Thursday 16 February 2017

MSHINDI wa pili wa shindano la insha la DStv Eutelsat 2017 akabidhiwa cheti chake



Meneja Masoko wa Multichoice-Tanzania, Alpha Mria (kulia) akimpongeza mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya wavulana ya Feza, Davids Bwana kabla hajamkabidhi cheti chake cha ushindi wa pili wa uandishi wa Insha katika shindano la Afrika lililofanyika hivi karibuni Lagos, Nigeria.


Na Mwandishi Wetu
MSHINDI wa pili wa shindano la insha la DStv Eutelsat 2017, Davids Bwana jana alikabidhiwa rasmi cheti chake kutoka kwa MultiChoice-Africa.

Bwana ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya wavulana ya Feza, alikabidhiwa cheti hicho shuleni hapo jana na meneja masoko wa MultiChoice-Tanzania, Alpha Mria mbele ya waalimu, baadhi ya wanafunzi na mama yake mzazi, Dk Esther Mbutolwe.
Davids Bwana akiwa na mama yake mzazi, Dk Esther Mbotolwe mara baada ya kijana huyo kukabidhiwa cheti chake jana.
Baada ya kukabidhiwa cheti hicho, Bwana alisema anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kupata nafasi hiyo ya pili kutokana na jitihada kubwa alizofanya.



Alisema haikuwa rahisi kupata nafasi hiyo kwani kulikuwa na changamoto nyingi kutoka kwa washindani wenzake, ambao baadhi yao walimkatisha tamaa kuwa hawezi kushinda.


Bwana ameshika nafasi ya pili katika uandishi wa insha nyuma ya Muethiopia, Leoul Mesfin huku Tanzania ikiwa nchi pekee ya Afrika Mashariki iliyoshika nafasi ya juu.
 

Kwa ushindi huo, Bwana atapata fursa kufanya ziara nchini Afrika Kusini kutembelea ofisi za MultiChoice pamoja na Shirika la Anga la Afrika Kusini.


Katika shindano hilo, mwanafunzi alitakiwa kuandika insha inayoeleza elimu ya anga, hasa masuala ya satelaiti na jinsi ambavyo ingeweza kulisaidia bara la Afrika.

Mkurugenzi wa shule za Feza, Ibrahim Rashid (kulia) akiwa na Bwana.
MultiChoice-Tanzania kupitia meneja masoko wake ilisema kuwa imefurahishwa na ushindi huo na itaendelea kuwashindanisha wanafunzi katika mashindano mbalimbali.


Naye Mkurugenzi wa shule za Feza, Ibrahim Rashid alisema wamefurahishwa na ushindi huo kwani Bwana ameongeza tuzo za kimataifa katika kabati la shule hiyo.
Alisema shule hiyo ilikuwa na tuzo 19 za kimataifa na baada ya ushindi wa mwanafunzi huyo, sasa zimefikia 20.
Naye mama wa mwanafunzi huyo, aliwataka wazazi wenzake kuwapa fursa watoto wao ili waweze kuonesha vipaji vyao badala ya kuwabana.

Alisema wazazi wanatakiwa kuwa karibu na watoto wao na kuwasaidia katika ukuaji wao kitaaluma kwani huo ndio urithi mzuri kuliko kitu kingine.


1 comment:

  1. Mbutolwe Esther Mwakitalu16 February 2017 at 04:46

    Congratulations Davids

    ReplyDelete