Saturday 11 November 2017

Nyota Kibao Kushiriki Tamasha la Karatu 2017

Na Mwandishi Wetu

NYOTA kibao wa riadha wanatarajia kushiriki mbio za kilometa 10 na zile za kilometa tano za wanawake na wanaume zitakazofanyika Desemba 23 mjini Karatu.

Mbio hizo pamoja na michezo mingine kama ya baiskeli, mpira wa wavu, soka, ngoma na kwaya zitakuwa ni hitimisho la Tamasha la Michezo la Karatu 2017.

Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo Meta Petro, mbio za mwaka huu zinatarajia kushirikisha wanariadha kibao nyota kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Alisema baadhi ya wanariadha hao watatoka katika taasisi za kijeshi, huku wengine wakitoka katika klabu za uraiani na sehemu mbalimbali katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Filbert Bayi

Tamasha hilo ambalo linaendeshwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) lilianza zaidi ya miaka 10 iliyopita na linafanyika Desemba ya kila mwaka.

Kwa mujibu wa Petro, tamasha hilo hasa mchezo wa mbio limekuwa na lengo la kuibua na kuuendeleza vipaji vya chipukizi ili kuwapata nyota wapya watakaochukua nafasi ya Bayi aliyewahi kuwa bingwa wa dunia wa mbio za meta 1500.

Mbali na meta 1500, Bayi pia aliwahi kutamba na kushikilia rekodi ya dunia ya mbio za maili moja na kutwaa medali ya fedha katika Michezo ya Olimpiki iliyofanyika Moscow, Urusi mwaka 1980.

Bayi ni mwenyeji wa Karatu mkoani Arusha na aliamua kuanzisha mbio hizo ili kupata vipaji vipya vitakavyomrithi yeye katika mchezo huo.


Meta Petro

Mbali na mbio za kilometa 10 na zile za tano, pia kutakuwa na mbio za watoto ambazo zitakuwa za kilometa 2.5.

No comments:

Post a Comment