Sunday 26 November 2017

Arusha Mabingwa wa Riadha ya Wanawake 2017

Wanariadha wakichuana katika mbio za meta 5,000 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
 Na Mwandishi Wetu
MKOA wa Arusha umekuwa bingwa wa kwanza wa mashindano ya taifa ya riadha yaliyomalizika jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Arusha walitawazwa mabingwa baada ya kumaliza wakiwa na medali mbili za dhahabu. Tatu za fedha na moja ya shaba, huku wenyeji Dar es Salaam walishika nafasi ya pili kwa kupata medali mbili za dhahabu na moja ya shaba.
Timu ya mkoa wa Kaskazini Pemba ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kupata medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na tatu za shaba.
Katika mashindano hayo yaliyofungwa jana na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida nafasi ya nne ilikwenda kwa mkoa wa Kaskazini Unguja iliyopata medali moja ya dhahabu na moja ya fedha.
Pwani walishika nafasi ya tano baada ya kupata medali moja ya dhahabu na moja ya fedha, huku Tabora wakimaliza wa sita kwa medali moja ya dhahabu na moja ya fedha.
Dodoma walimaliza wa saba wakiwa na medali moja ya dhahabu na moja ya shaba huku Kilimanjaro ikimaliza na medali moja ya dhahabu na kumaliza katika nafasi ya nane.
Kivutio katika ufungaji jana ilikuwa katika mbio za meta 5,000 wakati mwanariadha wa Mwanza, Silvia Masatu licha ya kukimbia akiwa peku, alitoka nyuma na kumshinda Amina Mohamed wa Arusha kwa kutumia dakika 17:52:00.
Mwanariadha wa Mkoa wa Ruvuma, Rose Seif akiruka chini katika mashindano ya taifa ya wanawake leo kwenye Uwanja wa Taifa.
Amina alimaliza wa pili baada ya kuongoza kwa muda mrefu na kumaliza mbio hizo kwa dakika 18:03:37 wakati Anastazia Dolimongo wa Shinyanga alimaliza watatu kwa dakika 18:06:50.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa udhamini JICA, lengo ni kuchagua timu ya taifa itakayosaka viwango vya kushiriko Olimpiki ya 2020 Tokyo.


Wanariadha wa mchezo wa kuruka chini wakipewa maelekezo kabla ya kushiriki katika mchezo huo leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment