Wednesday, 14 August 2019

Bodystreet Kumdhamini Masomo Ujerumani Mchezaji Tanzanite


Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akifanya mazoezi katika Gym ya Bodystreet iliyopo jirani na Makao Makuu ya Airtel Morocco jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Bodystreet, Emma Lehner Lyayuka akifuatilia mazoezi hayo leo.

Na Mwandishi Wetu
GYM ya kisasa nchini ya Bodystreet imempatia ofa ya masomo nchini Ujerumani mchezaji bora wa mashindano ya Kombe la Cosafa 2019 kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 iliyomalizika wiki iliyopita nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mtendaji Mkuu na muanzilishi wa Bodystreet hapa nchini, Emma Lehner Lyayuka alisema kuwa wameamua kumpatia Enekia Kasonga ofa ya masomo nchini Ujerumani.

Pia mbali na kusoma masomo hayo ya michezo, pia atakuwa akicheza soka katika timu ya wanawake ya FFC Wacker München  ya Munich, Ujerumani katika kipindi chote atakachokuwa akisoma.

Kasonga ambaye anaichezea Alliance Queens ya Mwanza, alikuwa mchezaji bora katika mchezo wa Tanzania (Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini, ambapo Tanzania ilishinda 2-0 na yeye alifunga bao moja. Pia alifunga jumla ya mabao manne katika mashindano hayo.
Pia mchezaji huyo alifunga bao pekee la Tanzania wakati ilipofungwa 2-1 na Zambia katika hatua ya makundi na kuifanya kumaliza ya pili na kutinga nusu fainali.

Lyayuka alisema kuwa walimuona Enekia katika mchezo wa Tanzanite na Afrika Kusini wa Kombe la Cosafa na walivutiwa sana jinsi alivyokuwa akicheza na kuisaidia Tanzania kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mwaka huu.

Alisema wanafanya mawasiliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kukamilisha taratibu mbalimbali za kumuwezesha mchezaji huyo kwenda kusoma Ujerumani mafunzo ya kuanzia miezi mitatu hadi mwaka.

Wakati wa kutangaza ofa hiyo, Bodystreet waliwaonesha waandishi wa habari vifaa vya teknolojia ya kisasa vya kufanyia mazoezi, ambavyo ni vya kwanza kuwepo nchini.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi alifanyishwa mazoezi kupitia vifaa hivyo, ambapo alikiri kuwa vinabana muda na mtu anafanyishwa mazoezi katika viungo vyote.

Bayi alisema kuwa gym hiyo inasaidia sana kubana muda kwani mtu hatumii muda mwingi, lakini mwili mzima unafanyishwa mazoezi kutokana na kizibao anachokivaa wakati wa mazoezi.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Alliance na TFF ili kuzungumzia ofa hiyo jana hazikufanikiwa baada ya baadhi yao simu zao kutopatikana kabisa na wengine ziliita bila majibu.

Thursday, 8 August 2019

TAA Yawahakikishia SADC Huduma Bora

Raia wenye Asili ya Asia, kuanzia kulia Cuco Donny, Dorony Mnarty na Zohra
Lukmanji leo wakimsikiliza Kaimu Meneja Biashara wa Kiwanja cha Ndege cha 
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bi. Herieth Nyalusi (kushoto), 
walipotembelea maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo 
Kusini Mwa Afrika (SADC) katika Banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania 
(TAA), kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo 
yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.
Kaimu Meneja Biashara, Bi. Herieth Nyalusi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (wa kwanza kulia), akitoa  maelezo mbalimbali kwa Bw. Mohamed Issa alipotembelea maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) katika Banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) waliopo kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.
 Mzee Iluganyuma (kulia) leo akimsikiliza Kaimu Meneja Biashara wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Bi. Herieth Nyalusi alipotembelea maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) katika Banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) waliopo kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bahati Mollel akitoa maelezo mbalimbali kwa Wilson Ishengoma (kulia) na watoto wake walipotembelea Banda la maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwenye viwanja vya Karimjee. Maonesho hayo yamefungwa leo na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.


Friday, 2 August 2019

DStv Yazindua `Soka Mwaa...Mwiii..’!

Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania, Jacquline Woiso (kulia) akimkabidhi zawadi mchezaji wazamani wa Simba, Dua Said wakati wa hafla ya uzinduzi wa Msimu Mpya wa Ligi za Ulaya, jijini Dar es Salaam leo. 

Na Mwandishi Wetu
WACHEAJI nyota wazamani wa Tanzania leo walipamba uzinduzi wa msimu mpya wa mechi za Ligi mbalimbali za Ulaya, ambazo zitaoneshwa na DStv katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya nyota hao waliowahi kutamba katika soka la Bongo ni pamoja na Edibily Lunyamila, Sekilojo Chambua, Fikiri Magoso, Dua Said na wengineo, ambao waliipongeza channel hiyo kuonesha ligi hizo.

Pazia la Ligi Kuu ya England msimu wa mwaka 2019/2020 linafunguliwa rasmi kesho Jumapili kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Manchester City na Liverpool utakaoneshwa moja kwa moja na DStv.

Kwa mujibu wa  Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Multchoice, Ronald Shelukindo, DStv wataanza kuonesha kipute hicho cha Ngao ya Jamii na baadae kuendelea na ligi zingine zote kubwa Ulaya, zikiwemo za Hispania (La Liga), Italia (Serie A) na zinginezo.

Alisema: “ Soka Mwaa…Mwiii…Ndani ya DStv, yaani wananchi watapata soka mwanzo mwisho mechi kibao.”

 Alisema pia DStv itaendelea kurusha hewani Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Ligi ya Ulaya pamoja na ligi zingine kubwa, ambazo zinafuatiliwa na watu wengi.
Wachezaji wazamani wa Tanzania (mstari wa nyuma waliosimama) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Multchoice-Tanzania, Jacquline Woiso (watatu kushoto mstari wa mbele) pamoja na wachambuzi wa soka katika hafla jijini leo.
Shelukindo alisema DStv itahakikisha wateja wake wote wanaendelea kuliona soka katika muonekano bora zaidi, huku wakipata matangazo hayo ya Ligi Kuu ya England kwa lugha ya Kiswahili.

“Kampeni yetu ya sasa tunasema ni ‘Soka Mwanzo Mwisho’ na tunamaanisha kwani kwa wateja wetu wa DStv, burudani ya soka haitawatindikia kamwe! 

Ni wapi unaweza kuona mechi zote 380 za ligi ya Uingereza, mechi  380, za Ligi Kuu ya Hispania, mechi 380 za Ligi Kuu ya Italia bila kusahau mechi  za ligi ya mabingwa Ulaya na nyingine nyingi?  Bila shaka ni DStv pekee. Ndiyo sababu tunasema kwetu DStv ni Soka Mwanzo Mwisho!”
Mchezaji wazamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Edibily Lunyamila akzungumza wakati wa hafla hiyo leo. Kulia ni mchezaji mwenzake wazamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua. 
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na wadau wa soka nchini wakiwemo wasanii mbalimbali, wachezaji wazamani na watangazaji wanaotangaza Ligi Kuu ya England kwa Kiswahil, ambao ni Salama Jabir, Edo Kumwembe, Maulid Kitenge, Ibrahim Masoud (Maestro), Abuubakar Lyongo na Oscar Oscar.

Thursday, 1 August 2019

Jengo la 3 la abiria JNIA kuongeza chachu ya Uchumi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi mbalimbali akikata utepe kuashiria kufungua rasmi Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 1, 2019
Na Mwandishi Wetu
JENGO la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB III) litaongeza chachu ya kukua kwa uchumi wa nchi, imeelezwa.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipozindua jengo hilo, ambalo sasa limeanza kutumika kwa safari za nje ya nchi baada ya kukamilika kwake.

Rais Magufuli amesema mbali na jengo hilo litatoa ajira mbalimbali kwa wazawa, pia litaruhusu wananchi kuwekeza katika huduma mbalimbali ndani na nje ya jengo hilo, ambapo ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha Wazawa wanapewa kipaumbele katika uwekezaji katika jengo hilo.
Rais Dk John Pombe Magufuli na Viongozi wa dini, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeiry bin  Ally na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Muadhama Polycarp Kardinali Pengo na viongozi wengine wakifunua pazia kama ishara ya ufunguzi rasmi wa Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 1, 2019
“Serikali inaimarisha usafiri wa anga kwa kununua ndege pamoja na kuimarisha miundombinu ya viwanja vya ndege, ambapo serikali inampango wa kukarabati na kujenga viwanja 15 nchini kikiwepo cha Kimataifga cha Msalato Dodoma, ili kuendelea kuufanya usafiri huu uendelee kuwa wa haraka na salama, ambapo utachangia kukuza pato la taifa kwa watumiaji wake, ambao kwa sasa abiria wameongezeka kwa asilimia 12 kwa mwaka,” amesema Mhe. Rais.

Amesema anaimani idadi ya abiria wa ndege wataongezeka zaidi kutokana na utalii unakwenca sambamba na usafiri wa anga, kutokana na Watalii wengi huja nchini kwa kutumia usafiri wa anga.

Hatahivyo, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa kufanikisha kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa jengo hilo, ambao mwaka 2016 ulisuasua kutokana na kukosekana kwa fedha za kuendelea na mradi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Wafanyakazi wa Benki ya NMB, ambao wanatoa huduma ya kubadilisha fedha ndani ya Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, ambalo amezindulia leo Agosti 1, 2019
Amewataka Watanzania kulipa kodi ili serikali iweze kukamilisha mapema kwa wakati miradi mikubwa, ambayo itakuja kuwanufaisha na kuwapa heshima kubwa.

“Miradi inawezekana kwani fedha nyingi zilikuwa zikitumiwa na mafisadi, hivyo nawataka tulipe kodi ili kufanikisha miradi yote, na tuachane na dhana ya wafadhili ambao wamekuwa na masharti,” amesema Mhe. Rais.

Hatahivyo, amewataka watumiaji wote wa Jengo hili kuhakikisha wanalitunza na wasiliharibu kutokana na kujengwa kwa fedha nyingi za Watanzania.

Katika hatua nyingine amempongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Jakaya Kikwete aliyeanzisha ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la abiria, na pia amewashukuru viongozi wa Dini nchini kuendelea kuliombea taifa.

Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kutokana na ongezeko la mara kwa mara la abiria, sasa Jengo la pili la abiria (JNIA-TBII) linaboreshwa na kukarabatiwa ili liweze kuhudumia abiria mara mbili ya sasa ambao ni Milioni 1.5 kwa mwaka.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (aliyenoosha kidole) wakati wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ,Mhandisi Julius Ndyamukama (kulia) mara baada ya kuzindua rasmi Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, leo Agosti 1, 2019
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patric Mfugale, ambao ndio walikuwa wasimamizi wa mradi huu wa kimkakati amesema jengo hili limekuja wakati muafaka kutokana na wananchi kuwa na mwamko wa kupanda ndege, ambapo kumekuwa na ongezeko la abiria, ambapo kwa sasa kati ya ndege 23 za nje tayari 18 zimeanza kutumia jengo hili.   

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama amesema TAA wapo tayari kuendesha huduma kwenye jengo hilo, ambapo wamefanya majaribio kadhaa ya ndege, ambapo tarehe 17 Julai, 2019 walianza na ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), iliyokuwa ikizindua safari yake ya kwanza kwenda nchini India.

Kwa upande wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amesema jengo hili la kisasa linaitoa Tanzania kimasomaso, kutokana na ukubwa na ubora wake.

“Nipo hapa kuwawakilisha Wabunge, ambapo tunaona fedha tunazopitisha zinatumika kihalali na tutaendelea kumuunga mkono Mhe. Rais katika jitihada zake za kuendeleza na kuanzisha miradi mbalimbali,” amesema Mhe. Spika.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma ame wataka wananchi kuhakikisha wanatatua migogoro yao ya ardhi inayohusisha ujenzi wa miradi mbalimbali nje ya mahakama, ili kufanikisha miradi hiyo kumalizika kwa wakati.

Sunday, 28 July 2019

Askari, Mbwa Kuongezwa Viwanja vya Ndege

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (kulia) akiongozana na maafisa wa ulinzi na usalama kukagua sehemu za kupitisha mizigo kwenye Jengo la tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa la Julius Nyerere (JNIA TB3), alipofanya ziara hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Mambo ya Ndani nchini, itaongeza askari watu na mbwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama kwenye viwanja vya Ndege nchini.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Masauni amesema hayo alipofanya ziara ya kikazi katika Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA TB3).

Masauni amesema serikali inatarajia kuongeza askari mbwa wengi wenye mafunzo na sifa, ili kuongeza ufanisi na ulinzi wa viwanja vyote vya ndege.

“Idadi ya mbwa inatakiwa iongezwe hasa inapokaribia kuhamia kwenye jengo jipya la tatu la abiria, ambalo litakuwa na idadi kubwa ya abiria na changamoto nyingi, pia kwa viwanja vingine navyo vitaangaliwa kwa suala la ulinzi,” alisema Masauni.

Hatahivyo, amesema hatasita kukifuta kitengo cha mbwa endapo hakutakuwa na mbwa wa kukidhi mahitaji na wenye sifa zote, kwani kwa sasa askari binadamu ni wengi zaidi.

Ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP), Simon Sirro  kuhakikisha mfumo na ushiriki wa askari wake unaweza kuboreshwa na wale wanapelekwa viwanja vya ndege wawe na sifa na vigezo maalum vya kuweze kubaini vitu kama nyara za serikali, madini na  madawa ya kulevyia.

“Hii itasaidia kwa kuwa na mfumo wa pamoja wa ushirikiano katika udhibiti, jingine ni kuhakikisha IGP analisimamia na kulitekeleza kwa haraka sana, kwani tumekuwa na askari mbwa waliopata mafunzo maalum ya kubaini vitu mbalimbali vinavyopitishwa kwenye viwanja vya ndege, hivyo maelekezo yangu kwake tuongeze idadi ya mbwa wenye sifa hapa JNIA ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Masauni.

Masauni amefanya ziara hiyo siku moja baada ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kushughudia makabidhiano ya kilo 35.267 za dhahabu zilizokamatwa Februari 15, 2019 katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta, Nairobi nchini Kenya.

Saturday, 27 July 2019

Real Yakiona cha Mtema Kuni, Yachapwa 7-3

Diego Costa, mfungaji wa bao nne pekee wakati Real Madrid ikifungwa 7-3 na Atletico Madrid.

NEW JERSEY, Marekani
DIEGO Costa alifunga mabao manne na alitolewa wakati Atletico Madrid ikiisambaratisha Real Madrid kwa mabao 7-3 jijini hapa.

Costa alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya kwanza na kukamilisha hat-trick yake kwa bao la penalti alilofunga katika dakika ya 45.

Joao Felix, mchezaji aliyesajiliwa katika kipindi hiki cha majira ya joto kwa ada ya  pauni milioni 113, naye pia alifunga bao lake la kwanza katika klabu hiyo wakati Atletico ikiongoza kwa mabao 5-0 hadi mapumziko.

Costa alingeza la nne dakika sita baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, kabla ya yeye na mchezaji wa Real Dani Carvajal hawajatolewa kwa kadi nyekundu baada ya kupigana katika dakika ya 61.

Angel Correa, aliyeingi aakichukua nafasi ya majeruhi Alvaro Morata, naye pia alizifumania nyavu katika kipindi cha kwanza, wakati Vitolo alifunga bao la saba kwa Atletico katika dakika ya 70.

Real waliendelea kuwa nyuma kwa mabao 6-0 kabla Real Madrid haijarekea katika ubao wa matangazo kwa mabao kupitia kwa Nacho, wakati Karim Benzema na Javier Hernandez wote wakifunga mabao katika dakika za majeruhi.

Gareth Bale, ambaye anajiandaa kuondoka Real Madrid na kujiunga klabu ya China ya Jiangsu Suning, alianzia katika benchi, lakini aliingia katika dakika 30 za mwisho.

Real, ambayo ilitumia kiasi cha pauni milioni 300 katika kipindi cha majira ya joto, ilianza kusajili kwa kumsajili Eden Hazard na Luka Jovic.

Lakini walipambana katika ziara yao ya Marekani kabla ya kuanza kwa ligi, ambapo walifungwa 3-1 na Bayern Munich na kuifunga Arsenal kwa penalti baada ya kutoka sare ya 2-2.

"Tulipoiangalia Madrid, tulikuwa tukiangalia wapi tutaimaliza, “alisema kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone. "Tulikuwa na muda mzuri hapa.”

Nahodha wa Real Sergio Ramos alisema: "Ni wazi hatuikuwa tukijisikia vizuri hapa. Na huu ndio mwanzo wa maandalizi yetu, Kuna njia nyingi zinazokufanya ushindwe, lakini hatuwezi kufanya kama tulivyofanya leo.

Kocha wa Real Zinedine Zidane aliongeza: "Hatuna haja ya kumtafuta mchawi katika hilo, hii ni mechi za maandalizi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.


Bale Kulamba Bil 2.4 Kwa Wiki Akicheza China

MADRID, Hispania
GARETH Bale anakaribia kukamilisha uhamisho kutoka Real Madrid kwenda katika klabu ya China ya Jiangsu Suning kwa mkataba wa miaka mitatu utakaomuwezesha kuweka kibindoni mshahara wa pauni milioni 1 (sawa na sh bilioni 3) kwa wiki.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales, yuko katika hatua za mwisho za makubaliano na Jiangsu, ambao sasa wana uhakika wa kukamilisha usajili wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30.

Endapo mpango huo utakwenda vizuri, basi Bale atakuwa amelamba dume kwa kupata karibu mara mbili ya mshahara wake wa pauni 600,000 kwa wiki ambao analipwa Real Madrid na atakuwa nyota mkubwa kujiunga na Ligi Kuu ya China.

Klabu ya Beijing Guoan nayo pia imeulizia kutaka kumsajili, lakini Jiangsu ndio inaonekana kushinda mbio hizo za kumpata mchezaji huyo.

Lionel Messi ndiye mchezaji soka anayelipwa zaidi duniani, ambapo kwa wiki anaondoka na karibu pauni milioni 1.7 katika Barcelona, na mkataba wa Bale pale  Jiangsu utamuwezesha kumkaribia mchezaji huyo wa Barca.

Chanzo cha karibu kabisa na mchezaji huyo wazamani wa Tottenham Hotspur kimeelezea ofa hiyo ya Jiangsu kama ni “isiyoelezeka”.

Bale alikuwa akijiandaa kung’ang’ania kubaki Real Madrid, licha ya kocha Zinedine Zidane kuweka wazi kuwa anamtaka mchezaji huyo kuondoka katika klabu hiyo, lakini taarifa zilizotolewa na Telegraph Sport, zinasema mchezaji huyo yuko tayari kwenda China.

Chanzo kutoka Hispania kinadai kuwa Bale atasaini mkataba wa miaka mitatu ndani ya saa kadhaa, ingawa marafiki wa mchezaji huyo Ijumaa walisema mpango huo bado haujakamilika vizuri.

Zidane alimaliza kipindi cha Bale Real Madrid baad aya mchezo wa kirafiki wa maandalizi uliofanyika Jumapili iliyopita dhidi ya Bayern Munich aliposema: 
“Hajamuhusisha mchezaji huyo katika kikosi chake wakati klabu hiyo ikifanyia kazi suala la kuondoka kwake, na ndio maana hakucheza.

“Tutaangalia nini kitatokea katika siku zijazo. Tunatakiwa kuangalia nini kitatokea kesho, endapo kitatokea, basi ni jambo zuri. Acha tuwe na matumaini kwa faida ya kila mmoja, na hilo litatokea haraka sana. Klabu inawasiliana na klabu nyingine…”

Wakala wa Bale, Jonathan Barnett aliendelea kusema kuwa Zidane “amekywqa amuheshimu” mteja wake, lakini kocha huyo ameendelea kusisitiza kuwa hali ya mshambuliaji hyo bado inabaki vile vile licha ya Marco Asensio kuendelea kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Zidane pia aliendelea kumbania Bale, huku akiendelea kuwa kimya bila kuelezea mcheaji huyo anataka nini.

Sasa inaonekana kipindi cha miaka sita cha Bale kukaa Real kimekaribia kumalizika na kuiacha klabu hiyo aliyotwaa nayo mataji manne ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na taji la La Liga.

Hiyo inamfanya Bale kuwa mwanasoka wa Uingereza mwenye mafanikio zaidi anayecheza soka nje hasa pale aliponunuliwa kwa rekodi ya ada ya pauni milioni 85 wakat akitua Real akitokea Tottenham mwaka 2013.

Dirisha la usajili China linatarajia kufungwa Jumatano ijayo, lakini Bale anatarajia kuwa mchezaji wa Jiangsu katika kipindi hicho na kuhamia kwake China kutamfanya kupata mapokezi ya kishujaa.

Kwa sasa Ezequiel Lavezzi ndiye mchezaji anayelipwa zaidi China kwa anapewa pauni 500,000 kajubu mkataba wa Bale utafunika huo wa Muargentina huyo.

Ni Kisasi Taifa Stars, Harambee Leo Uwanja wa Taifa

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wakijifua kwenye Uwanja wa Boko Veterani.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kucheza kesho dhidi ya timu ya taifa ya Kenya ‘Harembee Stars’ mchezo wa kwanza wa kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan 2020) utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni muhimu kwa Stars kuhakikisha inatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga raundi ya mwisho ya kufuzu. Timu hizo zitarudiana Agosti 4.

Stars inataka kulipiza kisasi hasa baada ya kufungwa katika mchezo wa makundi kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) Misri bada ya kuchapwa 3-2 licha ya kuongoza mara mbili.

Lakini mchezo wa leo utawahusisha wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani na Taifa Stars ndio inaonekana kuwa na faida zaidi baada ya kuwa na asilimia kubwa ya kikosi chake kilichoenda Misri kupata uzoefu mkubwa.

Iwapo watatumia vyema uwanja wa nyumbani watajitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu.

Hatahivyo, Kenya sio timu ya kubeza kwani wako vizuri na wanataka kuutumia mchezo huo kupata matokeo ili kujiweka vizuri kwa ajili ya mchezo wa mwisho utakaofanyika Nairobi wiki ijayo.

Katika viwango vya ubora wa soka duniani bado Kenya wako vizuri ukilinganisha na Tanzania, wanashikilia nafasi ya 107, huku ndugu zao wakishika nafasi ya 137.
Kila mmoja ana nafasi ya kupata matokeo kulingana na alivyojiandaa dhidi ya mpinzani wake kimbinu.

Mchezo huo utakuwa ni mtihani wa kwanza kwa makocha Ettiene Ndayiragije na wenzake walioteuliwa kukaimu nafasi ya Emmanuel Amunike na Hemed Morocco.
Akizungumzia mchezo huo Kocha Ndayiragije alisema alisema jana kuwa maandalizi yote yako vizuri na kwamba kinachohitajika kwa wachezaji ni umakini kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Nahodha John Bocco alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwani kila mmoja atahitaji matokeo kujiweka katika nafasi nzuri, lakini anaamini kwa morali walionao watapambana kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani.

Bocco aliwaomba Watanzania kutoenda uwanjani na matokeo yaliyopita bali sasa wako vizuri kulipiza kisasi kwa kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.

Tanzania kwa mara ya mwisho ilishiriki fainali za Chan zilipofanyika Ivory Coast 2009 ikiwa ni miaka 10 sasa, hivyo itataka mwaka huu iweke rekosi tena kwa kufuzi fainali hizo.

Fainali za kwanza za Chan zilifanyika mwaka 2009 na lengo la Shirikisho la Afrika (Caf) ni kutoa nafasi kwa wachezaji ambao hawajasajiliwa nje ya nchi zao na kuwawezesha kujitangaza.

Ulinzi Kuimarishwa Viwanja vya Ndege Tanzania


 
 Mhandisi Burton Komba (wanne kulia) anayesimamia mradi wa ujenzi wa Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), akimweleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Hamad Masauni  (mwenye suti) alipotembelea jengo hilo hivi karibuni.


Na Mwandishi Wetu

Wizara ya Mambo ya Ndani nchini, itaongeza askari watu na mbwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama kwenye viwanja vya Ndege nchini.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Masauni amesema hayo alipofanya ziara ya kikazi katika Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA TB3).

Masauni amesema serikali inatarajia kuongeza askari mbwa wengi wenye mafunzo na sifa, ili kuongeza ufanisi na ulinzi wa viwanja vyote vya ndege.

“Idadi ya mbwa inatakiwa iongezwe hasa inapokaribia kuhamia kwenye jengo jipya la tatu la abiria, ambalo litakuwa na idadi kubwa ya abiria na changamoto nyingi, pia kwa viwanja vingine navyo vitaangaliwa kwa suala la ulinzi,” alisema Masauni.

 Ofisa Usalama Mwandamizi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Ramadhani Mkumbukwa (aliyenyoosha mkono), akimweleza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (wapili kulia) namna ya ukaguzi wa abiria na mizigo unavyofanyika wakiwa kwenye jengo la tatu la abiria la JNIA hivi karibuni.

Hatahivyo, amesema hatasita kukifuta kitengo cha mbwa endapo hakutakuwa na mbwa wa kukidhi mahitaji na wenye sifa zote, kwani kwa sasa askari binadamu ni wengi zaidi.

Ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP), Simon Sirro  kuhakikisha mfumo na ushiriki wa askari wake unaweza kuboreshwa na wale wanapelekwa viwanja vya ndege wawe na sifa na vigezo maalum vya kuweze kubaini vitu kama nyara za serikali, madini na  madawa ya kulevyia.

“Hii itasaidia kwa kuwa na mfumo wa pamoja wa ushirikiano katika udhibiti, jingine ni kuhakikisha IGP analisimamia na kulitekeleza kwa haraka sana, kwani tumekuwa na askari mbwa waliopata mafunzo maalum ya kubaini vitu mbalimbali vinavyopitishwa kwenye viwanja vya ndege, hivyo maelekezo yangu kwake tuongeze idadi ya mbwa wenye sifa hapa JNIA ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Masauni.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (mwenye suti), akionyesha jambo akiwa kwenye eneo la ukaguzi wa abiria na mizigo wakati alipotembelea jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa la Julius Nyerere (JNIA TB3) hivi karibuni.
Masauni amefanya ziara hiyo siku moja baada ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kushughudia makabidhiano ya kilo 35.267 za dhahabu zilizokamatwa Februari 15, 2019 katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta, Nairobi nchini Kenya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (kulia) akiongozana na maafisa wa ulinzi na usalama kukagua sehemu za kupitisha mizigo kwenye Jengo la tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa la Julius Nyerere (JNIA TB3), alipofanya ziara hivi karibuni.


Thursday, 18 July 2019

STARS YAPANGWA NA TUNISIA, LIBYA NA GUINEA YA IKWETA MBIO ZA KUFUZU AFCON 2021 CAMEROON


CAIRO, Misri
TIMU ya taifa ya Tanzania imepangwa katika Kundi J pamoja na Tunisia, Libya na Guinea ya Ikweta, katika mbio za kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za michuano ya Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Cameroon 2021.

Hilo limebainka baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) kupanga ratiba hiyo katika hafla iliyofanyika jijini hapa.

Katika kundi hilo la Tanzania na Tunisia ndizo pekee zilikuwepo katika fainali za mwaka huu ambazo zinamalizika kesho jijini hapa, kwa kuzikutanisha Algeria na Senegalm ambazo zote zimetoka katika Kundi C pamoja na Tanzania, huku Guinea ya Ikweta na Libya zilishindwa kufuzu.

Tunisia wenyewe ilifungwa na Nigeria 1-0 jana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu Afcon 2019 Misri wakati Tanzania ilifungwa mechi zote tatu za Kundi C, ikiwa  2-0 na Senegal, 3-2 na Kenya huku Algeria ikiichapa Stars 3-0.
Kenya iliyokuwa kundi moja na Tanzania kwenye fainali za mwaka huu, yenyewe kwenye mbio za kusaka tiketi ya kwenda Cameroon 2021, imepangwa Kundi G pamoja na wenyeji wa mwaka huu Misri, Togo na Comoro.

Uganda wamepangwa Kundi B pamoja na Burkina Faso, Malawi na ama Sudan Kusini au Shelisheli, wakati Algeria imepangwa Kundi H pamoja na Zambia, Zimbabwe na Botswana na Senegal ipo Kundi I pamoja na Kongo, Guinea Bissau na Eswatini.

MAKUNDI YOTE KUFUZU AFCON 2021 CAMEROON

Kundi A: Mali, Guinea, Namibia, Liberia/Chad

Kundi B: Burkina Faso, Uganda, Malawi, Sudan Kusini/Shelisheli

Kundi C: Ghana, Afrika Kusini, Sudan, Mauritius/Sao Tome

Kundi D: DRC, Gabon, Angola, Djibouti au Gambia

Kundi E: Morocco, Mauritania, CAR, Burundi

Kundi F: Cameroon, Cape Verde, Msumbiji, Rwanda

Kundi G: Misri, Kenya, Togo, Comoro

Kundi H: Algeria, Zambia, Zimbabwe, Botswana

Kundi I: Senegal, Congo, Guinea Bissau, Eswatini

Kundi J: Tunisia, Libya, Tanzania, Equatorial Guinea

Kundi K: Ivory Coast, Niger, Madagascar, Ethiopia

Kundi L: Nigeria, Benin, Sierra Leone, Lesotho