Sunday, 12 February 2017

Cosafa yamuunga mkono rais wa soka madagascar kumpinga Hayatou katika urais wa Caf Machi



JOHANNESBURG, Afrika Kusini
BARAZA la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) limesema litamuunga mkono Ahmad Ahmad (pichani) katika uchaguzi ujao wa kiti cha urais katika Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).

Ahmad, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa Chama cha Soka cha Madagascar, tayari alishatangaza nia yake ya kumpinga kiongozi wa muda mrefu wa Caf Issa Hayatou katika uchaguzi utakaofanyika Machi nchini Ethiopia.

Cosafa ilitangaza msimamo wake huo wa kumuunga mkono Ahmad kufuatia mkutano wa marais wa vyama vya soka vya nchi za kusini mwa Afrika uliomalizika jijini hapa Jumamosi.

Katika taarifa yake, Cosafa ilitangaza kuwa watamuunga mkono kwa asilimia 100 mjumbe wao huyo katika uchaguzi wa Caf na Fifa, Shirikisho la Kimataifa la Soka.

"Huu ni mkutano wetu wa kwanza tangu kamati mpya ya utendaji ilipochaguliwa na tunafurahi na maamuzi yaliyochukuliwa na Barazala ambao utabadili sura ya soka katika ukanda wetu, “alisema Rais wa Cosafa Phillip Chiyangwa.

Issa Hayatou, ambaye amekuwa rais wa soka la kiafrika tangu mwaka 1988, anasaka kuongoza kipindi cha nane Caf.

Mcameroon huyo alichaguliwa tena bila kupigwa wakati wa uchaguzi wa mwisho uliofanyika mwaka 2013.

Awali alitangaza kuwa kipindi hiki kitakuwa cha mwisho kwake hadi pale walipobadilisha taratibu.

Mwaka 2015, Caf ilipiga kura kubadili utaratibu, ambapo viongozi hawaruhusiwi kugombea endapo watakuwa na zaidi ya umri wa miaka 70.

No comments:

Post a Comment