Monday 4 November 2019

Mwakyembe Azindua Kili Marathon 2020 Awataka Wanariadha wa Tanzania Kuchangamkia Zawadi


Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio za 18 za Kilimanjaro zitakazofanyika Machi mwakani,

Mwakyembe pia aliwataka wanariadha wa Tanzania kufanya maandalizi ya uhakika ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mbio hizo, ambazo ni kubwa zaidi hapa nchini na hushirikisha watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, ambazo zitafanyika mjini Moshi Machi mosi, 2020, mwakyembe alisema ni aibu kwa zawadi zote kwenda nje ya nchi, hivyo aliwataka wanariadha wa Tanzania kujiandaa vizuri ili kuhakiisha zawadi hizo zinabaki nchini.

Mwakyembe aliwapongeza wadhamini wa mbio hizo wakiongozwa na Kilimanjaro Premium, ambao hudhamini mbio za kilometa 42, Tigo (kilometa 21), Grand Malt (kilometa 5), ambazo ni mbio za kujifurahisha na hushirikisha watu wengi.

“Inatia moyo sana kuona kuwa Kilimanjaro Marathon sasa ina washiriki zaidi ya  11,000 kutoka nchi zaidi ya 56 kote duniani. Hili ni jambo zuri sana kwa taifa, kwani tunapata fedha za kigeni kutokana na matumizi yanayofanywa na wageni hawa nchini, ikiwemo utalii, “alisema.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, alitoa wito kwa washiriki wazalendo kuchangamkia zawadi zinazotolewa na Kilimanjaro Marathon badala ya kukimbilia kushiriki mbio za nje, ambazo zawadi zake ni ndogo.

 “Ni vizuri kwenda kupata exposure lakini tusiache zawadi nzuri nyumbani na kufuata hela ndogo huko nje wakati tunaweza kuzipata hapa hapa nchini, “alisema Mtaka.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, alisema tangu mashindano yaanze Kilimanjaro Premium Lager imewekeza hela nyingi sio tu kusukuma mauzo ambayo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini pia kutengeneza ajira na kuchangia uchumi kwa ujumla kupitia gharama za kuyatangaza, promosheni na masuala mengine ya kimasoko.

Naye Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema kampuni yake inajivunia kudhamini mbio za kilometa 21 kwa mwaka wa tano mfulululizo, ambayo ni sehemu ya mbio hizo. “Tunajivunia kuwa sehemu ya tukio hili kubwa ambalo linawaleta pamoja wanariadha wakubwa, “alisema.

Wadhamini wengine katika Kilimanjaro Marathon ni pamoja na Kilimanjaro Water, Barclays Bank, Simba Cement, TPC Sugar, Precision Air, Kibo Palace Hotel, Garda World Security, Keys Hotel na CMC Automobiles.

Kwa mujibu ya waandaaji wa Kilimanjaro Marathon-Wild Frontiers na Executive Solutions, usajili umeshaanza kwa mtandao kupitia www.kilimanjaromarathon.com.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na mwenyekiti na kaimu katibu mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Leodegar Tenga na Neema Msitha, kaimu msaijili wa michezo nchini, Mwita, Bodi ya Utalii na wadau wengine swa mchezo wa riadha.

No comments:

Post a Comment