Saturday 18 March 2017

Waziri Nape ataka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuba) iungwe mkono


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (wa pili kushoto) akiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma ya Jamii ilipotembelea Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo au TaSuba jana.
 Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema  Chuo cha Sanaa Bagamoyo kinatakiwa kuungwa mkono kutokana  na mchango wake nchini.

Nape aliyasema hayo jana wakati wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii walipofanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Chuo hicho, ambacho sasa kinatambulika kama Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuba).

"TaSuBa imekuwa ikifanya kazi kubwa katika Sanaa na Utamaduni, chuo hiki ni zao lililowaibua wasanii wengi maarufu nchini akiwamo Mrisho Mpoto.

"Ni wakati sasa wa kukiboresha zaidi na bahati nzuri kimeanza kushirikiana na Veta ili waweze kutoa elimu ya Sanaa na Utamaduni kuanzia ngazi za Wilaya nchi nzima," alisema Nape.

Mkuu wa Chuo hicho, Albert Makoye alisema Chuo licha ya kuwa msingi wa kutoa elimu ya Sanaa na Utamaduni nchini, lakini kimekuwa na changamoto ikiwamo ya vifaa na ukarabati wa majengo.

Huku akionesha baadhi ya maeneo yanayopaswa kuboreshwa, Makoye alisema, licha ya changamoto hizo lakini Chuo kimekuwa kikipokea wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi.

"Achilia mbali wanafunzi wa hapa nchini, kuna kundi la Sanaa la Vitimbi kutoka Kenya limeomba kuleta wasanii wao kujifunza chuoni hapa," alisema Mkuu huyo wa TaSuBa.
 
Katika ukaguzi wa miradid ya Chuo hicho, Waziri Nape na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii walitembelea majengo ya mafunzo mbalimbali ya Chuo hicho sanjari na kucheza ngoma ya asili na walimu wa chuo hicho ya Paukwa Pakawa.
 



No comments:

Post a Comment