Wednesday, 13 November 2019

Viwanja vya Ndege Nchini Kutumika Majira Yote

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bahati Mollel akiwakaribisha waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali (hawapo pichani) kusikiliza Mafanikio yaliyofikiwa na TAA kwa kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).


Na Bahati Mollel,TAA
VIWANJA vya Ndege Tanzania sasa vinaweza kutumika majira yote ya mwaka ya masika na kiangazi kutokana vingi barabara zake za kutua na kuruka ndege kujengwa kwa kiwango cha lami, imeelezwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi, Mhandisi Mbila Mdemu ametoa maelezo hayo leo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), alipozungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, wakati alipozungumzia mafanikio ya Mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Kaimu Mwanasheria wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Pamela Mugarula akizungumzia muundo na kazi za TAA mbele ya waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari (hawapo pichani) leo wakati Mamlaka hiyo ilipozungumzia Mafanikio iliyofikia kwa kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).



 Mhandisi Mdemu amesema Mamlaka inajivunia mafanikio ya kuwa na viwanja 16 vyenye barabara za kutua na kuruka ndege za kiwango cha lami, ambazo zinaruhusu kutumika kwa kipindi chote cha mwaka bila matatizo ya aina yeyote.

Viwanja hivyo ni Arusha, Tabora, Mwanza, Bukoba, Mafia, Iringa, Songwe, Tanga, Moshi, Songwe, Kigoma, Dodoma, Mtwara, Mpanda pamoja Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA). 

“Tangu kuanzishwa Mamlaka vilikuwepo viwanja nane pekee vyenye viwango vya lami, lakini sasa mpaka Novemba mwaka 2015 tumeweza kuongeza na kufikisha 16 ambavyo vinapitika kwa uhakika zaidi katika majira yote ya mwaka ya kiangazi na masika,” amesema Mhandisi Mdemu.

Mbali na barabara za kutua na kuruka ndege, pia Mamlaka hiyo imefanikiwa kufanya ukarabati na upanuzi wa majengo ya abiria na kufanikisha kuweza kuhudumia abiria wengi zaidi ya wa awali, ambapo ni pamoja na jengo la tatu la abiria la JNIA, Bukoba, Dodoma, Iringa, Mpanda, Mtwara na Mwanza.
Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),  Mhandisi Mbila Mdemu akizungumzia mafanikio ya TAA kwa kipindi cha Miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli, katika mkutano na waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari (hawapo pichani) uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).


Pia Mhandisi Mdemu amesema mafanikio mengine ni kuboresha ulinzi wa kutosha wa abiria na mizigo, kwa kufungwa kamera za kufuatilia matukio, kuwepo kwa mashine za kukagua abiria na mizigo na kujengwa kwa uzio kwenye baadhi ya viwanja,; pia kumefungwa mifumo ya kisasa ya kiyoyozi; na  kuanza kusimikwa kwa taa za kuongoza ndege ili ziweze kutua usiku.

Naye Meneja Mipango na Takwimu wa TAA, Asteria Mushi amesema kuwa Mamlaka imeweza kupata mafanikio kwa kuongeza mapato kutoka Tshs. Bil. 63 kwa mwaka 2015 na kufikia Bil. 105 kwa mwaka 2018, ambazo ni ongezeko la asilimia 66, ambapo lengo la Mamlaka ni kuongeza mapato na kufikia Tshs. Bil. 130 ifikapo mwaka 2020; pia wameweza kuongeza biashara za maduka na sasa serikali wanashirikiana na taasisi binafsi kujenga hoteli ya nyota nne yenye ghorofa nane (8) itakayojengwa karibu na jengo la pili la abiria (JNIA-TBII).

Hali kadhalika Mushi, amesema Mamlaka imeongeza idadi ya ndege za abiria ambazo awali zilikuwa zikifanya safari nchini, lakini baadaye zikasitisha na zimeanza tena safari hizo, ambazo ni Air Uganda na Zimbabwe. Ndege hizo zinafanya idadi ya ndege za nje kufikia 21.
Meneja wa Mipango na Takwimu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Asteria Mushi (kulia) leo akizungumzia ongezeko la mapato kwenye Viwanja vya ndege mbele ya waandishi wa habari wakati Mamlaka hiyo ilipoelezea mafanikio yake kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

“Katika viwanja vya ndege tumetenga asilimia 30 kwenye majengo ya abiria tumetenga huduma za abiria na biashara, lakini tunaangalia na ongezeko la ndege za Air Tanzania ambapo sasa zinakwenda njia 10 za ndani ya nchi na njia tano za kimataifa,” amesema Mushi.

Friday, 8 November 2019

Bombardier Nayo Kutua Kiwanja cha Arusha


Na Mwandishi Wetu
NDEGE aina ya Bombardier zitaweza kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Arusha baada ya kukamilika mpango wa kuongezwa barabara ya kutua na kuruka ndege, imeelezwa.

Hayo yalisema bungeni mjini Dodoma juzi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Issac Kamwelwe wakati akijibu swali la Mhe Husna Malima, Mbunge wa Kigoma Kusini aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Arusha ili ndege kubwa ziweze kutua.

Malima alisema kuwa kuongezwa kwa uwanja huo kutawawezesha wananchi wa mikoa ya Singida, Manyara, Simiyu, Mara na Dodoma kuamasika kutumia usafiri wa ndege, ambao unatosheleza kwa sasa?


Amesema mafaniko ya uwepo wa ndege nyingi za abiria nchini ni pamoja na ndege hizo kutumika kwa wananchi kuzipanda.

Kamwelwe amesema kurefushwa huko kutafanikisha ndege aina ya Bombardier ambayo inabeba abiria kuanzia 70 kutua na kuruka bila tatizo kwenye kiwanja hicho kilichopo Kisongo mkoani Arusha.


Amesema tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kazi hiyo, ambapo kiwanja hicho ni cha tatu nchini kwa kutua na kuruka ndege nyingi, ambapo hutua ndege zaidi ya 125 kwa siku.

“Tumeweka bajeti kuendeleza kiwanja cha ndege cha Arusha na tayari tenda imetangazwa, kiwanja hiki kinaongoza kwa kutua ndege nyingi zaidi kwa siku ni biashara kubwa na ndio maana tunataka ndege ya Bombardier itue hapo,” alisisitiza Mhe. Kamwelwe.

Amesema mikoa jirani na Arusha ya Manyara, Singida, Dodoma, Simiyu na Mara itafaidika na maboresho ya kiwanja hicho kwa kuwa wataweza kukitumia ipasavyo.

Naye Meneja wa Kiwanja hicho, Mhandisi Elipid Tesha amesema barabara ya kutua na kuruka ndege itaongezwa urefu kwa meta 200, ambapo sasa ina urefu wa meta 1600 na itakuwa 1800, na pia patajengwa eneo la kugeuza ndege.

Mhandisi Tesha amesema kwa sasa kazi inayoendelea ni ujenzi wa eneo la maegesho ya ndege (Apron), ambayo yakikamilika yatapunguza msongamano kwa asilimia 30; pia barabara ya kupita ndege kwenda katika maegesho (taxiway);  ujenzi wa maegesho ya magari yapatayo 350 kwa kiwango cha lami.

Pia ujenzi wa mfumo wa malipo ya maegesho hayo unaendelea sambamba na ule wa maegesho ya magari.

Pia amesema ujenzi huo wa maboresho ya kiwanja cha ndege cha Arusha utahusisha ujenzi wa eneo la kupumzika abiria, ofisi za waegesha ndege (mashellers), kibanda cha ulinzi na vyoo.

Monday, 4 November 2019

Mwakyembe Azindua Kili Marathon 2020 Awataka Wanariadha wa Tanzania Kuchangamkia Zawadi


Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za 18 za Kilimanjaro zitakazofanyika Machi mwakani,

Mwakyembe pia aliwataka wanariadha wa Tanzania kufanya maandalizi ya uhakika ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mbio hizo, ambazo ni kubwa zaidi hapa nchini na hushirikisha watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, ambazo zitafanyika mjini Moshi Machi mosi, 2020, mwakyembe alisema ni aibu kwa zawadi zote kwenda nje ya nchi, hivyo aliwataka wanariadha wa Tanzania kujiandaa vizuri ili kuhakiisha zawadi hizo zinabaki nchini.

Mwakyembe aliwapongeza wadhamini wa mbio hizo wakiongozwa na Kilimanjaro Premium, ambao hudhamini mbio za kilometa 42, Tigo (kilometa 21), Grand Malt (kilometa 5), ambazo ni mbio za kujifurahisha na hushirikisha watu wengi.

“Inatia moyo sana kuona kuwa Kilimanjaro Marathon sasa ina washiriki zaidi ya  11,000 kutoka nchi zaidi ya 56 kote duniani. Hili ni jambo zuri sana kwa taifa, kwani tunapata fedha za kigeni kutokana na matumizi yanayofanywa na wageni hawa nchini, ikiwemo utalii, “alisema.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, alitoa wito kwa washiriki wazalendo kuchangamkia zawadi zinazotolewa na Kilimanjaro Marathon badala ya kukimbilia kushiriki mbio za nje, ambazo zawadi zake ni ndogo.

 “Ni vizuri kwenda kupata exposure lakini tusiache zawadi nzuri nyumbani na kufuata hela ndogo huko nje wakati tunaweza kuzipata hapa hapa nchini, “alisema Mtaka.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, alisema tangu mashindano yaanze Kilimanjaro Premium Lager imewekeza hela nyingi sio tu kusukuma mauzo ambayo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini pia kutengeneza ajira na kuchangia uchumi kwa ujumla kupitia gharama za kuyatangaza, promosheni na masuala mengine ya kimasoko.

Naye Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema kampuni yake inajivunia kudhamini mbio za kilometa 21 kwa mwaka wa tano mfulululizo, ambayo ni sehemu ya mbio hizo. “Tunajivunia kuwa sehemu ya tukio hili kubwa ambalo linawaleta pamoja wanariadha wakubwa, “alisema.

Wadhamini wengine katika Kilimanjaro Marathon ni pamoja na Kilimanjaro Water, Barclays Bank, Simba Cement, TPC Sugar, Precision Air, Kibo Palace Hotel, Garda World Security, Keys Hotel na CMC Automobiles.

Kwa mujibu ya waandaaji wa Kilimanjaro Marathon-Wild Frontiers na Executive Solutions, usajili umeshaanza kwa mtandao kupitia www.kilimanjaromarathon.com.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na mwenyekiti na kaimu katibu mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Leodegar Tenga na Neema Msitha, kaimu msaijili wa michezo nchini, Mwita, Bodi ya Utalii na wadau wengine swa mchezo wa riadha.

TAA Kufanikisha Mazingira Bora ya Kujisomea Wanafunzi 1560

Skauti wa shule ya Sekondari ya Ilala (kushoto) akimvisha skafu mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule hiyo, Bi. Harieth Nyalusi, Kaimu Meneja Biashara na Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Julius Ndyamukama. Mahafali hayo yamefanyika hivi karibuni.



Na Bahati Mollel,TAA
WANAFUNZI 1560 wa shule ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam, watasoma kwa furaha baada ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kukubali kufanya ukarabati wa jengo la maktaba, ambalo ni chakavu.


Ahadi hiyo imetolewa hivi karibuni na Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa TAA, Harieth Nyalusi ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mahafali ya 11 ya shule hiyo, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama.

Nyalusi alisema kuwa Mamlaka inaunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli za kutoa elimu bure, ambapo sasa itaungana naye katika kukarabati chumba hicho cha maktaba, ili kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora, yatakayochangia kufanya vyema katika masomo yao na katika  mitihani ya kidato cha pili na yake ya kuhitimu kidato cha nne.

     Mwanafunzi Diana Seth wa shule ya sekondari ya Ilala (kulia) akionesha moja ya majaribio katika maabara ya Biolojia, wakati wageni waalikwa pamoja na mgeni rasmi wa mahafali ya 13 ya shule hiyo, Bi. Harieth Nyalusi kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania  (wa pili kushoto), akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama walipotembelea maabara hiyo.


“Pamoja na kuunga juhudi za Mhe. Rais pia ni sera ya taasisi yetu kutoa kwa jamii katika kusaidia kutatua changamoto zinazozibabili jamii hizo, hivyo kama Mamlaka tutasaidia kufanya ukarabati wa ndani wa jengo hilo ambalo limekuwa chakavu, linalosababisha ari ya kusoma kushuka,” amesema.

Pia alisema Mamlaka inatambua jitihada kubwa inayofanywa kwa kushirikiana kwa Walimu, wazazi na wanafunzi katika kuhakikisha shule inaboresha utoaji wa elimu bora na ufaulu wa wanafunzi wa mitihani yao ijayo kuongezeka.

Hatahivyo, ametoa wito kwa wahitimu wa kidato cha Nne 2019 kuhakikisha wanaweka nia thabiti ya kujiendeleza zaidi kwa wale watakaobahatika kuchaguliwa  kwenda kidato cha Tano na vyuo mbalimbali, na ambao hawatabahatika waangalie nyanja mbalimbali za elimu ili kujitengenezea wigo mpana wa uwezo wa utambuzi wa kubadilisha changamoto zinazoizunguka jamii kuwa fursa.

  Kaimu Meneja wa Biashara na Masoko  wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Harieth Nyalusi (aliyesimama), akiwakilisha salamu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama wakati wa mahafali ya 13 ya shule ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam, yaliyofanyika hivi karibuni.
“Ikumbukwe kuwa vijana ni hazina ya Taifa, hivyo napenda kuwasisitiza kuwa thamani yako kama kijana iko mikononi mwako, ishi kwa malengo, jitambue, jithamini, jilinde na ujitunze kwani wewe ni wathamani kuwa na Taifa linakutegemea,” amesema.

Akiizungumzia TAA, Nyalusi amesema imepewa jukumu la kusimamia na kuendeleza viwanja vya ndege 58 vilivyopo Tanzania Bara kati ya hivyo ni viwanja vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), ambavyo ndivyo milango mikuu ya kuingia nchini kwa kutokea nje ya nchi.

Amesema katika viwanja vya ndege kuna fursa mbalimbali za kibiashara, ajira rasmi na zisizo rasmi, ambapo amewataka vijana wanaohitimu kuzichangamkia ajira na fursa hizo pindi zitakapotangazwa.

Wanafunzi skauti wa shule ya sekondari ya Ilala wakionesha ukakamavu kwa kupasuliwa tofali kichwani katika sherehe za mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibu.


Kwa upande wa risala ya wahitimu, imeeleza kuwa shule hiyo iliyoanzishwa miaka 13 iliyopita pamoja na kufanya vyema kwenye mitihani yao ya taifa ya kumaliza kidato cha nne kila mwaka, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa vyoo vya wanafunzi, ambapo yapo matundu 18  kati ya 72 yanayohitajika; ukosefu wa maabara mbili za masomo ya Biolojia na Fizikia ambazo ujenzi wake haujakamilika.

Changamoto nyingine ni uchakavu wa majengo ya shule ikiwemo kuvuja kwa paa na ubovu wa sakafu madarasani; uchakavu wa rangi katika majengo yote ya shule; ukosefu wa chumba maalum cha watoto wa kike na wagonjwa pindi wapatapo matatizo wanapokuwa eneo la shule; ukosefu wa vifaa vya teknolojia na mawasiliano zikiwemo komputa, projeta, mashine za kurudufia na ‘printer’.

 Mmoja wa skauti wa shule ya sekondari ya Ilala ya Jijini Dar es Salaam akizuia pikipiki mbili kwa mikono na kichwa katika sherehe za mahafali ya 13 ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibuni.

Risala hiyo imeainisha pia changamoto za ukosefu wa jengo la ofisi za walimu, ambapo sasa wanatumia madarasa mawili kama ofisi jambo ambalo pia kumesababisha kuwe na upungufu wa madarasa; uchakavu wa maktaba na ukosefu wa vifaa muhimu ndani ya maktaba zikiwemo meza, viti, vitabu vya kiada na ziada, makabati; ukosefu wa kantini bora ya shule na ukosefu wa bwalo.
Mwanafunzi Salvatory Jeremia (kushoto), akipokea cheti cha kuhitimu kidato cha nne kutoka kwa mgeni rasmi Bi. Harieth Nyalusi, Kaimu Meneja Biashara na Masoko wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Julius Ndyamukama.  (Picha zote na Bahati Mollel wa TAA).
Pamoja na changamoto hizo, wahitimu hao wameahidi kufanya vyema katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha nne, ambapo kila mwaka ufaulu umekuwa ukiongezeka ambapo sasa umefikia asilimia 70.

   
Wahitimu wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari ya Ilala wakiimba wimbo wa kuwaaga wenzao pamoja na walimu katika mahafali yao yaliyofanyika hivi karibuni  jijini Dar es Salaam.


Sunday, 6 October 2019

MultiChoice yaanza maadhimisho ya wiki ya Wateja

Mkuu wa Huduma kwa Wateja wa MultiChoice Tanzania Ngwitika Mwakihesya  akimuelekeza mmoja wa wateja waliofika katika tawi la MultiChoice Mlimani City Aziz Makupa jinsi ya kupata huduma mbalimbali za DStv ikiwa ni sehemu ya maaadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja. Kushoto ni afisa wa huduma kwa wateja wa tawi hilo Vedastina Ishengoma. 

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya MultiChoice Tanzania imeanza maadhimisho ya wiki ya wateja, ambapo itaendesha shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa zawadi kwa wafanyakazi na wateja kwa muda wa mwezi mzima.

Mkuu wa huduma kwa wateja Ngwitika Mwakihesya amesema kuwa katika kipindi hicho, MultiChoice Tanzania itakuwa na matukio mbalimbali yenye lengo la kuiwezesha kuwasogelea wateja karibu zaidi na kufahamu kwa kina uzoefu wao wa kupata huduma za DStv.

‘MultiChoice inaamini kuwa wafanyakazi na wateja wetu ndiyo nguzo ya ustawi wetu hivyo katika kipindi hiki tutahakikisha tunawafikia na kuwasikiliza maoni yao na hili tunalifanya ili tuweze kuboresha zaidi huduma zetu na kumfanya mteja ajisikie kuwa yeye kweli ni mfalme,” alisema Ngwitika.

Aliongeza kuwa zoezi hilo litahusisha kuwazawadia wafanyakazi mbalimbali pamoja na wateja na pia kuwatembelea wateja wao maeneo mbalimblai ili kuwasikiliza na kupata maoni yao.
Mkuu wa Huduma kwa wateja wa MultiChoice Tanzania Ngwitika Mwakihesya (kushoto) na  Ofisa Uhusiano, Diana Ayo wakiwa na baadhi ya watoto waliofika na wazazi wao katika tawi la DStv Mlimani City mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Amesisitiza kuwa kutokana na uzito huo, zoezi la kutembelea wateja litafanywa kwa kushirikiana na uogozi wa kampuni hiyo “Zoezi hili la kuwatembelea wateja litafanywa kwa kushirikiana na viongozi hivyo hata mkurugenzi mwenyewe na timu yake ya Menejimenti wataenda kuwatembelea wateja” alisisitiza Ngwitika.

Wednesday, 25 September 2019

Messi Aumia Barca Ikishinda Kiduchu


BARCELONA, Hispania
LIONEL Messi alipata maumivu wakati akianza kwa mara ya kwanza msimu huu katika mchezo, ambao Barcelona ilipata ushindi kiduchu wa mabao 2-1 dhidi ya Villarreal kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Messi, ambaye alikuwa akiponya majeraha ya nyama za paja, alibadilishwa mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kujitonesha tena.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina, alianza mchezo wake wa 400 wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga alipiga mpira wa kona uliomkuta Antoine Griezmann aliyepiga kichwa juu ya mwamba, kabla Arthur hajafunga na kufanya matokeo kuwa 2-0.

Bao la kwanza la Barcelona lilifungwa katika dakika ya sita na Griezmann kabla Santi Cazorla hajaifungia Villarreal bao la kufutia machozi katika dakika ya 44.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Barca Ernesto Valverde alielezea maumivu ya Messi kuwa ni “tatizo dogo”, ambalo halitakawia kupona.

"Wakati kitu chochote kinapotokea kwa Messi, kila kitu kinasimama, sio tu uwanjani, lakini pia hata jukwaani mambo yanasimama, “alisema.

"Kama kuchukua tahadhari tuliamua kutofanya kitu hatari, kinadharia hakuna cha ziada, lakini kesho tutaona nini kinaendelea.”

Ingawa wako mbali na hali yao ya kawaida, kimsimamo Barcelona wamepanda hadi katika nafasi ya nne katika msimamo wa La Liga na kupunguza presha baada ya kuanaza msimu vibaya.

Baada ya maumivu, nahodha huyo wa Barca alipata matibabu nje ya uwanja kabla ya kuendelea hadi mapumziko.

Mshambuliaji huyo nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji Mfaransa wa Ousmane Dembele mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Kwingineko, timu iliyopanda daraja ya Granada ilishika usukani wa La Liga – wakiwa pointi sawa na Athletic Bilbao na Real Madrid – baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Real Valladolid.

Real Madrid jana ilitarajia kucheza dhidi ya Osasuna wakati Bilbao waliopo mkiani watachezaji dhidi ya Leganes.

Mamlaka ya Viwanjaj vya Ndege Yamaliza Kwa Kishindo Maonesho ya Utalii 2019 Mkoani Iringa

  Mhandisi Ibrahim Kibasa (kulia) akipata ufafanuzi kutoka kwa Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole (wapili kulia) wakati alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo, na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ali Hapi Wengine ni Robert Kisongo (kushoto) mkazi wa Iringa na Ofisa Masoko na Biashara wa TAA, Mbura Daniel.
  Wazee wa Kimila wa Mkoa wa Iringa kuanzia kulia Anthony Mbuta, Augustino Mkini na Kassian Ngenz wakiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), baada ya kutembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka hiyo, yaliyofungwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ali Hapi. Maonesho hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa, 
Mhandisi Astelius John (wa pili kushoto) akimpa maelezo mbalimbali yanayohusu viwanja vya ndege Tanzania vilivyopo chini ya serikali, Wingred Nkoma, wakati alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la mamlaka hiyo, yaliyofungwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ali Hapi kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.
    Maumivu Mdegela (mwenye koti) pamoja na watoto wake wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa Afisa Masoko na Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakati walipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini yaliyomalizika Septemba 22, 2019 kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa. Maonesho hayo yamefungwa na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Ali Hapi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ali Hapi  (wa kwanza kulia), pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mhe Richard Kasesela wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisiongole, wakati walipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Maonesho hayo yalifungwa na Hapi.

JAMAFEST, URITHI WETU WAPANDA MLIMA KILIMANJARO


Wawakilishi wa Matamasha ya JAMAFEST na URITHI FESTIVAL  kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro pamoja na wa Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuanza safari ya SIKU SITA kuelekea Kilele cha Uhuru Kama sehemu ya matukio ya Matamasha hayo yaliyozinduliwa na Makamu wa Rais ,Mama Samia Suluhu Hassan. (Na Mpigapicha Wetu).

Na Mwandishi Wetu, Moshi
WAWAKILISHI wanne kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika matamasha JAMAFEST na URITHI FESTIVAL wanaendelea na safari ya siku sita ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuelekea kilele cha Uhuru ikiwa ni sehemu ya matamasha hayo yaliyozinduliwa Jumapili na Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan.
Wanaopanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya matamasha hayo makubwa kwa nchi za Afrika Mashariki ni pamoja na Joel Acana kutoka nchini Uganda, Luca Waiganja kutoka nchini Kenya na Anita Brown wa Tanzania wakiwakilisha tamasha la JAMAFEST huku Jocktan Makeke akiwakilisha tamasha la Urithi Festival.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga washiriki hao, Mwakilishi wa Katibu Mkuu waWizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita alisema chanzo cha tamasha la JAMAFEST ni utekelezaji wa maelekezo ya sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kutaka Malikale na Utamaduni kutumika kama vivutio vya Utalii.
 “Sekretarieti ilizielekeza nchi wanachama  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2012 zihakikishe Malikale na utamaduni unatumika kama kivutio cha utalii ili uweze kutumika katika maendeleo ay nchi za afrika Mashariki,”alisema Mwita.
Alisema baada ya maelekezo hayo, sekretarieti ilianzisha tamasha la Sanaa na Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki likiwa tayari limefanyika katika majiji matatu; Kigali (Rwanda), Nairobi (Kenya), Kampala (Uganda) na sasa linafanyika Dar es Salaam Tanzania.
Kwa Tanzania, tamasha la JAMAFEST lilizinduliwa Jumapili sambamba na tamasha la URITHI FESTIVAL, tamasha ambalo liko kwenye ngazi ya kitaifa likiwa na maudhui kama ya tamasha la JAMAFEST.
Wakati Jamafest inaunganisha wana Afrika Mashariki na kutumika kama kivutio cha Utalii au zao la utalii, Urithi festival linafanya mambo hayo hayo kwa Tanzania, kamba unaunganisha Watanzania na inatumika kama zao la Utalii.
Mapema mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Victor Kitansi aliwakapongeza waratibu wa matamasha hayo kufanya uamuzi wa kutumia sehemu ya matukio kuwa ni kushiriki kupanda Mlima Kilimanjaro.
Tamasha la JAMAFEST ambalo hufanyika kila baada ya miaka miwili kuzunguka nchi wanachama linafanyika kwa muda wa siku nane huku Tamasha la Urithi Festiva likifanyika katika mikoa 12 ya Tanzania Bara kwa kila mkoa kuionesha kivutio ambacho kitatumika kama zao la Utalii.

Usalama Viwanja Vya Ndege Waimarishwa

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole (kushoto) akifafanua mambo mbalimbali yanayohusu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) walipotembelea maonesho ya Karibu Utalii Kusini, yanayofanyika kwenye viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeimarisha usalama kwa abiria, mizigo na wageni kwenye viwanja vyake vyote 58 inavyovisimamia.

Kaimu Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Lydia Mwenisongole amesema usalama huo ni pamoja na mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo, ambapo ukaguzi unafanywa kwa umakini na maafisa usalama waliothibitishwa (certified screeners) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

“Tunawakaribisha wageni wa ndani na nje ya nchi kutumia viwanja vyetu vya ndege kwani vina usalama wa uhakika, zikiwemo kamera za usalama, X-ray mashine na ukaguzi mwingine zaidi, ambazo zinafanikisha zoezi zima la usalama,” amesema Mwenisongole.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bahati Mollel akimpa maelezo Hamis Hassan alipotembelea banda la maonesho la Mamlaka hiyo la Karibu Utalii Kusini yanayofanyika kwenye Viwanja vya Kihesa-Kilolo mkoani Iringa.


Mwenisongole amesema pia tunatambua juhudi za serikali ya Awamu ya Tano, iliyopo chini ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kupitia TAA inampango wa kujenga uzio kwenye kiwanja cha ndege cha Iringa, ambapo zabuni imeshatangazwa ili kupatikana kwa mkandarasi wa ujenzi huo.

Pia amewaita wawekezaji kuwekeza kwenye viwanja vya ndege kwa kuwekeza kwenye maduka yenye bidhaa mbalimbali pamoja, hoteli na karakana za ndege.
Grace Sanga mkazi wa Kiwanja cha ndege, Dkt. G. Nyamubi wa Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Iringa alipotembelea banda la maonesho ya Karibu Utalii Kusini la Mamlaka hiyo.
 Naye Mhandisi Astelius John amesema TAA imefanya maboresho makubwa kwenye viwanja vya ndege kikiwemo kiwanja cha ndege cha Iringa, ambapo kumefanyiwa upanuzi wa jengo la abiria na ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege.

“Tunaboresha viwanja vya ndege ili viweze kuwa bora na kuhudumia abiria wengi wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kukuza uchumi wa taifa na sasa kwa Kiwanja cha Ndege Iringa hii ni kutokana na maboresho ya jengo la abiria    kubwa ambalo lina uwezo wa kuhudumia  abiria wanaotumia kiwanja cha Iringa kutoka 35 kwa siku hadi kufikia 200,” amesema.


Kwa upande wake Afisa Usalama, Miyaga Juma ametoa ushauri kwa wananchi na wageni kutoka ndani na nje ya nchi watumie Kiwanja cha ndege cha Iringa, kwani kina usalama madhubuti, kazi inayofanywa na Maafisa usalama wenye kufuata miongozo mbalimbali ya kiusalama, aidha TAA imenunua mashine ya kisasa ya Ukaguzi ili kurahisisha ukaguzi na kuwepo kwa mfumo wa kamera (CCTV) ambao unahifadhi kumbukumbu za matukio hali inayoboresha usalama Kiwanjani.

Monday, 16 September 2019

Menejimenti ya TAA yapata mafunzo ya usimamizi wa Fursa na vihatarishi

 Menejimenti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), leo kwenye ukumbiwa mikutano wa Watu Mashuhuri wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wamepata mafunzo ya usimamizi wa fursa na vihatarishi kwa wadau wa nje na ndani ya taasisi yaliyokwenda sambamba na kuwapa ufahamu juu ya Viwango vya Kimataifa vya ISO 9001:2015; 14001:2015 NA 45001:2018 vinavyotolewa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO), mbele ni Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Ali Helal kutoka Kampuni ya Ascent Emirates ya Dubai. Mafunzo hayo yaliyohusisha Menejimenti ya TAA, na yataendelea tarehe 19 na 20 Septemba, 2019 kwa kuhusisha Mameneja na Mabingwa wa kusimamia mfumo (Champions).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama (wanne kulia), akisisitiza jambo kwenye mafunzo ya usimamizi wa fursa na vihatarishi kwa wadau wa nje na ndani ya taasisi iliyokwenda sambamba na kuvitambua viwango vya Shirika la Viwango la Kimataifa vya ISO 9001:2015; 14001:2015; na 45001:2018 iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha Menejimenti ya taasisi hiyo. Mafunzo hayo yametolewa na Ali Helal wa Kampuni ya Ascent Emirates ya Dubai (aliyesimama). Mafunzo hayo yaliyohusisha Menejimenti ya TAA, na yataendelea tarehe 19 na 20 Septemba, 2019 kwenye ukumbi wa VIP-JNIA kwa kuhusisha Mameneja na Mabingwa wa kusimamia mfumo (Champions).

Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Viwango wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Vedastus Fabian (wa pili kushoto waliokaa), akifafanua jambo kwenye mafunzo ya siku moja ya   usimamizi wa mafunzo ya usimamizi wa fursa na vihatarishi kwa wadau wa nje na ndani ya taasisi pamoja na kuvitambua viwango vya Shirika la Viwango la Kimataifa vya ISO 9001:2015; 14001:2015; na 45001:2018 yaliyotolewa na Mkuu wa Mafunzo wa Kampuni ya Ascent Emirates ya Dubai. Mafunzo hayo yaliyohusisha Menejimenti ya TAA, na yataendelea tarehe 19 na 20 Septemba, 2019 kwenye ukumbi wa VIP- JNIA kwa kuhusisha Mameneja na Mabingwa wa kusimamia mfumo (Champions).


Sunday, 15 September 2019

Wafanyakazi TAA Watakiwa Kufanya Kazi Kwa Bidii


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama (kushoto), akimkabidhi zawadi ya ngao, Theobald Benigius wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius  Nyerere (JNIA) katika sherehe ya kuwaaga Wastaafu baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria na taratibu za Utumishi wa Umma.

Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wametakiwa kuchapa kazi kwa bidii ili kurudisha hadhi ya taasisi hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi Julius Ndyamukama wakati akiwaaga wastaafu watatu wa mamlaka hiyo.

Hafla hiyo ilikuwa mahsusi kwa ajili ya kuwaaga wastaafu kutoka Idara ya Uandisi na Huduma za Ufundi ya Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA), ambao ni Mhandisi Theobald Benigius, Ernest Kivela na Bertha Kipenda, ambao wamestaafu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha akimkabidhi mmoja wa wastaafu wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa JNIA, Mhandisi Bertha Kipenda zawadi ya vifaa vya mazoezi katika hafla ya kuwaaga iliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.


Alisema kuwa juhudi, maarifa na upendo ndio vigezo vitatu, ambavyo ni chachu ya kuipandisha na kuirejesha kileleni taasisi hiyo, ambayo ilianza kupoteza hadhi mbele ya uso wan chi na jamii, tofauti na huko nyuma, ambako ilikuwa ikifanya vizuri zaidi.

Alisema kwa sasa hadhi ya taasisi hiyo imeshuka mbele ya uso wa nchi na kusababisha baadhi ya kazi ilizokuwa ikizifanya zamani, sasa kufanya na taasisi nyingine.

“Nashauri tupendane na tuchape kazi kwa bidii, kwani sura yetu kama TAA hapo katikati ilidorora kwani tumepoteza kazi nyingi, hivyo tukitaka kurudisha hadhi yetu kama itatakiwa kusukumana, tutafanya hivyo kwa lengo hilo, ingawa najua wapo ambao hawataki hivyo,” alisema.

Hatahivyo, amewashukuru watumishi wenzake kwa kumpokea vizuri tangu kuteuliwa kwake kuongoza taasisi hiyo takribani miezi sita iliyopita, ambapo amewataka kushirikiana zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama, akiongea na watumishi walioudhuria hafla ya kuwaaga watumishi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), waliostaafu hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Pia ameweka angalizo kwa Watumishi wote kuwa muda wote atakaokuwepo hapo kama Mkurugenzi Mkuu, atalazimika kuwasumbua na kuwasukuma, ili sura ya TAA iliyopotea, kurejea katika hali yake yazamani.

 “Tukitaka kurudisha hadhi yetu kama ilivyokuwa zamani hivyo itahusu tusukumane na kusumbuana kidogo nitaomba mnivumilie, lakini lengo likiwa ni kutaka kurudisha TAA ya zamani, ingawa najua wapo wasiotaka,” alisema.

Aliwapongeza wastaafu hao na kuwataka kendelea kufanya kazi huko waliko ili kuendelea kuziimarisha afya zao.

Kwa upande wake
Kaimu Meneja wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi Diana Munubi (kushoto), akimkabidhi zawadi picha ya ua Ernest Kevela (wa kwanza kulia) katika hafla ya kuwaaga wastaafu wa Idara hiyo iliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha alisema watumishi hao walikuwa na nidhamu kubwa na kufanya kazi kwa bidii, pasipo kuchoka wala kuwa na malalamiko, ambapo amewataka wengine waliobaki kuiga mfano huo uliotukuka.

Lakini, pia amewataka Wastaafu hao kuendelea kufanya mazoezi kwani wamekuwa wakifanya kazi ngumu wawapo katika kituo chao cha kazi cha JNIA.

Watumishi kutoka Idara na vitengo mbalimbali vya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiserebuka kwa kucheza muziki katika hafla ya kuwaaga watumishi wenzao wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi waliostaafu hivi karibuni.


Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi, Mhandisi Alex Kalumbete amesema wastaafu hao walikuwa na uvumilivu mkubwa katika utumishi wa umma kutokana na kazi ngumu walizokuwa wakifanya za kiuhandisi.

Kaimu Meneja Uhandisi na Huduma ya Ufundi JNIA, Diana Munubi amesisitiza upendo uendelee kuwepo baina ya watumishi kama vile wastaafu hao walivyokuwa wakiuenzi wakati wa utumishi wao wote wa umma.

Mmoja wa wastaafu hao, Bw. Theobald Benigius kwa niaba ya wenzake ameishukuru TAA kwa kuwezesha kufanya kazi vizuri hadi utumishi wao kukoma kwa kustaafu, na amewaomba watumishi wenzake kuwa wavumilivu na tabia njema kwani wataweza kustaafu vizuri
.