Friday, 16 October 2015

Jembe Deo Filikunjombe vilio kila kona
Aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, deo Filikunjombe katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
Na Waandishi Wetu
MGOMBEA ubunge wa CCM katika Jimbo la Ludewa mkoani
Njombe, Deo Filikunjombe amekufa katika ajali ya helikopta iliyotokea mkoani Morogoro juzi.

Kwa mujibu wa gazeti la Habari Leo la leo Jumamosi, mbali na Filikunjombe, ajali hiyo pia imesababisha kifo cha Kapteni wake, William Silaa, ambaye ni baba wa mgombea ubunge wa Ukonga kupitia CCM, Jerry Silaa na abiria wengine wawili ambao hawajatambulika.

Uthibitisho wa vifo hivyo umetolewa jana alasiri na Kamishina wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, ambaye alikwenda katika eneo la tukio ambako walifanikiwa kutambua mwili wa Filikunjombe na Kapteni Silaa.

*Taarifa za awali
Taarifa kuhusu utata wa ajali ya helikopta hiyo, zilisikika kuanzia juzi saa tatu usiku na kusambaa kwa kasi katika mitandao ya simu kuanzia jana asubuhi.

Kwa mujibu wa taarifa za juzi, helikopta hiyo ilikuwa imepoteza mawasiliano ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Selou, ambayo ndiyo hifadhi ya wanyama iliyo kubwa kuliko zote duniani.
Hata hivyo, taarifa za jana asubuhi zilieleza kuwa helikopta hiyo, huenda ilipata ajali na kuwaka moto, lakini hakukuwa na taarifa sahihi kuhusu majaliwa ya abiria.

Miongoni mwa waliothibitisha ajali hiyo, alikuwa Jerry  ambaye pia ni Meya wa Ilala aliyemaliza muda wake. Yeye kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii alithibitisha kutokuwa na mawasiliano na baba yake tangu juzi alasiri mpaka jana saa tano asubuhi na kushauri wananchi kuwa watulivu, wakati timu ya uokoaji ikifuatilia chombo hicho.

*Uthibitisho 
Muda mfupi baada ya kutaka wananchi watulie kusubiri kazi ya timu ya uokoaji, Jerry alituma ujumbe katika akaunti yake ya instagram, akithibitisha kutokea kwa msiba huo.

Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji kwamba imefanikiwa kufika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha.

Nimepoteza baba na rubani mzuri wa nchi yetu, Kapteni William Silaa, nimepoteza rafiki na kiongozi wangu Mheshimiwa Deo Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndugu zao nawaombea marehemu mapumziko ya amani, alisema Silaa katika taarifa hiyo.

Pia aliwashukuru wote walioshirikiana na familia kusaidia uokozi, akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Adelhem Meru na  Kampuni aliyoitaja kwa jina la Everest kwa kazi waliyofanya ya kutafuta waathirika wa ajali hiyo.

*Kabwe Zitto
Mwingine aliyezungumzia msiba huo ni mgombea ubunge wa Kigoma Mjini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto, aliyekuwa rafiki wa karibu wa Filikunjombe, ambaye asubuhi alitoa taarifa ya kwenda katika eneo la ajali.

Nimepoteza rafiki. Nimepoteza ndugu. Nimepoteza mtu mtiifu kabisa kuwahi kuwa naye. Sina ya kueleza. Mungu ana mipango yake. Ndugu yetu, rafiki yetu na mzalendo mwenzetu Deo Filikunjombe, ametutoka katika ajali ya helikopta. Nawasihi tuwe na utulivu wakati huu mgumu, alisema Zitto.

*January Makamba
Naye Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba, alianza kuelezea msiba huo kwa kutaja watu walioanza kampeni pamoja katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, ambao leo hawapo naye.

Alimtaja Mohamed Mtoi, mgombea ubunge wa Lushoto kupitia Chadema, ambaye alikufa mwanzoni mwa kampeni za uchaguzi huu kwa ajali ya gari na kufuatiwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa Ulanga Mashariki kupitia CCM na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, ambaye alifariki hivi karibuni nchini India alikokuwa akiuguzwa.

Makamba pia amemtaja mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Estomih Mallah (ACT-Wazalendo), aliyefariki Jumamosi iliyopita baada ya kuugua ghafla na mgombea ubunge wa Handeni Mjini kupitia CCM, Dk Abdallah Kigoda na Waziri wa Viwanda na Biashara, aliyefariki mwanzoni mwa wiki hii nchini India na kuzikwa juzi mkoani Tanga.

Taarifa hiyo ya Makamba, pia ilimtaja Dk Emmanuel Makaidi, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa na mgombea ubunge wa Masasi kupitia NLD, ambaye amefariki juzi na anatarajiwa kuzikwa jijini Dar es Salaam Jumanne katika makaburi ya Sinza.

Tulianza nao kampeni, leo hatunao. Mungu waweke na watakatifu mbinguni. Zipe nguvu familia zao. Siku mbili zilizopita niliongea kwa kirefu na Deo kuhusu mikakati. Nimepoteza rafiki na ndugu. Mungu amrehemu na pole kwa familia za wafiwa.

Nimetoka kupokea taarifa inayothibitisha kwamba chopa aliyokuwa amekodi ndugu yetu Filikunjombe, imeanguka na watu wote wamefariki, alisema Makamba katika taarifa yake kwenye akaunti ya Tweeter. 

*Mamlaka ya Anga
Taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana jioni, ilieleza kuwa abiria wengine waliokufa katika ajali hiyo ni Kasablanka Haule na Egid Mkwela.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, helikopta hiyo iliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) juzi saa tisa alasiri na ilitarajiwa kufika Njombe saa 12 na dakika 20 jioni.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kituo cha mawasiliano cha JNIA (ACC) kilipokea taarifa ya ajali hiyo saa 11:54, kutoka kwa mtumishi wa TCAA, ambaye alipewa taarifa na mtumishi wa Flight Link, ambaye alipigiwa simu na shuhuda wa ajali hiyo.
 
Kwa mujibu wa shuhuda huyo aliyekuwa katika vitalu vya uwindaji vya hifadhi hiyo, helikopta hiyo ilionekana ikianguka huku ikiwaka moto.

Baada ya taarifa hiyo, imeelezwa kuwa timu ya uokoaji ilikutana juzi usiku kujiandaa na jana alfajiri iliondoka kwenda eneo la tukio, kwa kushirikiana na Kampuni ya Ndege ya Everet ya Jijini Dar es Salaam, ambako walikuta miili ya marehemu hao na kuisafirisha kwenda jijini Dar es Salaam. 

 *Rambirambi za Magufuli
Mgombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli, ameelezea kupokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za vifo vya Filikunjombe, Kapteni Silaa na abiria wengine wawili ambao wameaga dunia katika ajali hiyo.


Katika salamu hizo za rambirambi ambazo amewatumia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga na Meya wa Manispaa ya Ilala Mstahiki Jerry Silaa, Dk Magufuli amesema:


Kwa hakika, nimeshitushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya ndugu Filikunjombe na ndugu Silaa ambavyo nimetaarifiwa kuwa vimetokea kwa ajali ya helkopta aliyokuwa akiitumia ndugu Filikunjombe kwa Kampeni zake za ubunge katika jimbo hilo la Ludewa.

  Kama unavyojua, namfahamu vizuri ndugu Filikunjombe. Alikuwa mbunge mwenzangu katika Bunge lililomaliza muda wake mwaka huu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka mitano ndani ya bunge letu.

Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu

kwa wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Ludewa, ambao aliwawakilisha kwa miaka mitano iliyopita akiwa Mbunge wao.

Hata nilipofanya ziara ya kampeni katika Jimbo lake la Ludewa mwezi uliopita, nililala nyumbani kwake, hiyo inaonesha nilivyokuwa karibu naye. Tutakosa utumishi wake mahiri sana, alisema.

Salamu zake za rambirambi  kwa Meya Silaa, Dk Magufuli amesema;

"Nimesikitishwa sana na taarifa ya kifo cha baba yako Kapteni William Silaa, kwani ni tukio lisilozoeleka. Ni jana tu nimeshiriki nawe katika kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 katika jimbo unalogombea ubunge, jimbo la Ukonga, naungana nawe katika kipindi hiki kigumu cha msiba mkubwa. Nakupa pole wewe binafsi, familia yenu, ndugu, jamaa na marafiki wote".

 Nakutumia wewe ndugu Sanga, Mwenyekiti wetu wa CCM Mkoa wa Njombe salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha ndugu Filikunjombe na abiria hao wengine.

Kupitia kwako namtumia rambirambi nyingi kwa Spika wa

Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anna Semamba Makinda na wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao, amesema katika taarifa hiyo.

Dk Magufuli amemuomba Makinda pia umfikishie salamu za rambirambi kwa wananchi wa jimbo na wilaya ya Ludewa ambao wamepoteza mbunge wao aliyewatumikia kwa ustadi mkubwa kwa kipindi chote.


Pia Dk Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Filikunjombe kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao mpenzi.

 Amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu ya uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi na aziweke pema peponi  roho ya Filikunjombe na Kapteni Silaa.

No comments:

Post a Comment