Thursday 29 October 2015

Diamond kumsindikiza mkali Wizkid wa Nigeria Jumamosi


Muimbaji Nassib Abdul au Diamond akiimba wakati wakati wa mazoezi kwenye ukumbi wa King Solomon uliopo Namanga jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kutumbuiza na Wizkid wa Nigeria Jumamosi.


Na Mwandishi Wetu
MSANII wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul, Diamond Platinum ataimba jukwaa moja na msanii mahiri kutoka Nigeria, Wizkid katika tamasha litakalofanyika katika viwanja vya Leaders Kinondoni Jumamosi.

Akizungumza na waandishi wa habari mratibu wa onesho hilo, Solomon Nassuma alisema kuwa, msanii huyo atawasili Ijumaa mchana tayari kwa shoo hiyo.

Alisema kuwa tiketi za viti maalum ndio zimeshaanza kuuzwa katika vituo mbalimbali kama vile katika migahawa yote ya Eaters Points iliyopo Oysterbay na Namanga, Onetash, migahawa yote ya KFC pamoja na hotel ya Rainbow Mbezi. 

Aliongeza kuwa kwa wale watakaokata viti maalum kutakuwa na magari kwa ajili kuwachukua kutoka maeneo mbalimbali ambapo watakuwa wameegesha magari yao.

Alisema kuwa maeneo hayo ni katika eneo la ukumbi wa King Solomon Hall na mgahawa wa Eaters point Oysterbay yatawabeba na kuwapeleka moja kwa moja ukumbini na kisha kuwarudisha tena kwenye magari yao baada ya kumalizika kwa onesho.

"Hii inatokana na ukweli kwamba hawa watu wa VIP tunataka wafurahie fedha zao za kiingilio kwa kuwa wamekata fedha kubwa na inatakiwa kuhakikisha kuwa wanafurahia shoo pia" alisema Nassuma.

Aliongeza: "Kwa tiketi nyingine za kawaida zitaanza kuuzwa siku hiyo hiyo ya shoo na naomba wananchi mbalimbali kujitokeza kushuhudia kwani tayari zoezi la Uchaguzi Mkuu lilishamalizika.

Aliongeza kuwa pia watakuwa wasanii wengine kama vile Christian Bella pamoja na Farid Kubanda, Fid Q na wengine.
Baadhi ya madansa wa Diamond wakifanya mazoezi katika ukumbi wa King Solomon jana kwa ajili ya onesho la Jumamosi.
Meneja wa Diamond, Babu Tale alisema kuwa shoo hiyo imekuja wakati mzuri, ambapo Diamond ameshinda tuzo nyingi na tangu ashinde tuzo hizo hajawahi kufanya shoo hapa nchini, na hiyo itakuwa ya kwanza kwake.

"Hii inakuwa ni shoo ya kwanza ya Diamond tangia ashinde tuzo hizo na kwanza inakuwa ni shoo ya live sasa hayo ni mafanikio makubwa na wananchi wataona shoo hiyo wakati wakiwa ndio kwanza wametoka kwenye uchaguzi mkuu" alisema Tale.

Diamond ambae kwa sasa ni mmoja kati ya wasanii wakubwa barani Afrika ambapo ameshinda tuzo ya msanii bora wa Afrika Mashariki na Afrika katika tuzo za Afrima zilizofanyika Marekani huku akiwa pia ni mshindi wa tuzo ya msanii bora wa Afrika ya MTV EMA.

No comments:

Post a Comment