Wednesday, 21 December 2016

Ukata waifanya Temeke kuutema ubingwa taifa Cup bila kuingia dimbani, wamkumbuka Mbunge wao wazamani Mtevu


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKATI mashindano ya taifa ya netiboli yanatazamiwa kuanza Desemba 30 kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, mabingwa watetezi Temeke wameutema ubingwa huo hata kabla ya kuingia dimbani kwa sababu ya ukata.

Mashindano hayo yanashirikisha timu za mikoa, huku Halimashauri za Temeke, Ilala na Kindondo mkoani Dar es Salaam, kila moja ikipewa hadhi ya mkoa katika mashindano hayo yanayofanyika  kila mwaka.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania, Chaneta, Zainab Mbiro amesema leo kuwa mikoa ya Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Manyara, Arusha, Mara, Morogoro, Simiyu na Singida imethibitisha kushiriki  katika mashindano hayo.

Mbiro ambaye ni Mkuu wa Wilaya mstaafu alisema kuwa,  Dar es Salaam akiwa na maana Halimashauri zake zote tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni, hakuna iliyothibitisha kushishiriki katika mashindano hayo.

Katibu Mkuu wa timu ya Temeke, ambayo ndio bingwa mtetezi, Amina Mussa amethibitisha leo kuwa, ukata umewafanya washindwe kuthibitisha kushiriki mashindano hayo,  licha yao kuwa mabingwa watetezi.

Temeke imelitwaa taji hilo kwa mara tatu mfululizo na kama ingeshiriki mwaka huu na kulibeba, ingekuwa imelitwaa kwa mara ya nne mfululizo.

Amina alisema kuwa pamoja na jitihada zao kupeleka barua kwa mbunge wa Temeke, Meya na naibu Meya, lakini hadi sasa barua zao hazijajibiwa lolote na wamepoteza matumaini ya kusaidiwa na watu hao.

Alisema kuwa Mbunge aliyepita wa Temeke, Zuberi Mtemvu ndiye alikuwa mlezi wa timu hiyo na aliisaidia sana katika maandalizi yake na kuhakikisha inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.

Alisema kuwa timu yao tangu Mtemvu ashindwe Ubunge imekuwa ikitapatapa, ambapo ilishindwa kushiriki hata mashindani ya Ligi Daraja la Kwanza yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro na hawajui hatma yao kama watashushwa daraja kwani walishindwa hata kulipia ada.

“Viongozi hao tuliwaandikia barua ya kuwajulisha kuhusu mashindano hayo ya Morogor, lakini hadii hii leo tunaongea na wewe hakuna majibu na hatujui hatma yetu kama tutashushwa daraja au kufungiwa, “alisema Amina na kungeza:

“Tangu Mtemvu atoke madarakani Temeke tumekuwa watu wa kusuasua katika michezo,  kwani viongozi wetu wa sasa wako kimya kabisa hawajasema lolote.”

Amina aliwaomba wafadhili mbalimbali kujitokeza ili kuisaidia timu hiyo ambayo bado inaendelea na mazoezi kila siku na wako tayari kwa mashindano mbalimbali yatakayojitokeza.

No comments:

Post a Comment