Tuesday, 13 February 2018

Real Madrid Uso kwa Uso na PSG Mabingwa Ulaya


MADRID, Hispania
MABINGWA wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Real Madrid wamekamilisha kipindi chao cha mazoezi na leo watacheza dhidi ya Paris Saint Germain (PSG) katika mchezo wa kwanza.

Mchezo huo ni muhimu sana kwa Real Madrid kwani utaonesha mwelekeo wa mabingwa hao watetezi kama wataendelea kuwepo katika mashindano hayo au watatupwa nje.

Tayari Madrid ina rekodi ya mashindano hayo, ambapo mbali nakutwaa mara nyingi taji hilo zaidi ya timu nyingine, lakini pia timu hiyo ndio pekee iliyowahi kulitwaa taji hilo mara mbili mfululizo.

Nahodha wa Real Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Sergio Ramos amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi leo kuishangilia timu hiyo.

Ramos aliandika kupitia katika mitandao ya kijamii akiwataka mashabiki hao kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu hiyo itkapocheza dhidi ya Paris Saint Germain.

Naye kipa wa timu hiyo, Keylor Navas alisema kuwa PSG ni timu kubwa, lakini wanaamini katika kiwango chao.

“PSG ni timu kubwa, lakini sisi tunaamini katika kiwango chetu, “alisema Navas.
"Najisikia vizuri na ni jambo zuri sana. Msimu huu tulikuwa na baadhi ya mambo mazuri na baadhi sio mazuri. Hiyo ni sehemu ya soka.”

Alisema kuwa kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ni ndoto ya kila mchezaji hapa. Kushinda taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ni kitu fulani kizuri, ni faida kutwaa taji.

Katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya leo, Porto ya Ureno itaikaribisha Liverpool katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Dragão.

Sharapova Atolewa Raundi ya Kwanza Qatar Open


DOHA, Qatar
MARIA Sharapova amejikuta akitolewa katika raundi ya kwanza ya mashindano ya Qatar Open baada ya kufungwa na Mromania Monica Niculescu hapa.

Mrusi Sharapova, mwenye umri wa mika 30, alitolewa katika mashindano hayo baada ya kufungwa 4-6 6-4 6-3 katika mchezo uliodumu kwa saa mbili na dakika 38 na mchezaji anayeshikilia nafasi ya 92 kwa ubora duniani.

Sharapova, ambaye ni bingwa namba moja wazamani, alipambana kutaka kufanya vizuri, lakini alijikuta akifanya kizembe makosa 52 katika mchezo wote.

Kwa ushindi huo, Niculescu sasa katika raundi ijayo, atachesa ama na Magdalena Rybarikova au Fatma Al Nabhani ambaye hayumo katika orodha ya ubora duniani.

Sharapova, yuko katika nafasi ya 41 ya viwango vya ubora duniani, alikuwa akicheza kwa mara ya kwanza baada ya kutofuzu mashindano hayo ya Qatar tangu mwaka 2013.

Baada ya kupata seti ya kwanza katika nafasi ya nne, Sharapova alijikuta akizidiwa ujanja na Niculescu, na kupoteza mwelekeo wakati Mromania huyo akiendelea kufanya vizuri katika mchezo huo.

Muingereza Johanna Konta jana alitarajia kucheza raundi ya kwanza dhidi ya Mmarekani Bernarda Pera, ambaye alimshinda katika mashindano ya Australian Open Januari.

Conte Awapongeza Mashabiki Chelsea ikishinda 3-0


LONDON, England
KOCHA wa Chelsea Antonio Conte amewapongeza mashabiki wa klabu hiyo kwa kumuunga mkono, baadaya ushindi mnono dhidi ya West Bromwich Albion katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Stamford Bridge na kuounguza presha kwa Muitalia huyo.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya England, Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wa England, waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Hatma ya Conte katika klabu hiyo ya Chelsea iko katika wakati mgumu baada ya timu hiyo kutofanya vizuri msimu huu.

Chelsea ilipokea vipigo vizuri mfululizo kutoka kwa Bournemouth na Watford, lakini ushindi huo wa juzi katika Ligi Kuu kumeirejesha timu hiyo katika mstari wa ushindi.

Jina la Conte lilikuwa likitajwa katika nyimo za mashaiki hao waliokuwa kwenye uwanja wa nyumani, ikiwa ni wazi ilionesha kumuunga mkono kocha huyo.

"nawashuuru mashabiki kwa sababu wameniunga mkono kwa kiasi kikubwa sana, “alisema kocha huyo. “Pamoja na uvumi na tetesi kwangu nina furaha kubwa.”

"Ina maana wamenielewa, nia yangu ya kutetea jezi ya klabu hii na nembo ya klabu hii.”

"Natakiwa kuishi na presha hii hadi mwisho wa msimu. Sitaki shinikizo hili kukaa mabegani mwa wachezaji.”

Ushindi huo umeifanya Chelese au the Blues pointi moja mbele ya Tottenham iliyopo katika nafasi ya tano.

Wakati huohuo, West Brom wako pointi saba kutoka katika ukanda salama katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kushinda mchezo mmoja katika mechi 25 walizocheza.

Monday, 12 February 2018

Zuma Apewa Saa 48 Kuachia Ngazi Urais

Rais Jacob Zuma

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
RAIS wa Afrika Kusini Jacob Zuma amepewa saa 48 kujiuzulu mara moja nafasi yake hiyo ya uongozi, imeelezwa.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari likiwemo Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo ya zaidi ya saa 10 yaliyofanywa na chama tawala cha African National Congress (ANC) katika mkutano wa dharura mapema leo Jumatatu.

Vyanzo hivyo vya habari vinasema kuwa, kikao hicho kiliwaagiza watu wawili akiwemo Rais wa sasa wa ANC, Cyril Ramaphosa kwenda kumuona uso kwa uso Zuma na kumueleza maamuzi ya kikao hicho ya kumtaka kuachia ngazi ndani ya saa 48.

Inaelezwa kuwa Zuma ametakiwa kujiuzulu la sivyo chama hichi kitamtoa madarakani mara moja.

Hatua hii ya ANC inaonekana ndio njia rahisi zaidi ya chama hicho kumshinikiza rais Zuma kuondoka madarakani badala ya kusubiri utaratibu wa Bunge ambao ungeweza kuwa mrefu na wenye madhara zaidi kwa ANC.
Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa

Rais Jacob Zuma ambaye anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya rushwa, alishindwa uongozi wa chama tawala Desemba mwaka jana.

Rais mpya wa ANC, Ramaphosa ndiye anayeongoza shinikizo za kumuondoa Zuma katika nafasi yake hiyo ya Urais, na hatimaye kushika nafasi hiyo.

Ramaphosa ameahidi pia kupambana na rushwa iliyokithiri na kukijenga upya chama, wakati nchi hiyo ikielekea katika Uchaguzi Mkuu mwakani.

JNIA kuingizia TAA Sh milioni 253 kwa mwaka

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (kulia) akipokea taarifa ya mchakato wa vyanzo vya mapato katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), leo katika Jengo la kufikia na kuondokea abiria mashuhuri (VIP) Terminal Two kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Profesa Ninatubu Lema.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) itaongeza pato lake kwa kiasi cha Sh milioni 253 kwa mwaka kutokana na ungezeko la tozo la pango la ardhi watakalotozwa wapangaji katika Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TAA, Mhandisi Profesa Ninatubu Lema wakati akisoma taarifa ya wataalam kuhusu mchakato wa vyanzo vya mapato katika  Kiwanja cha JNIA kwa Waziri wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Makame Mbarawa.
Mhandisi Profesa Ninatubu Lema akisoma taarifa yake leo mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa. 
Profesa Lema alisema kuwa ongezeko hilo la fedha ni sawa na asilimia 35 mara baada ya kuanza kwa utekelezaji wa yalioyoridhiwa katika majadiliano ya mikataba husika.

Alisema kuwa mikataba karibu yote ya TAA imetoa mwanya wa kurejea tozo ya ardhi nay a tahafifi (review of land lease and concession rates) kila baada ya miaka miwili, zoezi la majadiliano na watoa huduma litakuwa endelevu na litakapofanyika litahusisha wataalam kutoka taasisi nyingione, pale panapohitajika, kama ilivyofanyika mwaka huu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (kulia) akizungumza leo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela.
Taarifa hiyo ilihusu majadiliano yaliyofanyika na watoa huduma/wafanyabiashara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere yamevaa matunda baada ya baadhi ya maeneo kukubalika, ambayo ni pamoja na ongezeko la tozo ya pango la ardhi (toka dola za Marekani 5.00 hadi 7.90) na riba ya ucheleweshaji malipo ambayo ni asilimia moja.

Profesa aliongeza kusema kuwa timu hiyo ya wataalam pia ilipendekeza tozo ya tahafifu kuwa kati ya asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mwaka.
Mbarawa aliipongeza timu hiyo ya wataalam kwa kazi waliyofanya, lakini alisisitiza kuwa wapangaji wa kiwanja hicho wasinyanyashwe na wale watakaozembea kulipa pango wasionewe huruma.

Alisema ni aibu kwa taasisi yenye uwezo wa kujiendesha kwa kutumia vyanzo vyake, kupiga hodi serikali na kuomba omba fedha kila siku.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kukabidhi taarifa ya wataalamu kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (kushoto)..
Wakati huohuo, Serikali imesema  mchakato wa uboreshaji wa Shirika la ndege la Tanzania(ATCL) unaoendana  na ununuzi wa ndege mpya unaoendelea kufanywa na Serikali hivi sasa, umelenga kuliboresha shirika hilo kwa lengo la kulikuza kibiashara ndani na nje ya Tanzania na hivyo kuliingizia fedha na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo leo baada ya kutembelea ujenzi wa sehemu ya tatu ya jengo la abiria la JNIA (Terminal 3) unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Bam International ya Uholanzi, ambao umekamilika kwa takeibani asilimia 68.5 na unatarajia kukamilika Septemba mwaka huu.

Sunday, 11 February 2018

Simba Yahamishia Makali ya Ligi Kuu Kimataifa


Na Mwandishi Wetu
SIMBA imeendekeza makali yake ya katika Ligi Kuu hadi katika mashindano ya kimataifa baada ya kuichalaza Gendarmerie mabao 4-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.


Wawakilishi hao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho walianza kuhesabu mabao dakika ya kwanza ya mchezo huo baada ya Said Ndemla kufunga kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja kutikisa nyavu.

Nahodha wa Simba, John Bocco alifunga mabao mawili katika mechi hiyo, dakika ya 32 alilolifunga baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Gendarmerie na dakika ya 45 alipofunga bao la kichwa akiunganisha krosi ya Emmanuel Okwi.

Simba ilitawala katika kila idara kwenye kipindi cha kwanza, lakini hali ilibadilika kwenye kipindi cha pili baada ya wapinzani wao kuonekana kujizatiti zaidi.

Pengine baada ya kujiuliza na kujirekebisha, dakika ya 90, Okwi aliandika bao la nne kwa Simba kwa mpira wa adhabu ulioanzishwa na Erasto Nyoni kabla ya ‘Mhenga’ huyo kuuwahi na kuujaza wavuni.

Shujaa mwingine katika mechi ya jana alikuwa kipa wa Simba, Aishi Manula aliyeoangua penalti katika dakika ya 50.

Penalti hiyo iliyopigwa na Abdorahim Mohammed ilitolewa na mwamuzi baada ya James Kotei wa Simba kumchezea rafu Ahamed Aden wa Gendarmerie.

Matokeo hayo yanaiweka Simba nafasi nzuri ya kusonga mbele kwani sasa wapinzani wake watalazimika kushinda 5-0 katika mechi ya marudiano ili wasonge mbele.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamefurahia matokeo hayo na sasa wanaiandaa na mechi za Ligi Kuu kwani lengo lao ni kufanya vizuri.

Simba endapo itavuka raundi hii, raundi inayofuata huenda ikakabiliana na kibarua kigumu kutoka ama timu ya Misri au kwingineko kwenye soka kubwa zaidi.

Watakaopisha Upanuzi JNIA kufidiwa Viwanja, Fedha

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia) kabla ya kukutana na wakazi wa Kipinguni kwenye Kiwana cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal One kuhusu fidia ya wakazi hao kupisha upanuzi wa kiwanja cha ndege. Kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala (DAS), Edward Mpogolo. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Segerea, Mona Kalua na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

 
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesisisitiza kuwa wananchi wa Kipunguni A na Kipunguni Mashariki, ambao wanatakiwa kuondoka katika maeneo hayo ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), watapatiwa viwanja mahali pengine pamoja na kulipwa fedha, imesisitizwa.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye alipozungumza na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa JNIA Terminal  I kuhusu upanuzi wa kiwanja hicho.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alipozungumza na wakazi wa Kipunguni.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe Magufuli kamwe haina nia ya kuwaumiza wananchi, ambapo watu wenye nyumba maeneo hayo watapatiwa viwanja katika maeneo ya Msongola na kupewa fidia ya fedha.

Alisema kuwa siku zote Serikali ya Magufuli inataka kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake anayostahili na sio kumuumiza.
Baadhi ya wakazi wa Kipinguni A na Kipunguni Mashariki wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Atashasta Nditiye alipozungumza nao kuhusu fidia watakapopisha upanuzi wa kiwanja cha ndege.
Alisema kuwa jumla ya wananchi 801 walitakiwa kupewa viwanja na tayari Kampuni ya Tanzania Remix ilishaandaa viwanja 537 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ugawaji viwanja hivyo.

Zoezi hilo kwa miaka mingi lilishindwa kufanyika licha ya Serikali kufanya tathmini, na sasa litafanikiwa baada ya wananchi kurudhika na maelezo ya Nditiye baada ya kusema kuwa hata wale ambao hawakufanyiwa tahmini wakati ule, alimuagiza Naibu Mkurugenzi Mkuu kuhakikisha wanafanyiwa tathmini ili nao wapatiwe viwanja na fedha wanazostahili.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye akizungumza na wakazi wa Kipunguni A na Mashariki kuhusu fidia watakapopisha upanuzi wa kiwanja wa cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere. Kulia ni Katibu Tawala wa Ilala, Edward Mpogolo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela. 
Alisema tathmini ya awali ilifanyika mwaka 2013 na kusema kuwa wale watakaovunjiwa nyumba zao watapatiwa viwanja na watafidiwa fedha.

Aidha, Naibu waziri alisema wote waliopewa viwanja baada ya kuvunjiwa Kigilagila, ambao hawakuwa wakazi wa eneo hilo na Kipawa, watanyang’anywa viwanja hivyo na kuchukulia hatua za kisheria.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala (DAS), Edward Mpogolo akizungumza wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alipozungumza na wakazi wa Kipinguni A na Mashariki kwenye kiwanja wa ndege cha JNIA. 
Alisema hata kama watakuwa wamejnga nyuma, lakini wakabainika kuwa walipewa viwanja wakati hawakuwa wakazi wa maeneo hayo, watapokonywa mara moja na kuchukuliwa hatua.

Alisema kuwa baada ya tahthmini kufanyika muda mrefu, wananchi hao wataongezewa asimilia ya fedha za awali kulingana na miaka iliyopo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela alisema kuwa maelekezo yaliyolewa na Naibu waziri atayafanyia kazi na ataunda tume kama alivyoagizwa ili kuhakikisha utekezaji unafanyika kwa ufanisi.

Mayongela alisema kuwa yeye kama mtendaji atahakikisha matatizo yote yaliyojitokexa na tayari mchakato wa kushughulikia tatizo hilo ulianza muda mrefu na ameanza kufanikiwa.
Alimtaka Mbunge wa Segerea, Mona Karia kumuagiza kaimu mkurugenzi huyo mkuu wa TAA kazi yoyote nay eye yuko tayari kuitekeleza ili kuhakikisha wanamaliza matatizo yote.

Alisema tayari viwanja 537 vyenye thamani ya Sh bilioni 3.7 vilishakbidhiwa kwa TAA mwezi uliopita pamoja na kuchelewa,  lakini wameshapata viwanja 700 lakini wanatakiwa kwenda kuvihakiki kama kweli vipo kwa ajili ya kuwapatia wahusika.
Alisema  kuwa tayari wananchi 57 kati ya 59 walishabomoa nujmba zao hadi mwezi uliopita na wamebaki wawili,ambao anategemea nao wakati wowote watavunja nyumba zao na kuondoka eneo hilo.

Alisema wiki hii ataunda kikosi kazi ambacho kitachunguza wale aliopewa viwanja wakati hawakuwa wakazi wa maeneo hayo, ambapo kwa kushirikiana na vyombo vvya dola mkondo wa sharia utachukua nafasi yake.




Saturday, 10 February 2018

Mourinho alia Sanchez kuchezewa rafu mbaya


MANCHESTER, England
KOCHA wa Manchester United Jose Mourinho anaamini kuwa anatakiwa kupiga kelele zaidi ili kuwalinda wachezaji wake.

Mourinho hakuwa na furaha kutokana na jinsi Alexis Sanchez alivyopchezewa rafu katika mchezo wa wiki iliyopita uliofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford wakati timu hiyo ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Huddersfield Town.

Kocha wa Man City Guardiola alirudia kilio chake kutaka wachezaji walindwe zaidi kufutia kuchezewa vibaya mchezaji wake Leroy Sane na mchezaji wa Cardiff, Joe Bennett na kumfanya mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani kuwa nje kwa wiki sita baada ya kuumia kifundo cha mguu.

“Labda kocha wake anataka kulia zaidi, “alisema Mourinho kwa adhabu aliyopewa Sanchez.

Leo Jumapili, Manchester United itakuwa mgeni wa Newcastle United katika mchezo wa Ligi Kuu ya England utakaofanyika kwenye Uwanja wa St  James' Park.



Aguero Atupia Nne City Ikishinda, Arsenal Hoi


LONDON, England
SERGIO Aguero amefunga mabao manne wakati Manchester City ikiendeleza ubabe wake katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu ya England na kufikisha pointi 16 zaidi, huku Harry Kane akifunga wakati Tottenham Hotspur ikiwachapa wapinzani wao wakubwa Arsenal kwa bao 1-0 jana.

Manchester City iliibuka na ushndi mnono wa mabao 5-1 katika mchezo huo uliotawaliwa na washindi.

Baada ya kuanza taratibu kipindi cha kwanza katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Wembley, Kane aliruka juu na kuifungia kwa kichwa timu yake akifunga kwa mara ya saba katika mchezo wa saba wa wapinzani hao huku likiwa goli lake la 23 katika ligi hiyo msimu huu.

Spurs, ambayo katika mchezo huo ungeweza kushinda mabao mengi kama ingekuwa makini, lakini umahiri wa kipa wa Arsenal Petr Cech, ndio ulizuia timu hiyo kupata mabao zaidi.

Kwa ushindi huo, Spurs sasa imepanda hadi katika nafasi ya tatu wakati Arsenal iko pointi sita tofauti na Liverpool katika nmafasi ya nne huku kikosi cha kocha Jurgen Klopp kikiwa na mchezo mkononi.

Kwenye Uwanja wa Etihad, Aguero na mkali Kevin De Bruyne, ambaye alisaidia mara tatu, waling’arawakati Man City ikitoa kipigo kwa mabingwa wazamani wa England Leicester katika kipindi cha pili na kuiwezesha timu hiyo kupata ushindi wa 23 katika ligi kati ya 27 msimu huu.

"Nafikiri tulicheza vizuri leo, vijana wamefanya vizuri sana na hasa Sergio Aguero alikuwa mchezaji tofauti kabisa, “alisema Raheem Sterling, ambaye alifunga bao la kwanza la Man City, alipozungumza baada ya mchezo huo.

AGUERO AISIYEZUILIKA

 Baada ya Sterling na Jamie Vardy walipofunga mabao katika kipindi cha kwanza kwa kila upande, Aguero alitawala ufungaji baada ya kutupia mabao mawili ndani ya kipindi cha dakika nane  baada ya mapumziko.

Mshambuliaji huyo alikamilisha hat-trick yake kabla ya kufunga la nne, baada ya kupiga mpira uliogonga mwamba na kutinga wavuni.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 tayari ameshafikisha mabao 21 ya ligi msimu huu na kuwa mchezaji wanne kufunga zaidi ya mabao 20 katika misimu minne ya ligi mfululizo.

Friday, 9 February 2018

Leicester kuikabili Manchester City bila Mahrez


MANCHESTER, England
KOCHA Claude Puel ana tumaini winga mahiri wa Leicester Riyad Mahrez atajisikia fahari kurejea katika kikosi chake.

Mahrez ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Algeria, mwenye umri wa miaka 26, hajaichezea timu hiyo tangu Januari wakati uhamisho wake kwenda Man City uliposhindikana.

Mchezaji huyo bora wa kulipwa wa mwaka 2016 aliwasilisha ombo lake la uhamisho, na Alhamisi kocha wa Mbweha hao Puel alithibitisha kuwa hatampanga katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu dhidi ya vinara City.

"Nafikiri ni muhimu sana sasa kuangalia mbele, “alisema Mfaransa Puel.

"Riyad ni mchezaji muhimu na anapenda soka. Anapenda uhusiano mzuri na marafiki zake. Ana uhusiano mzuri na wachezaji wenzake, “aliongeza.

"nafikiri ni muhimu katika kipindi hiki kigumu kuwaweka wachezaji wote na klabu pamoja ili kuendelea na kazi ngumu uwanjai. Njia bora ni kurudi nyuma na kufurahia soka.”

Mahrez alijiunga na Leicester akitokea klabu ya Ufaransa ya Le Havre kwa ada ya pauni milioni 400,00 Januari mwaka 2014.

Alifunga mabao 35 na kusaidia kupatikana kwa mengine 24 katika mechi 127 alizocheza katika Ligi Kuu, na alitangazwa kuwa mchezaji bora wakati Mbweha ho walipotangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu 2016.


Tenga mwenyekiti mpya BMT, Ikangaa mjumbe

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk  Harrison Mwakyembe amemteua Rais wazamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodger Tenga kuwa mwenyekiti mpya wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Lorietha Laurence, Dk Mwakyembe amemteua Tenga na wajumbe wengine kwa mujibu wa Sheria ya BMT ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake.

Dk Yusuph Singo.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo imesema kuwa Waziri amewateua wajumbe sita wa baraza hilo, ambao ni Profesa Mkumbwa Mtambo, Beatrice Singano, Kanali Mstaafu Juma Ikangaa, John Joseph Ndumbaro, Rehema Madenge na  Salmin Kaniki.

Pia, Dk Mwakyembe amewateua wajumbe wengine watatu Baraza kutokana na nafasi za vyeo vyao ambao ni:

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Yusuph Singo,  Dk Edicome Shirima- Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu,Sayansi,Teknolojia  na Mafunzo ya Ufundi.

Mwingine aliyeteuliwa na Mwakyembe ni Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo ulianza tangu juzi Februari 8 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja.
Aidha, Dk  Mwakyembe kwa mujibu wa sheria amemteua Timothy Mganga kuwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Kanali Mstaafu Juma Ikangaa.

Friday, 2 February 2018

Wagosi Coastal, KMC Kucheza Ligi Kuu Bara

Wachezaji wa Coastal Union wakishangilia bao la kwanza walipocheza dhidi ya Mawezi katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza leo kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Coastal ilishinda 2-0.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
TIMU za Coastal Union ya Tanga na KMC ya Kinondoni jijini Dar es Salaam leo zimekata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao kutoka katika Kundi B baada ya kushinda mechi zao za mwisho.

Coastal Union imerejea katika ligi hiyo baada ya kuifunga Mawenzi 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa, huku KMC iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Mlale kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Kwa matokeo hayo, KMC inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi 28 ikifuatiwa na Coastal Union yenye alama 26, huku JKT Mlale wakibaki na pointi zao 25 na Polisi Dar es Salaam wameshuka daraja baada ya kumaliza wakiwa na pointi tano tu.

Katika mchezo huo, Coastal Union waliandika bao la kwanza katika dakika ya 24 lililofungwa kwa penalti na Raizin Hafidh baada ya kuchezewa rafu.

Hatahivyo, mashabiki wa Mawenzi waliwarushia mawe wachezaji wa Coastal Union wakati wakishangilia bao hilo na kuzua mtafaruku.

Ulinzi uliimarishwa baada ya vurugu hizo kufuatia kuongezwa kwa askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia, FFU.

Ukongwe wa Athuman Idd Chuji pamoja na kipa Hussein Sharifu au Cassilas waliibeba timu yao kutokana na uzoefu wao.

Dakika  ya 72 ya mchezo huo, Chuji aliipatia Coastal Union bao la pili lililoihakikishia ushindi timu hiyo na kuondoka na pointi tatu muhimu.

Chuji alifunga bao hilo baada ya kucheza kwa utulivu zaidi baada ya kupata mpira uliopigwa na Andrew Simchimbi na kuokolewa na mabeki wa Mawenzi na kumkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.

Mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakimshangilia Chuji kwa kumuita `Babu, Babu, Babu’.

Katika matokeo mengine ya kundi hilo, Polisi Tanzania ilibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mufundi huku Mbeya Kwanza wakiibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Polisi Dar es Salaam.


Timu hizo mbili zinaungana na JKT Tanzania iliyokuwa ya kwanza kupanda daraja kutoka katika Kundi A huku mechi za kundi hilo zikitarajia kumalizika Jumatatu huku zile za Kundi C zitaisha keshokutwa Jumapili.

TAA Yaikabidhi Zimamoto JNIA Gari Toyota Hilux

*Pia Yaahidi Kuipatia Sh milioni 120 Kwa Ajili ya Mafunzo
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela (kushoto) akimkabidhi funguo ya gari , Kamishna Generali wa Idara ya Zimamoto  na Ukoaji nchini, Thobias Andengenye katika hafla iliyofanyika leo kwenye Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imekabidhi gari kwa Idara ya Zimamoto ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ili kuboresha utendaji kazi.

Akikabidhi gari hilo katika hafla fupi iliyofanyika leo katika Idara ya Zimamoto kiwanjani hapo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela alisema gari hilo litasaidia usafiri kwa mkuu wa idara hiyo kiwanjani hapo Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa.
Mayongela alisema kuwa gari hilo aina ya Toyota Hilux lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 80, mbali na kusaidia usafiri kwa bosi huyo wa Zimamoto, pia litasaidia kwa shughuli zingine.

Alisema Zimamoto ni miongoni mwa wadau wakubwa wa TAA, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanawezeshwa kutekeleza shughuli zao bila matatizo yoyote.

Mbali na kutoa gari hilo lenye namba za usajili STL 5570,pia TAA imesema kuwa itaipatia Zimamoto kiasi cha Sh milioni 120 kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa idara hiyo ya Zimamoto katika viwanja vya ndege.

Bosi huyo wa TAA alisema kuwa, mafunzo kwa Zimamoto ni muhimu sana, kwani wanahitaji kwenda na wakati na kujifunza mambo mapya, kwani wengi wao kwa muda mrefu hawajapata mafunzo yoyote.
Alisema TAA itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na idara hiyo ya Zimamoto, ambao ni miongoni mwa wadau wakubwa wa viwanja vya mdege.

Naye Thobias Andengenye, ambaye ni Kamishna Generali wa Zimamoto na Ukoaji nchini, baada ya kupokea gari hilo, aliishukuru TAA kwa msaada huo na kusema utasaidia sana.

Alisema viwanja vya ndege ndio lango kuu la kuingilia wawekezaji na watalii, hivyo usalama ni jambo muhimu sana.

Alisema bila usalama wawekezaji hao na watalii wataogopa au kushindwa kuingia nchini kuwekeza na kufanya utalii.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kukabidhi gari kwa Idara ya Zimamoto ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA)
Hafla hiyo iliyofanyika katika eneo la idara hiyo katika kiwanja cha JNIA na kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa TAA pamoja na JNIA na wale wa Zimamoto.

Alisema gari alilokuwa akilitumia bosi huyo wa Zimamoto Jnia ni chakavu, hivyo hilo walilopewa litasaidia kufanikisha shughuli mbalimbali.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, Thobias Andengenye akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kupokea gari lililotolewa na TAA jijini Dar es Salaam.