Thursday 7 June 2018

Simba, Gor Mahia Kucheza Fainali ya SportPesa Cup

Wachezaji wa Simba wakishangilia baada ya kuifunga Kakamega Home Boyz kwa penalti 5-4.

Na Mwandishi Wetu, Nakuru
TIMU ya soka ya Simba leo imekata tiketi ya kucheza fainali ya mashindano ya SportPesa Super Cup baada ya kuifunga Kakamega Home Boyz kwa penalti 5-4, katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa Afraha mjini hapa.

Ushindi wa mabingwa hao wapya wa Tanzania Bara, haukuwa rahisi kwani walihitaji kutoka jasho na damu baada ya vijana wa Kakamega kuwang’ang’ania na kulazimisha suluhu hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika na kufanya mchezo hu kwenda katika matatu.

Waliofunga penalti za Simba Sports jana ni Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Shiza Kichuya na Jonas Mkude, wakati penalti ya mwisho ya Kakamega iliota mbawa baada ya mpigaji kupaisha.

Simba SC sasa Jumapili katika fainali na bingwa wa Kenya na mshindi wa mwaka jana wa SportPesa Super Cup, Gor Mahia baada ya jana kuifunga Singida United 2-0.

Ikumbukwe mchezo wa kwanza pia Simba ilipenya kwa matuta, ikishinda kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 0-0 dhidi ya Kariobangi Sharks nayo ya Kenya, kabla ya kuendeleza ushindi wa staili hiyo mbele ya Kakamega iliyowatoa Yanga  ya Tanzania pia kwa kuwachapa 3-1.

Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup 2018 itafanyika Jumapili na mshindi pamoja na kupata dola za Marekani 30,000 pia atapata nafasi ya kwenda kucheza na klabu ya Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park mjini Liverpool, England.

Mshindi wa pili atajipatia dola za Marekani 10,000, wa tatu dola 7, 500 na wa nne dola za Marekani 5,000 wakati timu nyingine zitapewa kifuta jasho cha dola 2,500.

Bingwa mtetezi ni Gor Mahia ambayo mwaka jana iliifunga AFC Leopards 2-1 katika fainali Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na mbali na dola na Kombe, pia ilipata nafasi ya kucheza na Everton kwenye uwanja huo.

No comments:

Post a Comment