Friday 1 January 2016

Mh. Profesa Mbarawa ataka Taasisi Viwanja vya ndege ziwajibike kwa TAA




WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mh.Prof.  Makame Mbarawa ameagiza  watumishi wa Tassisi  zote  zinazotoa  huduma katika viwanja vya ndege  hapa nchini kuwajibika kwa Mameneja  wa Mamlaka  ya Viwanja vya Ndege  (TAA)  wanaosimamia  viwanja  ambavyo  watumishi hao wamepangiwa  kufanya  kazi. 

Mh. Mbarawa ametoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara ya siku moja kwenye Makao Makuu  ya  TAA  ambapo  pamoja na mambo mengine  alikagua  ujenzi unaondelea wa jengo la tatu la abiria (TBIII), na  kituo cha Zimamoto na Uokoaji. Pia  alitembelea mradi  wa usimikaji wa vivuko vipya vya abiria (Passenger Boarding  Bridges) na  usimikaji wa mitambo mipya ya kufua umeme wa dharura (Standby Generators) iliyopo katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Mkurugenzi wa  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Suleiman S. Suleiman akimuonesha kitu Prof. Makame Mbarawa wakati alipotembelea TAA jana.
Akizungumza  na menejimenti ya TAA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi  Suleiman S. Suleiman  katika Ofisi  za TAA  ikiwa ni sehemu ya majumuisho ya ziara yake, Prof. Mbarawa  aliwapongeza TAA kwa kazi nzuri wanayoifanya hususan  katika uboreshaji wa muindombinu na kuhudumia wateja. Hata hivyo alisema pamoja na sifa hiyo nzuri, kuna haja kwa TAA kuwa mdhibiti wa taasisi nyingine zote  zinazofanyakazi katika viwanja vya  ndege hapa nchini kama njia ya  kuepuka kuchafua sifa nzuri ya viwanja hivyo na nchi kwa ujumla.

“ Pamoja na kazi nzuri mnayoifanya,nadhani  wakati umefika sasa kwa taasisi zote zinazotoa huduma katika viwanja vya ndege hapa nchini  ziwe chini ya TAA”,  alisema  Prof. Mbarawa  huku akisisitiza umuhimu wa  taasisi hizo kufanya kazi  kwa kushirikiana  kama timu moja.  “Nyinyi ndio kioo katika jamii yetu, taasisi nyingine mfano uhamiaji wakachelewa kugonga mhuri kwenye hati za kusafiria, watu hawatambui kama ndio wao waliochelewesha na lawama watawatupia nyinyi,” alisisitiza Mh. Mbarawa na kuongeza kwamba anafanya utaratibu wa kuwasiliana na Wizara zote zinazohusiana  na taasisi hizo ili kupanga utaratibu muafaka.

Mbali na idara ya uhamiaji,  taasisi nyingine zinazotoa huduma kwenye viwanja vya ndege ni pamoja na Idara ya maliasili,  afya, kilimo, mifugo, madini,  polisi na kitengo cha kuzuia madawa ya kulevya.  
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akipata maelezo ya uboresha unaoendelea wa terminal Two kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Suleiman Suleiman jana
Mh. Mbarawa  pia  ameiagiza  TAA kubuni  mikakati  ya kuongeza ukusanyaji wa mapato zaidi ili iweze kujiendesha na pia ihakikishe kuwa inaepukana  na matumizi yasiyo ya lazima. Aliitaka watumishi wa TAA  kuzingatia uadilifu na weledi katika utendaji wao wa kazi na kuhudumia wateja  ikizingatiwa kuwa viwanja vya ndege ni kioo cha nchi.

“Nisingependa taarifa za matukio mbalimbali yanayotokea kwenye viwanja niyasikie au kuyaona kwenye vyombo vya habari wakati mimi mwenyewe sijui, hivyo tujenge utamaduni wa kuwa waadilifu na tufanye kazi kwa kuzingatia weledi, tuepukane na matukio ya hovyo,” alisisitiza Mh. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Suleiman alimhakikishia Waziri Mbarawa kutekeleza maagizo yake, likiwemo la kubuni mbinu mpya za mapato, na hata kuweka utaratibu wa kumpatia taarifa mbalimbali zinazotokea kwenye viwanja kabla hazijapelekwa sehemu nyingine yeyote, kwa ajili ya utekelezaji na kujenga uhusiano mzuri baina ya mamlaka na wizara kwa ujumla.

“Kuhusu mapato tunauhakika wakati wa jengo la tatu la abiria likifunguliwa yataongezeka, lakini tunaahidi kubuni mbinu nyingi zaidi, ili  tuwe na vyanzo vya uhakika vya mapato,” alisema Mhandishi Suleiman. Alisema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza idadi ya abiria watakaosafiri na ndege za ukubwa mbalimbali ikiwemo 380 Airbus yenye uwezo wa kubeba abiria 300.
Mkurugenzi wa TAA, Suleiman S. Suleiman akimuonesha Waziri Prof. Mbarawa ujenzi unaoendelea wa jengo la tatu la abiria (Terminal Three) wa uwanja huo wa ndege wa Julius Nyerere jijjini Dar es Salaam.
Awali,  Mh. Mbarawa alipotembelea ofisi za zimamoto zilizopo JNIA, alielezwa wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vifaa na hususan  magari ya zimamoto ambayo mbali na kuhudumia viwanja vya ndege, wakati mwingine  kulazimika pia kusaidia  jamii endapo nyumba zao zinakumbwa na majanga ya  moto.

       Imetolewa na kitengo cha Habari na Mahusiano na Sheria TAA.

No comments:

Post a Comment