Na Mwandishi Wetu
VINARA wa
Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamezidi kuukaribia ubingwa baada ya leo kuibuka
na pointi zote tatu kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo
uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Bao hilo
pekee lililoifanya Simba kuzidi kuukaribia ubingwa ambao kwa mara ya mwisho
waliutwaa katika msimu wa mwaka 2011-12, lilifungwa na Erasto Nyoni katika
dakika ya 37 kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Shiza Kichuya
na kuparazwa na Rafael Daud na kumkuta mfungaji.
Yanga
walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wake Hassan Kessy kutolewa baada
ya kupewa kadi ya pili ya njano kutokana na kumchezea vibaya Asante Kwasi
katika dakika ya 48.
Pamoja na
kucheza pungufu, lakini Simba walishindwa kutumia nafasi hiyo kupata bao
jingine na badala yake kila dakika zilipotokomea, waliendelea kucheza kwa
kujihami zaidi na kurudi nyuma.
Hatahivyo,
Simba ndio walitawala zaidi mchezo huo, ambapo walipata jumla ya kona nane
wakati watani zao Yanga hawakupata kona yoyote huku Yanga wakiwa nakadi mbili
za njano wakati Simba moja na washindi walipiga mashuti matano yaliyolenga bao
wakati Yanga mawili tu.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 62 na sasa kuhitaji pointi sita tu ili kujihakikishia
ubingwa kwani Yanga akishinda mechi zake zote sita zilizobaki atafikisha pointi
66 tu, ambazo zitakuwa zimepitwa na Wekundu wa Msimbazi.
Baada ya
kipigo hicho, Yanga wanaendelea kuwa katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi zao
48 wakiwa pointi moja nyuma ya Azam FC, ambayo iko katika nafasi ya pili licha
ya kucheza mechi 26 wakati Yanga wamecheza jumla ya mechi 24.
Akizungumza
baada ya mchezo huo, Nyoni ambaye alifunga bao hilo pekee alisema kuwa wao
wamepania kila mechi kupata pointi tatu na alifanikiwa kufunga bao hilo baada
ya mabeki wa Yanga kuwabana wafungaji wa Simba, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na
John Bocco.
Endapo Simba
itatwaa ubingwa wa Tanzania Bara, itapata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika
mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika msimu ujao.
Kikosi Simba kilikuwa: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Nicholas Gyan/ Paul Bukaba, Yusufu Mlipili, James Kotei, Jonasi Mkude, Asante Kwasi, Shomari
Kapombe, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.
Yanga:Youthe
Rostand, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Said
Makapu, Yusuph Mhilu, Papy Tshishimbi/Emmanuel Martin, Obrey Chirwa, Raphael
Daud/ Juma Mahadhi na Ibrahim Ajibu/
Pius Buswita.
MP W D L GF GA +/- Pts
Simba 26 18 8 0 59 13 46 62
Azam 26 13 10 3 25 12 13 49
Yanga 24 13 9 2 40 14 27 48
Prisons 25 9 11 5 22 18 4 38
Singida 26 9 11 6 23 24 -1 38
Mtibwa 25 8 9 8 20 19 1 33
Lipuli 26 7 11 8 19 20 -1 32
Ruvu 26 8 8 10 26 33 -7 32
Stand 26 7 8 11 19 30 -11 29
Mbeya City 26 5 13 8 23 30 -7 28
Kagera Sugar 26 5 12 9 17 25 -8 27
Mwadui 25 5 11 9 27 34 -7 26
Mbao 25 5 9 11 23 33 -10 24
Majimaji 26 4 11 11 26 36 -10 23
Ndanda 26 4 11 11 17 28 -11 23
Njombe Mji 26 4 10 12 16 33 -17 22