Sunday 28 July 2019

Askari, Mbwa Kuongezwa Viwanja vya Ndege

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (kulia) akiongozana na maafisa wa ulinzi na usalama kukagua sehemu za kupitisha mizigo kwenye Jengo la tatu la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa la Julius Nyerere (JNIA TB3), alipofanya ziara hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Mambo ya Ndani nchini, itaongeza askari watu na mbwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama kwenye viwanja vya Ndege nchini.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hamad Masauni amesema hayo alipofanya ziara ya kikazi katika Jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA TB3).

Masauni amesema serikali inatarajia kuongeza askari mbwa wengi wenye mafunzo na sifa, ili kuongeza ufanisi na ulinzi wa viwanja vyote vya ndege.

“Idadi ya mbwa inatakiwa iongezwe hasa inapokaribia kuhamia kwenye jengo jipya la tatu la abiria, ambalo litakuwa na idadi kubwa ya abiria na changamoto nyingi, pia kwa viwanja vingine navyo vitaangaliwa kwa suala la ulinzi,” alisema Masauni.

Hatahivyo, amesema hatasita kukifuta kitengo cha mbwa endapo hakutakuwa na mbwa wa kukidhi mahitaji na wenye sifa zote, kwani kwa sasa askari binadamu ni wengi zaidi.

Ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP), Simon Sirro  kuhakikisha mfumo na ushiriki wa askari wake unaweza kuboreshwa na wale wanapelekwa viwanja vya ndege wawe na sifa na vigezo maalum vya kuweze kubaini vitu kama nyara za serikali, madini na  madawa ya kulevyia.

“Hii itasaidia kwa kuwa na mfumo wa pamoja wa ushirikiano katika udhibiti, jingine ni kuhakikisha IGP analisimamia na kulitekeleza kwa haraka sana, kwani tumekuwa na askari mbwa waliopata mafunzo maalum ya kubaini vitu mbalimbali vinavyopitishwa kwenye viwanja vya ndege, hivyo maelekezo yangu kwake tuongeze idadi ya mbwa wenye sifa hapa JNIA ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Masauni.

Masauni amefanya ziara hiyo siku moja baada ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kushughudia makabidhiano ya kilo 35.267 za dhahabu zilizokamatwa Februari 15, 2019 katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta, Nairobi nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment