Saturday 18 March 2017

Arsenal yapokea kichapo cha nne katika Ligi Kuu England, mashabiki hawamtaki Wenger


LONDON, England
ARSENAL leo imepokea kichapo cha nne katika mechi tano za Ligi Kuu ya England wakati Craig Dawson akifunga mara mbili na kuisaidia West Brom kupeleka kipigo kikubwa kwa the Gunners.

Kipigo hicho kimeifanya Arsenal kupoteza matumaini ya kumaliza ligi hiyo ikiwa ndani ya nne bora, nafasi ambayo ingeiwezesha kufuzu moja kwa moja kwa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Dawson alifanikiwa kufunga mabao yake mawili kwa kichwa, akiunganisha mipira ya kona huku mabeki wa the Gunners wakishindwa kuokoa.

Arsenal ilisawazisha kupitia kwa Alexis Sanchez aliyefunga kwa shuti la karibu likiwa ni bao lake la 18 katika ligi msimu huu.

Hatahivyo, Arsenal walijikuta wakiwa nyuma tena ndani ya kipindi cha pili wakati mchezaji aliyetokea benchi Hal Robson-Kanu akifunga bao baada ya kuugusa mpira mara ya pili tangu aingie uwanjani.

Arsenal, iliyopoteza kipa wao Petr Cech kutokana na maumivu, walishindwa kufanya kweli na kujikuta wakichapwa la tatu.

Kipigo hicho ni pigo mara mbili kwa kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, ambaye jana alijikuta matatani baada ya baadhi ya mashabiki kubeba mabango wakimtaka ajiuzulu.

Kundi la mashabiki ambao hawamtaki Wenger walikuwa wakipiga kelele huku wakiwa wamebeba mabango, ambayo mengine yalisomeka ‘inatosha inatosha’.

Hatma ya Wenger kuendelea kuifundisha timu hiyo baada ya kumalizika msimu huu, iko matatani baada ya kutupwa pointi tano kutoka katika nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo.

No comments:

Post a Comment