Friday 3 November 2017

Naibu Waziri aridhishwa na maendeleo ya ujenzi TB III

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema ukusanyaji wa mapato unaofanywa kwa sasa ni muhimu kwani unaweza kuifanikisha Tanzania kuwa na uwezo wa kujenga miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa wakati alipotembea leo mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria au Terminal III la Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Alisema serikali inajenga awamu ya pili ya mradi huo kwa kutumia fedha za ndani, ishara ambayo ni nzuri, kwani inaonesha kuwa katika siku za mbele serikali itakuwa na uwezo wa kujenga miradi kwa kutumia fedha zake.

“Tunajenga mradi huu kwa fedha zetu za ndani, lakini pia kwa kushirikiana na wdau wengine, hii ni ishara nzuri kwamba sasa tunakokwenda tunao uwezo katika siku za usoni kuwa na miradi kama hii kwa fedha zetu,” alisema Kwandikwa.

Alisema kwa sasa hatua ya ujenzi wa mradi huo imefikia asilimia 66 na kwamba utakamilika Septemba mwakani na kwamba baada ya ujenzi huo kukamilika itakuwa ni picha ya kuelekea kwenye Tanzania mpya.

Kwandikwa alisema mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya Bam International imelipwa fedha zake na kwamba wizara inahakikisha mkandarasi huyo anapata haki yake kwa wakati.

“Nilitembelea kule KIA (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro), nikaona maendeleo ya ujenzi kule na nikaridhishwa, nikatamani nije hapa, lakini nimefika hapa pia nimeridhishwa na kasi ya ujenzi unaoendelea,” alisema.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi huo, Barton Komba alisema, mkandarasi wa ujenzi huo ameshalipwa fedha zake zote, hivyo kwa sasa hadai serikali na anafanya kazi yake vizuri.


“Mpaka mwezi wa tisa mwakani utakuwa umekamilika, lakini pia uwanja huu umezingatia watu wote hata ndugu zetu wenye mahitaji maalumu, n uwanja uliozingatia viwango vya kimataifa,” alisema Komba.




No comments:

Post a Comment