Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Vedastus Fabian (katikati waliokaa), akiwa kwenye picha ya pamoja na wakufunzi na washiriki wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo inayosafirishwa kwa ndege, mara baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo jana katika Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo Jengo la Kwanza la abiria la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere. (Picha zote na  Bestina Magutu wa TCAA).



Na Bahati Mollel,TAA
WANAUSALAMA wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini, wameiva na kuimarika katika usalama wa vifurushi na mizigo inayosafirishwa kwa njia ya ndege baada ya jana kufuzu mafunzo yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), iliyofanyika kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo katika Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Wakati akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Vedastus Fabian kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, amewataka wahitimu hao kutumia vyema ujuzi walioupata kwa kufanyakazi kwa ufanisi na kuboresha kazi hiyo, ili kuepuka kupitisha mizigo hatarishi kwa usalama wa usafiri wa anga.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Vedastus Fabian (aliyesimama) akiwahutubia wahitimu wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo (hawaonekani pichani) wakati akifunga mafunzo hayo jana kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo katika jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).


“Tunavyojua mfumo wa usafiri wa anga duniani ni moja kwa hiyo tunavyoonesha usalama katika viwanja vyetu vya ndege hapa Tanzania kunajenga imani kubwa kwa mashirika ya ndege na wadau wote wanaofanya shughuli nakutumia viwanja vyetu vya ndege, hivyo tutaongeza wingi wa mizigo,” amesema Fabian.

Hata hivyo, alitoa pongezi kwa wahitimu wote 19 kwa kuweza kufaulu vyema mafunzo hayo, ambapo sasa watakuwa na weledi na ufanisi bora katika kazi hiyo.

Amesema TAA inategemea mafunzo hayo yataleta manufaa na sio kuonesha vyeti ukutani kuwa wamehitimu bali ni kuonesha ujuzi walioupata kutasaidia kutambua mizigo na vifurushi vyenye matatizo ya kutishia usalama wa anga na kuongeza uhakika wa safari za anga.

Mkufunzi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), Bw. Sunday Mweemba wa Zambia akielezea namna walivyotoa mafunzo kwa wahitimu wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo akishirikiana na mkufunzi mwenzake Bw. Ernest Bongane wa Afrika ya Kusini, wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyomalizika jana kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).
Fabian pia amesema wanategemea washiriki kufikisha na kusambaza ujuzi huo kwa wanausalama wengine, ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo adimu, ili nao waboresha kazi zao.

Hali kadhalika amewataka washiriki kujiendeleza zaidi kwa kupata mafunzo  mbalimbali ya masuala ya usalama katika usafiri wa anga, kwa kuwa wahalifu wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali kila wakati.

Naye Kaimu Meneja wa Usalama wa TAA, Julius Misollow amesema washiriki wote wameiva kwa kutambua na kubaini mizigo na vifurushi vyenye utata na vyenye kutishia usalama wa usafiri wa anga nchini.

Missolow amesema wahitimu hao wataendelea na mafunzo ya ukufunzi, ambapo wakihitimu wataisaidia mamlaka kwa kutengeneza wataalam zaidi wa masuala ya usalama, ambao watapunguza gharama za kutumia wakufunzi kutoka nje ya nchi.

Naye mmoja wa wakufunzi hao Sunday Mweemba kutoka Zambia amesema washiriki wote wamepata mafunzo ya msingi kwa upana, ambapo yataisaidia nchi kufanya vizuri katika usalama wa  usafiri wa anga.

Washiriki wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo wakimsikiliza mgeni rasmi, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Viwango cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Vedastus Fabian (hayupo pichani) aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu, wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika jana kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo katika Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Mweemba amesema mafunzo haya yamekuwa yakitolewa nje ya nchi, lakini ameishukuru menejimenti ya TAA kwa kujitoa kwa hali na mali na kufanikisha kuwaleta wakufunzi hapa nchini ili wanausalama wengi zaidi waweze kushiriki, endapo yangeendeshwa nje ya nchi wangeshiriki wawili au mmoja.

Kwa upande wa wahitimu, Bw. Wenceslaus Sango ameishukuru menejimenti ya TAA kwa kufanikisha mafunzo hayo, wakufunzi na mratibu kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), Bw. Burhan Majaliwa, ambapo wameahidi kuyatumia vyema kwa faida ya taifa.

Washiriki walioshiriki na viwanja wanavyotoka kwenye mabano ni pamoja na Mohamed Makau (TAA Makao Makuu), Zalia Msangi na Stephen Magambo (Arusha); Philbert Lyimo, Ahmed Zomboko, Thawabu Njeni, Rehema Mlanzi, Nuhu Kisweswe, Martha Kilunga, 

Levina Valasa, Josephine Kahimba, Anna Myovela, Fatma Shomari na Stephen Ntambi (JNIA);.

Wengine ni   Felister Lutonja (Shinyanga) Mathias Gombo, Lilian Malero na Wenceslaus Sango (Mwanza)  na Bebedict Ole Laput (Songwe).

Mwanafunzi Auwa 10 kwa Risasi Marekani


TEXAS, Marekani
WATU 10 wameuawa huku wengine 10 wakijeruhiwa baada ya mwanafunzi mmoja kuvurumisha risasi katika shule ya sekondari ya Texas, gavana wa jimbo hilo amesema.;

Mshambuliaji huyo, ambaye alikamatwa na kushitakiwa kwa mauaji, alifahamika kwa jina la Dimitrios Pagourtzis, ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 katika Shule ya Santa Fe High School.

Alidaiwa kutumia binduki aina ya mashine gani ambayo aliichukua kutoka kwa baba yake, ambaye alikuwa akimiliki bundiki hiyo kihalali.
 
Wengi waliokufa katika tukio hilo ni wanafunzi, polisi ilisema katika tukio hilo.

Gavana wa Texas, Greg Abbott alisema "vimekuta katika shule hiyo aina tofauti tofauti ya vilipuzi, maili 40 (kilometa 65 kusini mwa Hoston.

Abbott alisema polisi ilikuta taarifa katika shajala ya mtuhumiwa huyo , komputa na simu ya mkononi akidai kuwa alipanga kufanya shambulizi hilo na baadae kujiua.

Gavana huyo alisema kuwa kijana huyo “alijisalimisha kwa sababu halikosa ujasili wa kujiua.”
 
Mkuu wa Polisi wa Santa Fe, Jeff Powell aliwataka wakazi wa eneo hilo kuwa makini na vitu vyovyote watakavyoviona nakuwataka kutoa taarifa polisi haraka. “Mshishike kitu chochote mtakachokiona.”

Ofisa polisi wa shule ya Santa Fe John Barnes ametajwa kuwa mmoja wa walioumia. Yuko katika hali mbaya na amefanyiwa upasuaji, kilieleza chombo kmoja cha habari mjini hapa.

Ajali ya Ndege Yaua 100 Cuba, Watatu Wanusurika


HAVANA, Cuba
ZAIDI ya watu 100 wamekufa baada ya ndege aina ya Boeing 737 kuanguka jirani na kiwanja kikubwa cha ndege cha Cuba mjini hapa, ikiwa ni ajali mbaya zaidi ya anga kuwahi kutokea katika miongo kadhaa.

Wanawake watatu waliokolewa wakiwa hai kutoka katika mabaki ya ndege hiyo, lakini wakiwa katika hali mbaya sana.

Ndege hiyo, ambayo inakaribia umri wa miaka 40 tangu itengenezwe, ilikuwa imepakia abiria 104 na wafanyakazi sita.

Mamlaka ya Cuba imeanzisha uchunguzi, huku ikitangaza siku mbili za maombolezo kutokana na ajali hiyo.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737-201 iliyokuwa ikifanya safari za ndani, ilianguka majira ya saa 10:08 jioni juzi, muda mfupi baada ya kupaa kutoka katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha José Martí  jijini Havana wakati ikienda kwenye Kiwanja cha Frank Pais huko Holguin, mashariki ya kisiwa hiki.
 
Wafanyakazi wote wa ndege hiyo walikuwa ni raia wa Mexico, huku abiria wengi wakiwa ni raia wa Cuba, huku miongoni mwao walikuwa abiria watano wakigeni.

"Kuna ajali mbaya ya anga imetokea. Habari hazifurahishi na inaelekea kuna idadi kubwa ya abiria wamekufa, “alisema Rais wa Cuba, Miguel Diaz-Canel alipotembelea eneo la tukio, ndege hiyo ilipoangukia.

Nini sababu za ajali?

Taarifa zilisema kuwa ni mapema mno kusema sababu za ajali hiyo, lakini mashuhuda waliokuwa chini walielezea kuwa waliiona ndege hiyo ikilipuka kabla ya kuanguka msituni jirani na kiwanja kikubwa cha ndege cha Havana.

"Niiona ndege hiti ikiruka, “alisema mfanyakazi mmoja wa duka kubwa Jose Luis aliliambia Shirika la Habari la AFP. “Mara, iligeuka, na kuanguka chini. Wote tulishangaa.”

"Tulisikia mlipuko na badae tuliona moshi mkubwa ukieenda juu, “alisem aGilberto Menendez, ambaye anaendesha mgahawa mmoja jirani na eneo lililotokea ajali hiyo.

Idara ya usafiri ya Mexico ilisema katika mtandao wake kuwa “wakati ikipaa (ndege hiyo) ilipata matatizo na kurudi chini.”

Kampuni ya Boeing ilisema kuwa iko tayari kupeleka timu ya mafundi Cuba kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina kujua tatizo lililoisibu ndege hiyo hadi kuanguka.

Watu Walionusurika

Waru wanne walinusurika katika jail hiyo lakini mmoja alikufa mara baada ya kufikishwa hospitalini, alisema mkurugenzi wa hospitali ya Calixto Garcia iliyopo Havana, Carlos Alberto Martinez.

Watui hao watatu walionusurika wote ni wanawake, kwa mujibu wa gazeti la Chama cha Kikomunisti  la Granma: mmoja akiwa na umri kati ya miaka 18 na 25, wakati mwingine mwenye umri wa miaka 13 wakati watatu ana miaka 39.

"Yuko hai lakini ameungua vibaya, “alisema ndugu ya mwanamke huyo katika hospitali hiyo.

Nchi zote, Argentina na Mexico zilithibitisha kuwa wananchi wa mataifa yao ni miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo.

Tunachijua Kuhusu Ndege
Ndege hiyo ilitolewa na kampuni ya Mexico ya Aerolines Damojh kwa shirika la ndege la serikali la Cuba la Cuban de Aviación.

Mamlaka ya Mexico ilisema kuwa ndege hiyo ilitengenezwa mwaka 1979 na ilikaguliwa Novemba mwaka jana. Mexico imesema kuwa imetupa wataalam wawili wa mabo ya anga kusaidia katika uchunguzi huo.

Aerolineas Damojh, ambayo pia inajulikana kama Global Air, ina ndege tatu ambazo zinafanya kazi.

Ajali Zingine za Ndege

Kwa mujibu wa tafiti, mwaka jana ndege ya biashara ambayo ilikuwa ikisafiri bila abiria, ilianguka. Lakini mwaka huu kumekuwa na ajali kibao mbaya za ndege.

Mwezi uliopita, ndege ya jeshi ilianguka na kuua zaidi ya watu 250. Februari , ndege ya Saratov Airlines ilianguka karibu na Moscow, iliua watu 71 mwezi Machi, ndege ya Marekani ya Bangla Airlines ilianguka Kathmandu, Nepal; iliua watu 51.

Ajali nyingine mbaya ya ndege ilitokea mwaka 1989, wakati ndege ya abiria  iliyotengenezwa nchini Urusi aina ya Ilyushin-62M ilianguka jirani na jiji la Havana na kuua abiria wote 126 waliouwemo ndani ya ndege hiyo na wengine 24 waliokuwa ardhini.

Thursday, 17 May 2018

Katibu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza Atembelea JNIA Dar Leo

Koplo Chesco Mbise akimwongoza mbwa anayeitwa Max-Z kuondoka mara baada ya zoezi la kuonesha namna anavyokamata dawa za kulevyia katika mizigo ya abiria kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo leo Katibu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza (hayupo pichani) alipotembelea na kuona zoezi hilo. Mbwa huyu ni kati ya wawili waliotolewa kwa msaada na serikali ya Marekani.
Askari Hadson Muhuma akiwa amemshika mbwa anayeitwa Nopi wakati akifanya zoezi la kutambua mizigo ya abiria yenye nyara za serikali zikiwemo pembe za Ndovu, lililofanyika leo kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), baada ya kutembelewa na Katibu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza (hayupo pichani).
  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (mwenye suti ya bluu kulia), leo akiteta jambo na Katibu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza, Bw. Matthew Rycroft mara baada ya kukamilika kwa zoezi la mbwa wa polisi kuonesha namna wanavyokamata dawa za kulevyia na nyara za serikali katika mizigo ya abiria kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
 Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (kulia) akiongea na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela baada ya zoezi la mbwa kuonesha namna wanavyobaini mizigo yenye nyara za serikali na dawa za kulevyia leo kiwanjani hapo.
 Katibu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza, Bw. Matthew Rycroft (wapili kushoto) akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wa pili kulia) wakimsikiliza Bw. Matt Jenkins (aliyekaa), ambaye ni Afisa wa UK Border Force wa Kitengo cha dawa za kulevyia katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). (Picha zote na Bahati Mollel wa TAA). 


Monday, 14 May 2018

Conte Akata Tamaa ya Ubingwa FA Cup


LONDON, England
KOCHA Antonio Conte anadai Chelsea haina nafasi ya kushinda fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United isipokuwa kama itajiimarisha haraka baada ya kuhoji uwezo wa wachezaji wake.

Kocha huyo Mhitalia alisema kikosi hicho kinatakiwa kuboreshwa baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Newcastle United Jumapili na kumaliza msimu vibaya na kushindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Kikosi cha Conte kilikuwa na nafasi ya kumaliza ligi juu ya nafasi ya tano, lakini sasa watacheza Ligi ya Ulaya, wana nafasi ya kutwaa taji wakati watakapocheza dhidi ya Man United kwenye Uwanja wa Wembley Mei 19.

Hilo linatarajia kuwa pambano la mwisho kwa Conte katika kikosi hicho cha Chelsea, ambacho kitacheza dhidi ya kocha wao wazamani Jose Mourinho, kocha huyo mwenye umri wa miaka 48  anajua kuwa klikosi chake kinahitaji kuinua kiwango chake katika idara zote ili kutwaa taji kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012.

"Tulitaka kumaliza msimu katika njia nzuri, lakini tungeweza kufanya vizuri zaidi ya hivi, “alisema.

"Kwa hilo, nimekuwa wa kwanza kujibu kuhusu mchezo mbovu. Newcastle walionesha mchezo mzuri na kupambana, na kama tutacheza kama hivi katika fainali ya Kombe la FA, basi kamwe hatutakuwa na nafasi.

"Tuna siku sita tu kubadili muelekeo wetu, na tunatakiwa kupambana kwasababu tunaweza kufanya vizuri zaidi.”

Amebakisha miezi 12 kabla ya kumalizika kwa mkataba wake wa sasa, na alipoulizwa kuhusu hatma yake, kocha huyo wazamani wa timu ya taifa ya Italia aliongeza: “Nina mkataba, na najituma na klabu inajua kila kitu.

"Mchezo wa Jumamosi ndio utakuwa wa mwisho? Hapana, sifikiri hivyo. Kitu muhimu ni klabu, na sio uvumi kuhusu mimi.”

Salah Aweka Rekodi ya Mabao Ligi Kuu England


LONDON, England
MOHAMED Salah ameweka rekodi mpya ya kufunga mabao katika Ligi Kuu baada ya kupachika mabao 32 katika mechi 38 alizocheza na kuuhakikishia Liverpool nafasi ya kurejea katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Brighton katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Anfield.

Ushindi huo kwa Liverpool unamaana kuwa haijalishi Chelsea imepata matokeo gani katika mchezo wake dhidi ya Newcastle United, lakini ilifungwa mabao 3-0 katika mchezo wake uliofanyika kwenye Uwanja wa St James's Park.

Chelsea hata kama ingeshinda bado isingeweza kumaliza katika nafasi ya nne, kwani Liverpool ilitakiwa kufungwa ndio Chelsea ifuzu kwa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao.
 
Liverpool imepania kutwaa taji la sita Ulaya wakati itakapokutana na Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Mei 26.

Lakini vijana wa Jurgen Klopp wanajua kuwa hata kama hawata twaa taji katika fainali hiyo huko Kiev, watarejea katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao baada ya kuisambaratisha Brighton ugenini katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya England.

"Sasa tuko katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao na nimepata tuzo pia, hivyo ninajivunia sana, “alisema Salah wakati akikabidhia tuzo ya kiatu cha dhahabu kwa ufungaji bora katika Ligi Kuu ya England.

Mabingwa wapya Manchester City imevunja rekodi ya ushindi, kupata pointi nyingi na mabao mengi msimu huu na kuwa timu ya kwanza ya Uingereza kufikia rekodi ya pointi 100 wakati Gabriel Jesus alipofunga bao la dakika za mwisho wakati wakiifunga Southampton 1-0.
Man City pia imeweka rekodi katika Ligi Kuu kwa kuwa na pointi nyingi dhidi ya timu inayofuatia ya Manchester United, ambayo ilishinda bao 1-0 dhidi ya Watford kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Swansea City Yashuka Daraja Baada Misimu Saba


LONDON, England
TIMU ya Swansea City imeteremka daraja baada ya misimu saba kucheza Ligi Kuu ya England, baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Stoke City, ambayo tayari ilishatangulia katika Ligi Daraja la Kwamza.

Swansea City imemaliza ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya klabu 20 ikiwa katika nafasi ya 18 baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 33 ikiwa pointi sawa na Stoke City iliyopo katika nafasi ya 19 huku West Bromwich Albion ikishika mkia ikiwa na pointi 31.

Klabu hiyo ya Welsh ilihitaji mabo 10 ili iweze kubadili matokeo na kuiporomosha Southampton, kitu ambacho haikutokea na kushangaza yenyewe ndio imeporomoka baada ya misimu saba ya kucheza ligi hiyo.

Lakini hadi mapumziko, Swansea City, ambayo haijashinda mchezo wowote ugenini katika mechi 13 zilizopita, iliongoza kwa bao la Msenegal Badou Ndiaye na baadae Peter Crouch. Xherdan Shaqiri walifunga kwa Stoke huku pia ikikosa penalti.

Kocha Mreno wa Swansea City, Carlos Carvalhal ana nafasi kubwa ya kuondoka katika klabu hiyo, miezi mitano tangu aanze kuifundisha.

"Jana nilizungumza na mmiliki, jana Jumatatu tulitarajia kuzungumza tena, “alisema.
"Mimi mwenyewe nitafikiria kuhusu Swansea na nitazungumza na famnilia yangu. Baada ya hapo nitatoa uamuzi sahihi kuhusu hatma yangu.

"Najua Ligi Daraja la Kwanza na tulifikia hatua ya mchujo mara mbili. Hiyo sio kawaida timu kucheza mchujo mara mbili mfululizo.”

Kocha wa Stoke City Paul Lambert naye pia muda wake wa kuifundisha timu hiyo haukutosha kubadili mambo baada ya kuanza kuifundisha timu hiyo Januari.
"Kuna mambo hayako vizuri, hilo halina wasiwasi, “alisema.

Simba Watua Bungeni, Wabunge Wapagawa


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana lilipuka kwa shangwe baada ya mabingwa wapya wa soka kutinga katika chombo hicho cha kutunga sheria nchini.

Shangwe hizo zililipuka baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga kutangaza kwamba timu hiyo imekuja bungeni  kutembelea, hali iliyofanya wabunge kushindwa kujizuia na kuinuka kwenye viti huku wakishangilia, wengi wao wakionesha vitabu vya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambavyo vilikuwa vya rangi nyekundu.

Hali hiyo ilitokea baada ya kipindi cha maswali na majibu na iliwachukua wabunge takriban dakika tatu kushindwa kuficha hisia zako na kushangilia na wengi wao wakisema ‘This is Simba’, msemo ambao umekuw ukisemwa na msemaji wa klabu hiyo, 

Haji Manara na sasa umekuwa maarufu zaidi kwa mashabiki wa timu hiyo.

Miongoni mwa wabunge walionogesha bunge ni Mbunge wa Lushoto, Shaaban Shekilindi (CCM) ambaye alionesha fulana jezi ya Simba iliyoandikwa ‘Simba Bingwa  2018-2019, huku akiizungusha na kuzidisha shangwe, huku Mbunge wa Mbozi, Pascal Haonga(Chadema) alionesha juu tai nyekundu.

Awali, akikaribisha timu hiyo, Giga alisema timu hiyo imekuja na viongozi 10 na wachezaji 48 na kuwataja viongozi hao kwa majina wakiwemo Salim Abdallah, Aden Rage, Mohamed Dewji, Idi Kajuna, Haji Manara, Richard, Kocha Pierre, Masoud Juma na mwisho akamtambilisha Emmanuel Okwi na kuufanya ukumbi wa bunge kulipuka ingawa wapo waliomkosoa kwa kutosimama kama wenzake walivyokuwa wakitambulishwa.
Okwi ndiye mfungaji bora hadi sasa wakati ligi hiyo ikielekea ukingoni.

Mara baada ya wachezaji hao kusimama Wabunge walianza kushangilia huku baadhi wakipiga makofi na viti kuonesha kufurahishwa na ujio wa timu hiyo ambapo Giga aliingilia “Waheshimiwa,Waheshimiwa Wabunge naomba tusikilizane naamini kabisa vifijo hivi vimesaidiwa na Wabunge ,mashabiki wa Yanga kwa vile ni waungwana”.

Kabla ya timu hiyo kutambulishwa, wabunge wakati wakiuliza maswali na mawaziri kujibu wengi walikuwa wakieleza furaha yao kwa timu hiyo kunyakua ubingwa.

TAA Yawapiga Msasa Wanausalama Wake



Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Joseph Nyehende (aliyesimama) akifungua kozi ya Usalama wa vifurushi na mizigo iliyoanza leo kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI). (kulia) ni Bw. Sunday Mweemba wa Zambia na (kushoto) ni Bw. Ernest Bongane wa Afrika Kusini, ambao ni wakufunzi. (Picha Zote na Bahati Mollel wa TAA).

 Na Bahati Mollel, TAA
WANAUSALAMA 18 kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wametakiwa kuzingatia mafunzo ya Usalama wa vifurushi na mizigo vinavyosafirishwa kwa ndege za mizigo, yaliyoanza leo kwenye ukumbi wa Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo kwenye jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI) Jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Joseph Nyahende, ambapo amesema kuwa, mafunzo hayo yatasaidia zaidi kuongeza uelewa wa vifurushi na mizigo hiyo inatakiwa kusafirishwa bila abiria kuambatana nao.
Mkufunzi Sunday Mweemba kutoka Zambia akieleza jambo baada ya kozi ya Usalama wa Vifurushi na Mizigo kufunguliwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Joseph Nyehende (katikati), kushoto ni mkufunzi mwingine Bw. Ernest Bongane wa Afrika ya Kusini. Kozi hiyo itamalizika Mei 18, 2018. 
“Tunania njema ya kuwatengeneza wanausalama wetu na hili darasa ni muhimu sana kwa ajili yenu, hivyo tunahitaji mjifunze kwa faida yenu binafsi, taasisi na taifa kwa ujumla, kwani hamtaweza kuruhusu vitu visivyostahili kupita, kwani mtakuwa sasa mmepata mafunzo ya kuvitambua,” alisema Bw. Nyahende.

Naye mmoja wa wakufunzi Bw. Sunday Mweemba kutoka Zambia ameishukuru Menejimenti ya TAA ya kuomba kozi hiyo kupitia taasisis ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), ambayo itawafanya wanausalama wake kutambua vitu vingi vinavyofanyika katika viwanja vingine Duniani.
 Kaimu Meneja wa Usalama wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Julius Misollow (aliyeipa kamera mgongo) akifafanua jambo mbele ya washiriki wa kozi ya mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo inayosafirishwa na ndege za mizigo iliyoanza leo kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo kwenye Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI). 
“Tumeona ni jinsi gani menejimenti yenu ilivyojitoa kwa ajili yenu, na hii inatolewa na ICAO na kupitia kazi yenu mnatakiwa kuwa makini zaidi na kuzijua sheria zote zinazohusika na mizigo, na tunamatumaini hadi mwisho mtakuwa mmeweza kujijengea uwezo,” alisema Bw. Mweemba.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Usalama wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Julius Misollow alisema mafunzo hayo ni ya kwanza, ambayo yanalengo la kuwajengea uwezo wanausalama kukagua vifurushi na mizigo inayosafirishwa yenyewe bila abiria kwa kutumia ndege za mizigo.
Mkufunzi Bw. Ernest Bongane wa Afrika ya Kusini akisalimiana na washiriki wa kozi ya usalama wa vifurushi na mizigo inayosafirishwa na ndege za mizigo iliyoanza leo kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI). 
“Magaidi wamekuwa wakitumia njia mbalimbali na wengine wanatumia mizigo au vifurushi kufanya hujuma, hivyo tunaimani kwa mafunzo haya tutawajengea uwezo wa kutambua mizigo, ambayo ni hatarishi, ingawa kwa Tanzania haijawahi kutokea tatizo hilo,” alisema Bw. Misollow.

Hata hivyo, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mitihani na watakaofaulu kwa alama 70 wataendelea na kozi ya ukufunzi, ambayo itaanza baadaye kuanzia Mei 19, 2018.
Washiriki, Wakufunzi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Joseph Nyahende (wa pili kushoto waliokaa) wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya usalama wa vifurushi na mizigo inayosafiri kwa ndege za mizigo iliyoanza leo kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kilichopo kwenye jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI). 
Washiriki wanaoshiriki na viwanja wanavyotoka ni pamoja na Philbert Lyimo, Ahmed Zomboko, Thawabu Njeni, Rehema Mlanzi, Nuhu Kisweswe, Martha Kilunga, Levina Valasa, Josephine Kahimba, Anna Myovela, Fatma Shomari na Stephen Ntambi (JNIA); Zalia Msangi na Stephen Magambo (Arusha).

Wengine ni   Mathias Gombo, Lilian Malero na Wenceslaus Sango (Mwanza); Bebedict Ole Laput (Songwe); na Felister Lutonja (Shinyanga).