Saturday 27 July 2019

Ni Kisasi Taifa Stars, Harambee Leo Uwanja wa Taifa

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, wakijifua kwenye Uwanja wa Boko Veterani.

Na Mwandishi Wetu
TIMU ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kucheza kesho dhidi ya timu ya taifa ya Kenya ‘Harembee Stars’ mchezo wa kwanza wa kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan 2020) utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni muhimu kwa Stars kuhakikisha inatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga raundi ya mwisho ya kufuzu. Timu hizo zitarudiana Agosti 4.

Stars inataka kulipiza kisasi hasa baada ya kufungwa katika mchezo wa makundi kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) Misri bada ya kuchapwa 3-2 licha ya kuongoza mara mbili.

Lakini mchezo wa leo utawahusisha wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani na Taifa Stars ndio inaonekana kuwa na faida zaidi baada ya kuwa na asilimia kubwa ya kikosi chake kilichoenda Misri kupata uzoefu mkubwa.

Iwapo watatumia vyema uwanja wa nyumbani watajitengenezea mazingira mazuri ya kufuzu.

Hatahivyo, Kenya sio timu ya kubeza kwani wako vizuri na wanataka kuutumia mchezo huo kupata matokeo ili kujiweka vizuri kwa ajili ya mchezo wa mwisho utakaofanyika Nairobi wiki ijayo.

Katika viwango vya ubora wa soka duniani bado Kenya wako vizuri ukilinganisha na Tanzania, wanashikilia nafasi ya 107, huku ndugu zao wakishika nafasi ya 137.
Kila mmoja ana nafasi ya kupata matokeo kulingana na alivyojiandaa dhidi ya mpinzani wake kimbinu.

Mchezo huo utakuwa ni mtihani wa kwanza kwa makocha Ettiene Ndayiragije na wenzake walioteuliwa kukaimu nafasi ya Emmanuel Amunike na Hemed Morocco.
Akizungumzia mchezo huo Kocha Ndayiragije alisema alisema jana kuwa maandalizi yote yako vizuri na kwamba kinachohitajika kwa wachezaji ni umakini kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Nahodha John Bocco alisema mchezo huo utakuwa mgumu kwani kila mmoja atahitaji matokeo kujiweka katika nafasi nzuri, lakini anaamini kwa morali walionao watapambana kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani.

Bocco aliwaomba Watanzania kutoenda uwanjani na matokeo yaliyopita bali sasa wako vizuri kulipiza kisasi kwa kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.

Tanzania kwa mara ya mwisho ilishiriki fainali za Chan zilipofanyika Ivory Coast 2009 ikiwa ni miaka 10 sasa, hivyo itataka mwaka huu iweke rekosi tena kwa kufuzi fainali hizo.

Fainali za kwanza za Chan zilifanyika mwaka 2009 na lengo la Shirikisho la Afrika (Caf) ni kutoa nafasi kwa wachezaji ambao hawajasajiliwa nje ya nchi zao na kuwawezesha kujitangaza.

No comments:

Post a Comment