Wednesday 14 August 2019

Bodystreet Kumdhamini Masomo Ujerumani Mchezaji Tanzanite


Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi akifanya mazoezi katika Gym ya Bodystreet iliyopo jirani na Makao Makuu ya Airtel Morocco jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Bodystreet, Emma Lehner Lyayuka akifuatilia mazoezi hayo leo.

Na Mwandishi Wetu
GYM ya kisasa nchini ya Bodystreet imempatia ofa ya masomo nchini Ujerumani mchezaji bora wa mashindano ya Kombe la Cosafa 2019 kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 iliyomalizika wiki iliyopita nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mtendaji Mkuu na muanzilishi wa Bodystreet hapa nchini, Emma Lehner Lyayuka alisema kuwa wameamua kumpatia Enekia Kasonga ofa ya masomo nchini Ujerumani.

Pia mbali na kusoma masomo hayo ya michezo, pia atakuwa akicheza soka katika timu ya wanawake ya FFC Wacker München  ya Munich, Ujerumani katika kipindi chote atakachokuwa akisoma.

Kasonga ambaye anaichezea Alliance Queens ya Mwanza, alikuwa mchezaji bora katika mchezo wa Tanzania (Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini, ambapo Tanzania ilishinda 2-0 na yeye alifunga bao moja. Pia alifunga jumla ya mabao manne katika mashindano hayo.
Pia mchezaji huyo alifunga bao pekee la Tanzania wakati ilipofungwa 2-1 na Zambia katika hatua ya makundi na kuifanya kumaliza ya pili na kutinga nusu fainali.

Lyayuka alisema kuwa walimuona Enekia katika mchezo wa Tanzanite na Afrika Kusini wa Kombe la Cosafa na walivutiwa sana jinsi alivyokuwa akicheza na kuisaidia Tanzania kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa mwaka huu.

Alisema wanafanya mawasiliano na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kukamilisha taratibu mbalimbali za kumuwezesha mchezaji huyo kwenda kusoma Ujerumani mafunzo ya kuanzia miezi mitatu hadi mwaka.

Wakati wa kutangaza ofa hiyo, Bodystreet waliwaonesha waandishi wa habari vifaa vya teknolojia ya kisasa vya kufanyia mazoezi, ambavyo ni vya kwanza kuwepo nchini.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi alifanyishwa mazoezi kupitia vifaa hivyo, ambapo alikiri kuwa vinabana muda na mtu anafanyishwa mazoezi katika viungo vyote.

Bayi alisema kuwa gym hiyo inasaidia sana kubana muda kwani mtu hatumii muda mwingi, lakini mwili mzima unafanyishwa mazoezi kutokana na kizibao anachokivaa wakati wa mazoezi.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Alliance na TFF ili kuzungumzia ofa hiyo jana hazikufanikiwa baada ya baadhi yao simu zao kutopatikana kabisa na wengine ziliita bila majibu.

No comments:

Post a Comment