Friday, 23 December 2016

Yanga yasimamishwa na African Lyon yashindwa kurejea kileleni, Simba wenyewe kesho dhidi ya JKT RuvuNa Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo wameshindwa kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na timu iliyopanda daraja ya African Lyon katika kipute kilichopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mchezo huo wa leo, Yanga ilikuwa na pointi 36 huku watani zao Simba wakiwa pointi 38, mbili zaidi ya wenzao hao na kama Vijana hao wa Jangwani wangeshinda mchezo huo wa leo, basi wangekalia kiti cha uongozi japo kwa muda kabla ya Simba kesho Jumamosi kukutana na JKT Ruvu kwenye Uwanja huohuo wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Endapo Simba itashinda kesho, basi itafikisha jumla ya pointi 41 wakati Yanga wakiwa na pointi zao 37, hivyo watakuwa wamepitwa kwa pointi nne na kuzidi kujiweka katika wakati mgumu wa kutetea taji lao hilo.

Athari za Mgomo?
Wengi wanajiuliza kama kweli matokeo hayo ya sare dhidi ya timu iliyopanda daraja ni athari za mgomo wa wachezaji wa timu hiyo hivi karibuni wakidai fedha zao za mishahara?

Wachezaji wa timu hiyo ndio wanajua siri ya matokeo ya mchezo huo kama ni matokeo halalai au ni moja ya njia za kuushinikiza uongozi wa timu hiyo kuwalipa fedha zao katika kipindi hiki cha Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.

 
Yana ilishindwa kupata mabao baada ya kocha wao mpya, Mzambia George Lwandamina kuljaza viungo watano, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Said Juma na Deus Kaseke akitumia mshambuliaji mmoja tu, Amissi Tambwe.

Yanga walilisakama lango la Lyon kuanzia dakika ya tatu baada ya Tambwe kupiga kichwa vizuri akimalizia krosi ya Msuva, lakini mpira ukaenda juu kidogo na dakika ya 33 Niyonzima akapiga juu ya kuikosesha timu yake bao la wazi.

 Lyon ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Ludovic Venance aliyefunga katika dakika ya 67 akiunganisha pasi ya Abdallah Mguhi ‘Messi’.
 
Venance aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Mbao FC ya Mwanza, alifunga bao hilo baada kuingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awadh Juma.

Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani Yanga walifanikiwa kusawazisha dakika ya 74 kupitia kwa mkali wake mabao, Amissi Tambwe akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia Juma Abdul.

Wakati huohuo, ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa Simba kucheza na JKT Ruvu, huku Mbeya City ikiwa mwenyeji wa Toto Africans ya Mwanza, Stand United itacheza na Kagera Sugar, Ndanda FC itakwaana na Mtibwa Sugar, Majimaji dhidi ya Azam FC, Mwadui watakwaana na Mbao  FC wakati Ruvu Shooting wenyewe watacheza Jumatatu dhidi ya Mwadui.

No comments:

Post a Comment