Tuesday 17 March 2020

BMT yapongeza Kilimanjaro Premium Lager kwa Udhamini


Mshindi wa mbio za Kilometa 42 za Kilimanjaro Marathon 2020, Kiplagat akimaliza mbio hizo Moshi hivi karibuni.
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limesema Kilimanjaro Premium Lager ni mfano pekee wa kuigwa katika udhamini wa mchezo wa riadha hapa nchini.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro, imekuwa mdhamini mkuu wa mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon mfululizo toka zilipoanzishwa hadi sasa zinatimiza miaka 18.

Kauli hii inakuja siku chache baada ya kumalizika mbio maarufu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2020 mjini Moshi ambazo zilihusisha washiriki zaidi ya 11,000 na idadi kama hiyo ya watazamaji.

Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha, ambaye alishuhudia msimu wa 18 Kili Marathon Machi Mosi mwaka huu, aliwapongeza wadhamini hao huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kudhamini mashindano mbalimbali katika kukuza mchezo wa Riadha Tanzania.

Msitha, alisema kwa miaka yote hiyo 18 kumekuwa na mabadiliko makubwa Kilimanjaro Marathon na leo limekuwa tukio kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo Kilimanjaro Premium Lager wanapaswa kupongezwa na kuigwa na wengine pia.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla akikabidhi hundi kwa mshindi wa mbio za Km 42 upande wa wanawake, Lydia Wafula (kulia) huku Mkurugenzi wa Masoko wa TBL Group, Doreen Tumubeebire akishuhudia. Kilimanjaro Premium Lager imekuwa mdhamini wa mbio hizi kwa miaka 18 sasa.
Aliongeza kuwa, mashindano kama hayo husaidia pia kuleta umoja kwa jamii.

“Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali wanaohitaji kutoa udhamini katika matukio kama haya, kujitokeza kwani husaidia katika kuleta umoja wa kipekee kwa jamii,” alisema.

Hivi karibuni, BMT ililiagiza Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kupunguza tozo kwa waandaaji wa mbio za barabarani kutoka Sh. Milioni 3 hadi Sh. Milioni 1.5 ili kuwasaidia waandaaji katika kuandaa matukio yenye uhakika.

Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi amewashukuru watanzania na washiriki wote kwa kujitokeza kwa wingi katika mbio za mwaka huu ambapo namba za mbio za km 42 na 21 ziliisha mapema kabla ya muda wa mwisho uliotangazwa.

“Hii ni dhahiri kuwa mbio hizi zimekuwa maarufu sio nchini tu ila hata nje ya nchi ndio maana sisi kama wadhamini tumekuwepo kwa miaka 18 sasa tangu mbio ghizi zianzishwe,” alisema.

Wadhamini wengine waliofanikisha mbio za mwaka huu ni TPC Limited, Simba Cement, Unilever, Absa Bank Tanzania Limited na watoa huduma rasmi ni Kibo Palace Hotel, Keys Hotel, GardaWorld Security, Precision Air na CMC Automobiles.
  

No comments:

Post a Comment