Thursday, 9 March 2017

Senegal yaifuata Zambia fainali Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20LUSAKA, Zambia
SENEGAL itakutana na wenyeji Zambia katika fainali ya mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 Jumapili baada ya kuifunga Guinea 1-0 katika nusu fainali juzi.

Senegal walifunga bao hilo mapema kabisa katika mchezo huo uliofanyika mjini Ndola baada ya Aliou Badji kupachika wavuni mpira katika dakika ya 12.

Katika dakika za majeruhi za kipindi cha kwanza, Ibrahima Niana nusura aifungie Senegal bao la pili lakini penalti yake iliokolewa na Moussa Camara.

Senegal imetinga fainali kwa mara ya pili mfululizo.

Kwa mara ya kwanza nchi hiyo ilitinga fainali mwaka 2015 lakini walijikuta wakifungwa na Nigeria na kulikosa taji hilo.

Sio Senegal au Zambia, ambayo Jumatano iliifunga Afrika Kusini kwa bao 1-0, ambapo hakuna kati yao iliyowahi kutwaa taji la mashindano hayo huko nyuma.

Fainali ya Jumapili itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Mashujaa jijini hapa, ambapo bingwa wa mwaka huu atapatikana.

No comments:

Post a Comment