Wednesday, 25 September 2019

Usalama Viwanja Vya Ndege Waimarishwa

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole (kushoto) akifafanua mambo mbalimbali yanayohusu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) walipotembelea maonesho ya Karibu Utalii Kusini, yanayofanyika kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeimarisha usalama kwa abiria, mizigo na wageni kwenye viwanja vyake vyote 58 inavyovisimamia.

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole amesema usalama huo ni pamoja na mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo, ambapo ukaguzi unafanywa kwa umakini na maafisa usalama waliothibitishwa (certified screeners) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

“Tunawakaribisha wageni wa ndani na nje ya nchi kutumia viwanja vyetu vya ndege kwani vina usalama wa uhakika, zikiwemo kamera za usalama, X-ray mashine na ukaguzi mwingine zaidi, ambazo zinafanikisha zoezi zima la usalama,” amesema Mwenisongole.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bahati Mollel akimpa maelezo Hamis Hassan alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka hiyo la Karibu Utalii Kusini yanayofanyika kwenye Viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.


Mwenisongole amesema pia tunatambua juhudi za serikali ya Awamu ya Tano, iliyopo chini ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia TAA inampango wa kujenga uzio kwenye kiwanja cha ndege cha Iringa, ambapo zabuni imeshatangazwa ili kupatikana kwa mkandarasi wa ujenzi huo.

Pia amewaita wawekezaji kuwekeza kwenye viwanja vya ndege kwa kuwekeza kwenye maduka yenye bidhaa mbalimbali pamoja, hoteli na karakana za ndege.
Grace Sanga mkazi wa Kiwanja cha ndege, Dkt. G. Nyamubi wa Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Iringa alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka hiyo.
 Naye Mhandisi Astelius John amesema TAA imefanya maboresho makubwa kwenye viwanja vya ndege kikiwemo kiwanja cha ndege cha Iringa, ambapo kumefanyiwa upanuzi wa jengo la abiria na ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege.

“Tunaboresha viwanja vya ndege ili viweze kuwa bora na kuhudumia abiria wengi wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa na sasa kwa Kiwanja cha Ndege Iringa hii ni kutokana na maboresho ya jengo la abiria    kubwa ambalo lina uwezo wa kuhudumia  abiria wanaotumia kiwanja cha Iringa kutoka 35 kwa siku hadi kufikia 200,” amesema.


Kwa upande wake Afisa Usalama, Miyaga Juma ametoa ushauri kwa wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya nchi watumie Kiwanja cha ndege cha Iringa, kwani kina usalama madhubuti, kazi inayofanywa na Maafisa usalama wenye kufuata miongozo mbalimbali ya kiusalama, aidha TAA imenunua mashine ya kisasa ya Ukaguzi ili kurahisisha ukaguzi na kuwepo kwa mfumo wa kamera (CCTV) ambao unahifadhi kumbukumbu za matukio hali inayoboresha usalama Kiwanjani.

No comments:

Post a Comment