Saturday, 18 March 2017

mafunzo ya walimu wa walimu wa mchezo wa riadha kwa watoto wadogo yaanza uwanja wa taifa leo


Makamu wa Kwanza wa Rais Utawala wa Riadha Tanzania (RT), William Kalaghe akifungua mafunzo ya siku mbili ya walimu wa mchezo huo watakaowafundisha makocha wa riadha katika shule za msingi nchini.
Na Mwandishi Wetu
WASHIRIKI wa mafunzo ya riadha kwa watoto wametakiwa kupokea kwa makini mafunzo hayo ili nao wakawafundishe walimu wa shule za msingi ili kuwa na msingi imara wa mchezo huo na kuiwezesha Tanzania kupata wanariadha bora kama huko nyuma.

Hayo yalisemwa jana na Makamu wa Kwanza wa Rais Utawala wa Riadha Tanzania (RT), William Kalaghe wakati akifungua mafunzo hayo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mkufunzi wa mafunzo ya walimu wa walimu watakaofundisha wanafunzi wa shule za msingi nchini katika mchezo wa riadha, Dk. Hamad Ndee.
 
Kalaghe alisema kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwao, kwani wataweza kuwafundisha walimu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kuuendeleza mchezo huo.

Alisema bila kuwa na msingi imara kamwe Tanzania haitaweza kurejea katika mafanikio ya mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wanariadha wake walipofanya vizuri.

Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kupokea kwa makini, kwani huo ndio msingi imara wa Tanzania kufanya vizuri katika mchezo huo.
 
Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Dk Hamad Ndee alisema kuwa hakuna msingi imara katika mchezo fulani bila kufundisha watoto wadogo.

Alisema hata akina Usain Bolt walianzia utotoni na kutokana na msingi imara walioupata, sasa wanatamba duniani kwa kufanya vizuri katika mchezo huo.

Mmoja wa washiriki wa mchezo hyo kutoka mkoani Mbeya, Lwiza John alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuwafudisha walimu wa watoto wadogo katika mikoa watokayo.
John ambaye pia ni mmoja wa makocha wa timu ya taifa yam bio za nyika ya Tanzania inayojiandaa kwa mashindano ya dunia wiki ijayo nchini Uganda alisema mafanikio ya kila mchezo yanaanzia chini kabisa.

Jumla ya washiriki 29 wanashiriki katika mafunzo hayo kutoka mikoa mbalimbali huku sita wakitoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yatafungwa leo na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza mkufunzi Dk. Hamad Ndee leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment